DOYO HASSAN DOYO: Guru wa madini ya viwandani anayeusaka urais 2025

Dar es Salaam. Januari mosi, 1974, ilikuwa Jumanne. Ulimwengu ulipokea taarifa za mafanikio ya kisayansi baada ya chombo cha kiroboti kinachoitwa Mariner 10 kuwasili kwenye sayari ya Zebaki (Mercury), hivyo kuchagiza mafanikio makubwa ya uvumbuzi wa anga na maisha ya sayari.

Mariner 10 ni chombo kilichobuniwa na kuundwa na wanasayansi wa Shirika la Sayansi ya Anga Marekani (NASA). Chombo hicho ndicho kilichotumika pia kupeleleza sayari ya Zuhura (Venus).

Saa 6:00 usiku, tarehe ilibadilika. Ni mwaka mpya tayari, dunia ilihama kutoka mwaka 1973 na kuingia 1974. Tanzania, sawa na mataifa yote yenye kufuata kalenda ya Gregory, ilisherehekea mwaka mpya.

Kijiji cha Misimu, Kata ya Misimu, Wilaya ya Handeni, Tanga, kaya moja iliupokea mwaka katika sura tofauti. Mume, Mohammed Doyo, na mkewe, Zaina Jira, walikuwa kwenye matarajio ya mtoto. Alfajiri ya Januari mosi, 1974, alizaliwa mtoto wa kiume.

“Anaitwa Hassan,” baba, Mohammed Doyo, alimpa mwanaye jina.

Mtoto Hassan alikua salama. Januari 1983, akiwa na umri wa miaka tisa, aliandikishwa kuanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Misimu, wilayani Handeni, Tanga. Desemba 1984, Hassan akiwa amemaliza mwaka wa pili darasani na akiwa likizo ya mwisho wa mwaka akisubiri Januari 1985 ili aingie darasa la tatu, alishuhudia tukio lililojenga uelekeo wa maisha yake.

Siku hiyo, mama yake mzazi, Zaina, alikamatwa na maofisa wa kodi akidaiwa Sh200 ya kodi ya maendeleo, ambayo ilikuwa maarufu kama kodi ya kichwa wakati huo. Zaina alipandishwa kwenye karandinga pamoja na wananchi wengine ambao hawakuwa na uwezo wa kulipa kodi hiyo.

Ilipofika jioni, baba yake Hassan, Mohammed, alikwenda kumkomboa mkewe (Zaina). Alilipa faini ya Sh270 ndipo akamchukua na kurudi naye nyumbani. Hilo ndilo tukio lililomsababisha Hassan ajiapize kuwa mwanasiasa, ili yaliyomtokea mama yake yasiwatokee Watanzania wengine.

Alikula yamini kuwa mwanasiasa, kwa sababu kitendo cha mama yake kukamatwa alikiona kilikuwa cha uonevu. Kuanzia akili yake ya kitoto hadi kukua kwake, amekuwa akiamini kuwa nchi haikuwa sawa kuendeshwa kwa kuwakamata wananchi na kuwatoza Sh200 za kodi ya kichwa.

Hassan ndiye Doyo Hassan Doyo, ambaye ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, kwa tiketi ya chama cha National League for Democracy (NLD). Wazazi wake walimwita Hassan na nyaraka zake za kuzaliwa na shule zilimtambulisha kama Hassan Mohammed Doyo.

Hata hivyo, alipojiingiza rasmi kwenye siasa Februari 25, 1993, alitaka atambulike kama Doyo Hassan Doyo badala ya Hassan Mohammed Doyo. Kwa hivyo, alikwenda mahakamani, akaapa na kuanza kutambulika kisheria kwa jina hilo.

Januari 1983, Doyo alijiunga na Shule ya Msingi Misimu iliyopo Handeni, Tanga. Alisoma hapo kwa miaka saba hadi alipohitimu elimu ya msingi mwaka 1989. Baada ya hapo, alihamia Dar es Salaam na kujiunga na Shule ya Seminari ya Kiislam ya Masjid Quba kuanzia mwaka 1990 kabla ya kuhitimu mwaka 1993.

Mwaka 1998, Doyo alijiunga na Chuo cha Dar City kusomea Mawasiliano ya Umma, Utangazaji na Uhusiano wa Umma. Alianza ngazi ya cheti, kisha diploma. Safari hiyo ya elimu ilimchukua miaka mitatu (1998 – 2001).

Mwaka 2003, Doyo alihudhuria kozi ya Mikakati ya Uchaguzi, Hamburg, Ujerumani. Mwaka 2004, alisoma kozi ya Usalama wa Nchi Kupitia Viongozi wa Siasa katika Chuo cha Ulinzi wa Taifa (kozi ya 17). Mwaka 2011, alisomea Ujengaji wa Migodi na Utambuzi wa Miamba katika Chuo cha Madini, Dodoma.

Februari 25, 1993, akiwa na umri wa miaka 19, alianza safari yake ya kisiasa alipojiunga na Chama cha Wananchi (CUF). Anasema kadi yake ya uanachama alikabidhiwa mkononi na Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, James Mapalala.

Doyo alidumu CUF kwa miaka 17, miezi 10 na siku 10. Januari 4, 2011, alifukuzwa uanachama baada ya kuonekana anakinzana na msimamo wa viongozi wa juu wa chama hicho, hasa Profesa Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti) na Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu).

Ndani ya CUF, alianza kama mwanachama wa kawaida kijana, kisha kiongozi wa ngazi za chini wilayani Handeni, kabla ya kupanda hadi kuwa Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Handeni. Nafasi hiyo aliishikilia kwa miaka 15 (1996 – Januari 4, 2011).

Kipindi chote akiwa Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Handeni, pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Uongozi CUF. Hivyo, alikuwa sehemu ya jopo la juu la maamuzi kwa miaka 15.

Doyo, alifukuzwa CUF akiwa pamoja na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, mwaka 2005 – 2010, Hamad Rashid Mohamed. Hata hivyo, Hamad, alibaki CUF, baada ya kuomba zuio la Mahakama la kulinda uanachama wake hadi kesi ya msingi ya kupinga kufukuzwa kwake, isikilizwe.

Wakati Hamad akibaki CUF, na akiendelea kuwa mbunge kupitia chama hicho kwa ulinzi wa Mahakama, Doyo alihamia na kuasisi chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) ambacho kilipata usajili wa kudumu Agosti 22, 2012.

Baada ya hapo, Doyo aliteuliwa kuwa mlezi wa ADC Kanda ya Kaskazini (2012), Mkurugenzi wa Habari wa ADC (2013 – 2014), Naibu Katibu Mkuu wa ADC, Bara (2014 – 2016), Katibu Mkuu wa ADC (2016 – 2024).

Mwaka 2024, aligombea uenyekiti wa taifa wa ADC lakini akashindw, akajiweka kando kidogo, kabla ya kukaribishwa NLD na kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu.

Mkutano Mkuu wa Taifa wa NLD mwaka 2025 ulimteua kuwa mgombea urais kwa kura nyingi, huku Chausiku Khatib Mohamed akipitishwa kuwa mgombea mwenza. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ilimteua Doyo kupeperusha bendera ya NLD, katika mapambano ya kuusaka urais.

Katika msako wa urais, Doyo anabeba ajenda sita ambazo ni ajira, afya, elimu, miundombinu, kilimo na rushwa. Mkazo wake katika ajira ni kutumia rasilimali zilizopo kama chanzo cha fursa za ajira. Pia anaahidi kuikabili rushwa na kufuta mfumo wa elimu wa sasa ambao anadai hauna tija.

Ahadi yake ni kuwa akiingia madarakani, atahakikisha anatumia ipasavyo rasilimali zilizopo ili kuwapa wananchi maendeleo ya haraka, vilevile kutokomeza tatizo la ajira nchini.

Kingine, Doyo anaahidi kuikabili na kuishinda rushwa pamoja na vitendo vyote vya ufisadi.

Doyo anasema kama ilivyoandikwa kwenye Ilani ya NLD, ndivyo itakavyokuwa, kwamba atakaposhinda urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali atakayoiongoza, itaanzisha Kituo cha Utafiti wa Kisayansi.

Anaahidi kufuta mfumo wa elimu wa sasa ambao amedai haumsaidii mhitimu, kisha ataleta mpya utakaokuwa na tija.


Kati ya mwaka 1996 – 2000, Doyo anakiri kuwa aliteseka sana kisiasa. Hakuwa na kipato cha uhakika, alitembea umbali mrefu kueneza chama na kufanya kampeni. Alipokuwa hana uwezo wa kuhudumia familia, alimrudisha mkewe, Lina, nyumbani kwa wazazi wake ili ajipange upya.

Anasema kwamba alijiingiza kwenye siasa bila kuwa na shughuli yenye kumpa kipato cha uhakika, matokeo yake aliiumiza familia yake.

Kwa sasa, anasema maisha yanamwendea vizuri. Amejipatia umaarufu kama guru wa madini ya viwandani, akimiliki migodi 54 na kuajiri vijana 400. Anaeleza kwamba watu wengi wanamwona akipambana kwenye siasa wanadhani hiyo ndiyo sifa ya pekee, lakini jumuiya ya wachimbaji wa madini, inamtambua kama “Mzee wa Madini ya Viwandani”.

Pia ni mkulima mkubwa wa katani na mazao ya chakula. Mwamko na uzoefu wake kwenye uchimbaji wa madini na kilimo, ndivyo vinampa ari ya kuona kwamba anaweza kuifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa nchi yenye maendeleo makubwa, endapo ataaminiwa na kuchaguliwa kuwa Rais.

Katika harakati zake za kisiasa, Doyo amegombea nafasi mbalimbali, udiwani Kata ya Misima mwaka 2005, kwa tiketi ya CUF. Ubunge jimbo la Handeni kupitia CUF mwaka 2010 na kwa tiketi ya ADC mwaka 2015.

Mwaka 2020, alisimama Handeni Vijiji kuwania ubunge kwa mwavuli wa ADC. Majaribio yote hayo, Doyo hakufaulu. Pamoja na hivyo, haijamzuia kuupigia hesabu urais mwaka 2025.

Doyo ni mume wa wake wawili—mke mkubwa, Lina Burhani Kilo, anaishi Tanga, na mke wa pili, Halima Rajab Msumari, anaishi Dar es Salaam. Kutokana na waka zake kuwa mikoa mwili tofauti, Doyo amekuwa mkazi wa Tanga na Dar es Salaam kwa wakati mmoja.

Ana watoto watano, wa kwanza Fahdi, ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha IFM, Dar es Salaam, akisomea Shahada ya Usalama wa Mtandao. Fahdi anafuata nyayo za baba yake, kwani anagombea ubunge Jimbo la Kawe 2025.

Mtoto wa pili, Ibad, sasa yupo kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), baada ya kupata stashahada ya Maendeleo Vijijini kutoka Chuo cha Mipango, Dodoma.

Mwingine ni Zakati, anayesoma biashara katika Shule ya Wali Ul Asr, Kibaha, Pwani.

Awena ni mtoto wa nne, yupo darasa la tano na wa mwisho, Ummy anayesoma darasa la pili.

Doyo anasema familia yake pia ina asili ya siasa, kwani baba yake, Mohammed Doyo, aliwahi kuwa mjumbe wa Serikali ya Mtaa na mjumbe wa CCM, Kijiji cha Misimu, Kata ya Misimu, Kitongoji cha Masuini, Wilaya ya Handeni, Tanga.