DKT. SERERA AVUTIWA NA USHIRIKI WA NEMC KWENYE MAONESHO YA IATF

Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa namna ambavyo linatoa elimu kwa wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Barani Afrika yanayotambulika kama Intra African Trade Fair (IATF) yanayoendelea jijini Algiers nchini Algeria kuanzia Septemba 4-10, 2025.

Dkt. Serera ambaye ni Mkuu wa msafara wa Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Maonesho hayo, ametoa pongezi hizo alipofika Banda la Tanzania akiambatana na mwenyeji wake ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman S. Njalikai.

“Uchumi tunaoutaja ni Uchumi wa Viwanda, lakini Viwanda tunavyohitaji ni viwanda vinavyozingatia Uhifadhi wa Mazingira, hivyo basi NEMC kwa kuja hapa wanawaambia wawekezaji waje lakini yapo ya kuzingatia kuhusu Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira” amesema Dkt. Serera.

“NEMC inalo jukumu la kuendelea kutoa elimu na nilichopenda zaidi ni kwamba hakuna urasimu, nimeona hapa taarifa zote unaweza kuzisoma na kuzipata kupitia “QR Code” kabla hata ya kuja kuwekeza Tanzania, Na hapa niwapongeze sana NEMC kwa namna mnavyofanya kazi vizuri na muendelee hivyo kwani Mazingira ni uhai ni lazima tuyatunze ili yatutunze” Amesisitiza Dkt. Serera.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Imani S. Njalikai amezitaka Taasisi zinazoshiriki Maonesho hayo kuitumia fursa hii vizuri hasa katika maeneo ambayo Algeria inafanya vizuri kwenye sekta ya nishati ambayo ni pamoja na gesi, mafuta, mbolea na sekta ya madawa (pharmaceutical) ambayo ni pamoja na mafunzo kwenye maeneo hayo.

NEMC ikiwa ni moja ya Taasisi inayoshiriki Maonesho hayo ikiwakilishwa na Mhandisi Mkuu, Peres Ntinginya na Afisa Uhusiano na Mawasiliano, Bw. Tajiri Kihemba. Taasisi nyingine zinazoshiriki ni pamoja na TANTRADE ambao ni waratibu kwa upande wa Tanzania, TMDA, FCC, TISEZA, PURA, TFS, ZIPA

.