Bandari Dar na rekodi ya kuhudumia meli kubwa

Dar es Salaam. Baada ya mageuzi ya huduma yaliyochochea ufanisi katika uendeshaji wa bandari, hatimaye Bandari ya Dar es Salaam imeanza kupokea na kuhudumia meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 300.

Hatua hiyo inakuja baada ya uwekezaji katika sekta ya bandari uliolenga kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa kituo kikuu cha kuhudumia shehena ya mizigo inayokwenda nchi jirani.

Uwekezaji huo ulifanywa kupitia mradi wa maboresho wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP).

Hivi karibuni, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia meli ya MV MYNY aina ya Post Panamax, yenye urefu wa mita 300 na uwezo wa kubeba tani 75,201, ikiwa imebeba shehena ya makasha 6,840.

Akizungumza baada ya meli hiyo kufunga gatini, Mkurugenzi wa Marini na Shughuli za Bandari, Abdullah Mwingamno, amesema hatua hiyo ni ushahidi wa uwezo mpya wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia meli kubwa za kisasa.

“Mafanikio haya ni matokeo ya maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali kupitia TPA. Tunapenda kuwahakikishia wateja na wadau wetu kwamba sasa Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa na za kisasa kwa ufanisi zaidi,” amesema Mwingamno.

Ameeleza, mbali na maboresho ya miundombinu, Serikali kupitia TPA imewekeza kwenye ununuzi wa mitambo ya kisasa ikiwemo Ship to Shore Gantry Cranes (STS), Rubber Tyred Gantry Cranes (RTG), Reach Stackers na Forklifts za kisasa.

Amesema mitambo hiyo itapunguza muda wa meli kukaa bandarini kwa kuongeza kasi ya upakuaji na upakiaji wa mizigo.

Katika maboresho hayo, kupitia mradi wa DMGP, amesema Serikali imeimarisha gati namba 1 hadi 7 kwa kuongeza kina kutoka mita nane hadi mita 14.5.

Lingine lililofanyika, amesema, ni eneo la kuhudumia mizigo limeongezwa, eneo la kugeuzia meli limeongezwa kina hadi mita 15 ili kuruhusu meli kubwa zaidi kuhudumiwa kwa ufanisi.

Lango la kuingilia meli, amesema, limepanuliwa na kuongeza kina chake ili kuruhusu meli zenye upana mkubwa kuingia bila changamoto

“Mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) unagharimu Sh1.118 trilioni, ambazo zinatokana na mkopo wa Benki ya Dunia, misaada ya wafadhili na mapato ya ndani ya TPA,” amesema.

Mradi huo, amesema, umehusisha pia ujenzi wa gati maalumu la kuhudumia meli za magari, kuimarisha gati za 8–11 kwa kuongeza kina kutoka mita 12 hadi 14.5, kuboresha mtandao wa reli ndani ya bandari na usimikaji wa mfumo wa umeme bandarini.

Meli kubwa zilizowahi kuhudumiwa

Agosti mwaka 2021, bandari hiyo ilipokea meli kubwa ya Tranquil Ace, yenye urefu wa mita 199.95 na upana wa mita 32.2. Meli hiyo ilifika bandarini ikiwa na magari 3,743.

Mei 2022, meli ya mizigo ya Meridian Ace ilifika bandarini ikiwa na magari 4,397. Ilikuwa rekodi mpya ya meli iliyobeba magari mengi kuwahi kusafirishwa kwa njia ya moja kwa moja kupitia bandarini hiyo.

Aprili mwaka 2022, meli nyingine kubwa ya magari, Frontier Ace, ilifika ikiwa na magari 4,041, ikionesha kwamba bandari iliendelea kuboresha uwezo wake wa kupokea meli kubwa zenye mizigo.

Januari mwaka jana, kwa mara ya kwanza, bandari hiyo ilipokea meli ya kitalii ya Norwegian Cruise Line Dawn, yenye urefu wa mita 294, ikiwa na watalii 2,210 na wafanyakazi zaidi ya 1,000.