Dk Nchimbi: Wilaya zote nchini kuunganishwa kwa lami

Biharamulo. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo wanakwenda kuziuganisha wilaya zote nchini kwa barabara za kiwango cha lami.

Amesema hilo litawezekana iwapo, Watanzania watamchagua mgombea urais wa CCM,  Samia Suluhu Hassan kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kuendelea kusalia madarakani.

Dk Nchimbi amesema hayo jana Jumamosi, Septemba 6, 2025 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, akimwombea kura Samia, wabunge na madiwani wa chama hicho uliofanyika Uwanja wa CCM, Biharamulo, mkoani Kagera.

Dk Nchimbi amefanya mkutano huo mkoani humo akitokea Mkoa wa Geita. Kabla ya Geita alizisaka kura Shinyanga, Simiyu, Mara na Mwanza alipoanzia Agosti 29, 2025.

Wakati Dk Nchimbi akiwa amepita mikoa hiyo, Rais Samia amekwishafanya mikutano kwenye mikoa ya Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amesema Serikali ya CCM chini ya Rais Samia itahakikisha wilaya zote nchini zinajengwa kwa kiwango cha lami ikiwemo ya Biharamulo.

Tanzania Bara yenye mikoa 26, ina jumla ya wilaya 139.

Amesema hatua hiyo itachochea maendeleo ya wananchi na nchi kwani itawarahisishia kusafiri na kusafirisha bidhaa za kibiashara hivyo kufungua zaidi shughuli za kiuchumi na kijamii.

Pia, amesema mtandao wa barabara mbalimbali za Biharamulo nazo zitaboreshwa. Sekta za kimageuzi, zinazochochea maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla kuziboresha.

“Matumizi ya sayansi na teknolojia katika kukuza uchumi yatafanyiwa kazi kwa kasi ili mafanikio ya miaka mitano ijayo tuwe tumepiga hatua,” amesema Dk Nchimbi.

Awali, katika mkutano huo, Dk Nchimbi amesimikwa kuwa Katikilo ambaye ni msaidizi wa Chifu Mkuu, Rais Sami ambaye pia ndiye mgombea wa urais wa chama hicho.

Septemba 8, 2021 Samia, alisimikwa kuwa Chifu Mkuu wa Tanzania na kupewa jina la Chifu Hanganya.

Dk Nchimbi amewaambia wananchi wa Biharamulo kuwa ameajiandaa vyema kuwa msaidizi wa Rais Samia ili dhamira ya kuwatumikia Watanzania ifanikiwe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Wilaya ya Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma, Hamis Ally amewaomba wana CCM wa Biharamulo na nchi nzima kuzisaka kura za Rais Samia, wabunge na madiwani kwa ustaarabu.

“Twendeni tukaziombe kura  kistaarabu, siyo unakwenda kuomba kura kwa lugha zisizofaa. Kuna wenzetu unakuta yeye ni ACT Wazalendo, TLP, NCCR-Mageuzi na au Chadema mchana lakini usiku ni CCM na au mwili uko huko lakini moyo wake upo CCM,” amesema Ally.

Naye mbunge wa zamani wa Busega, Mkoa wa Simiyu, Dk Raphael Chegeni amesema Rais Samia amefanya kazi kubwa, miradi yote ya maendeleo iliyoachwa na mtangulizi wake, ameikamilisha kwa kiwango kikubwa ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere.

Dk Chegeni amewaomba wananchi wa ndani na nje ya Biharamulo Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kujitokeza kwa wingi kwenda kukichagua  Chama cha Mapinduzi (CCM), akisema kuwa  kimeonesha dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania.

Mwaka 2021 wakati Samia anaapishwa kuwa Rais, Bwawa hilo lilikuwa takribani asilimia 33 ya ujenzi wake na sasa limekamilika na uzalishaji wa umeme umeshaanza.

Samia aliyekuwa Makamu wa Rais aliapishwa Machi 19, 2021 kuwa Rais akichukua nafasi ya Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Dk Nchimbi na ujumbe wake leo Jumapili, Septemba 7, 2025 anaendelea kuzisaka kura mkoani Kagera ambapo atafanya mikutano minne akianza na Ngara, Kyerwa, Bukoba Vijijini na kumalizia Bukoba Mjini.

Katika mikutano ya leo, Dk Nchimbi atatumia usafiri wa Helikopta ili kumwezesha kufikia maeneo hayo ndani ya siku moja kutokana na jiografia ya maeneo hayo.

Endelea kufuatilia Mwananchi…