DK.SAMIA AAHIDI KUENDELEA KUSIMAMIA MAENDELEO YA VYAMA VYA USHIRIKA NCHINI

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Iringa

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameeleza kwa jina kina kuhusu mkakati wa Serikali kuhusu maendeleo ya vyama vya ushirika nchini.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Iringa wakati wa mkutano wake wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu, Mgombea Urais Dk.Samia amesema anatambua nafasi ya ushirika katika maendeleo ya kilimo nchini.

“Tumechukua hatua makusudi kufufua na kuimarisha uchumi ikiwemo kuanzisha benki ya ushirika na kuimarisha usimamizi kupitia tume ya maendeleo ya ushirika lengo kuwezesha vyama vya ushirika kupata mahitaji nafuu au mitaji nafuu.

“Kujitegemea na kujiendesha kibiashara kama ilivyo kwa chama cha iringa farmers cooperative union kilichoanzishwa mwaka 1993 ambacho ni moja ya vyama vikuu mkoani hapa.

“Mwaka huu 2025/26 chama hiki kinatarajia kusambaza pembejeo na mbolea ya ruzuku kwa wanachama wake.Tumewakuza wamekuwa kiasi ambacho sasa wanaweza kufanya hivyo.”

Ameongeza kuwa kutokana na jitihada za kutafuta masoko benki ya maendeleo ya kilimo kiasi cha shilongi bilioni moja , hivyo inawezekana vyama vya ushirika vikasimama vikatafuta mikopo vikasambaza pembejeo kwa wanachama wake .

“Wakanunua mazao kwa wanachama wake , wakatafuta masoko ndani na nje ya nchi ya mazao wanayolima lakini pia kujenga maghala ya kuhifadhia mazao yao huko ndiko tunakotaka kuelekea.

“Nataka niwahakikishie kwamba tumejipanga vyema kuvilea vyama vya ushirika ndani ya nchi yetu lengo ni kumuwezesha kufaidi nguvu na jasho lake huku ndiko kumuinua mkulima.”

Ameongeza kuwa la muhimu katika vyama vya ushirika wanalifanyia kazi kuhakikisha wana watu mahili wenye kuelewa jinsi ya kuongoza ushirika lakini pia matumizi ya tehama katika kuongeza uwazi hususan kwenye mahesabu mapato na matumizi ya ushirika.”Huko ndiko kunaleta vurugu mpaka ushirika unavurugika.”