Enekia Lunyamila, akiri Mexico ngumu

FC Juarez inayoshiriki Ligi Kuu ya wanawake Mexico, juzi ilikubali kichapo cha mabao 3-2 dhidi ya Pachuca, ukiwa ni mchezo wa tatu kupoteza kwenye mechi 10 walizocheza za ligi.

Chama hilo, ambalo wanatumikia Watanzania wawili, Julietha Singano na Enekia Lunyamila, matokeo hayo yameifanya ishuke hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo kutoka ya saba, ikiwa na pointi 15.

Kwenye mechi hiyo, beki wa kati, Singano alicheza kwa dakika 89 na baadaye akapumzishwa, kwa upande wa Lunyamila aliingia katika dakika ya 68.

Hadi sasa, Julietha Singano ndiye beki aliyecheza mechi zote za ligi na amekuwa na mwendelezo mzuri tangu aliposajiliwa mwaka 2022 akitokea Simba Queens.

Huu ni msimu wa nne mfululizo kwa beki huyo wa Twiga Stars kuichezea timu hiyo, akiingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja mbele ya nyota kibao kutoka Ulaya.

Lunyamila, ambaye ni msimu wake wa pili kuichezea Ligi ya Mexico, awali aliitumikia Mazatlan ambako alicheza mechi 16, akifunga mabao sita na kuisaidia timu hiyo kumaliza katika nafasi ya 15 kati ya 18 kwenye msimamo wa ligi.

Hata hivyo, bado hajaonyesha makali yake akiwa na chama la Mtanzania mwenzake, Singano ambaye analimudu eneo la beki kutokana na kiwango bora anachoendelea kukionyesha na kuishika nafasi hiyo.