City FC Abuja mabingwa Tanzanite Pre-Season International

MASHINDANO ya Tanzanite Pre-Season International yamehitimishwa leo Septemba 7, 2025 kwa City FC Abuja kuwa mabingwa.

City FC Abuja kutoka Nigeria, imetwaa ubingwa huo kufuatia ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Namungo ya Ruangwa mkoani Lindi.

Katika mchezo huo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, dakika tisini zilimalizika kwa timu hizo kushindwa kufungana.

Katika penalti, zile tano za kwanza kila timu ilipata tatu na kukosa mbili, baada ya hapo, Namungo ikakosa ya sita, City FC Abuja ikafunga na kutwaa ubingwa.

Waliokosa upande wa Namungo ni Abdulkarim Kiswanya, Abdulaziz Shahame na Fabrice Ngowi huku waliofunga ni Hebert Lukindo, Cyprian Kipenye na Rogers Gabriel.

Kwa City FC Abuja, waliokosa ni Sunday Oliseh na Oscar Otu, wakati Abiola Oyeyemi, Chijindu Okah, Imanuel Adayilo na Austin Ozowuru wakifunga.

Wakati huohuo, kwa upande wa tuzo binafsi, Kipa Bora ni Mussa Webilo kutoka Namungo, Mchezaji Bora ni Sunday Odongs wa City FC Abuja na Abulaziz Shahame wa Namungo ni Mfungaji Bora baada ya kutupia mabao manne.

Jumla ya timu kumi zikiwemo sita zitakazocheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026 ambazo ni Fountain Gate, Dodoma Jiji, Namungo, Tabora United, Tanzania Prisons na Coastal Union, zimeshiriki mashindano hayo yaliyoanza Agosti 31, 2025 na kuhitimishwa leo Septemba 7, 2025.

Timu hizo zilipangwa katika makundi matatu. Kundi A limeundwa na timu za Fountain Gate, Tabora United na Eagle FC kutoka mkoani Manyara.

Kundi B ni Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union, huku Kundi C kuna Namungo, JKU ya Zanzibar, City FC Abuja kutoka Nigeria na TDS iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa inaibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.