Hatari ya wazazi kubagua watoto

Katika kila familia, watoto ni zawadi ya kipekee yenye thamani isiyo na kifani.

Kila mtoto huja duniani akiwa na vipaji, ndoto, na uwezo wa kuchangia kwa namna yake katika jamii. Hata hivyo, hali ya ubaguzi wa watoto imekuwa changamoto inayokua kwa kasi katika jamii nyingi. Wazazi na walezi, kwa kujua au kutojua, huonyesha upendeleo kwa baadhi ya watoto huku wakidharau au kuwanyima wengine haki ya upendo, usikivu na msaada.

Hii ni hatari kubwa ambayo husababisha madhara ya muda mfupi na muda mrefu kwa watoto, familia na jamii kwa ujumla.

Ubaguzi wa watoto ni hali ambapo mzazi au mlezi anampendelea mtoto mmoja au baadhi ya watoto kuliko wengine katika familia.

Upendeleo huu unaweza kuonyeshwa kwa njia mbalimbali kama vile kumpatia mtoto mmoja vitu vizuri zaidi, kumtetea kila mara hata anapokosea, kumpa muda zaidi wa mazungumzo au mapenzi, au kumnyima mwingine nafasi ya kujieleza au kushiriki shughuli za familia.

Wengine hupendelea mtoto kwa sababu ya jinsi, mwonekano wa kimwili, uwezo wa kitaaluma, tabia au hata hali ya kiafya.

Tatu Hamidu mkazi wa jijini Mwanza, mama wa watoto watano, anasema amekuwa akiwatendea haki watoto wake wote, japo anakiri kuwa yule wa pili anampenda zaidi, lakini hajafikia hatua ya kuwa mbaguzi kwa wote.

“Wakati mwingine nashindwa kujizuia hasa nikiwa nawapa zawadi lazima yeye nimpe kikubwa. Mwanzo nilipojifungua nilijua nampendelea kwa sababu ni mdogo lakini nilipopata wadogo zake nikajua ile siyo sababu kuna nyingine,” anasema.

Anaongeza: “Najitahidi kuwatendea sawa, wakati mwingine naweza kumtuma mdogo wake au kaka yake ukasikia anasema mama unampenda zaidi Joan, najisikia vibaya nawambia nawapenda wote ila ukweli ni kwamba najisahau. Wakati mwingine hata nikiwa nawaadhibu wote naanza na wengine, hadi nimfikie yeye hasira zimeisha kwa hiyo kama fimbo zilikuwa tatu tatu najikuta namchapa mbili namuacha… siyo kama napenda ila inatokea tu.”

Sababu zinazochangia ubaguzi wa watoto ni nyingi. Mojawapo ni mila na desturi, ambapo baadhi ya jamii huamini kuwa mtoto wa kiume ana thamani zaidi ya wa kike.

Aidha, baadhi ya wazazi huathiriwa na matarajio yao binafsi na hivyo kumpendelea mtoto anayekidhi matarajio hayo.

Wengine huathiriwa na hali ya kifamilia kama vile mtoto aliyepatikana kwa tabu kubwa au kwa muda mrefu anapewa mapenzi ya ziada.

Pia hali ya kiuchumi, elimu ya wazazi, na malezi waliyopewa wao wenyewe, vinaweza kuchangia kuendeleza ubaguzi huu.

Hatari za ubaguzi ni nyingi na zenye madhara makubwa. Kwanza, mtoto anayehisi kutengwa hukua akiwa na majeraha ya kisaikolojia.

Anaweza kujiona hana thamani, asiyehitajika, na kushindwa kujiamini. Hali hii inaweza kuchangia matatizo ya afya ya akili kama msongo wa mawazo, huzuni sugu au hata matendo ya kujidhuru.

Pili, watoto wanaobaguliwa hukua wakiwa na chuki, hasira au uhasama kwa wale waliopendelewa. Hii husababisha migogoro ya kudumu kati ya ndugu na kuvunjika kwa uhusiano wa kifamilia.

Watoto hao wanaweza pia kukuza tabia ya uasi, kushiriki katika makundi hatarishi au kuwa na tabia zisizofaa kama vile wizi, matumizi ya dawa za kulevya au ulevi.

Tatu, mtoto anayependwa kupita kiasi naye huathirika. Anaweza kukua akiwa mzembe, mwenye kiburi, au asiyejali wengine.

Anaweza kutojifunza maadili muhimu ya maisha kama heshima, uvumilivu, au huruma kwa wengine. Hali hii humletea matatizo anapoanza kuishi au kufanya kazi na watu wengine nje ya familia.

Athari kwa familia na jamii

Ubaguzi wa watoto hauathiri tu watoto binafsi bali pia familia nzima. Familia hupoteza mshikamano na upendo wa kweli kati ya wanandugu.

Uhusiano wa baadaye huwa wa mashaka, chuki na visasi. Watoto wanaobaguliwa huacha kusaidiana wanapokuwa wakubwa, jambo linaloathiri ustawi wa familia.

Katika jamii, watoto waliobaguliwa na kulelewa katika mazingira ya upendeleo hukua wakiwa watu wasiojiamini au wasio na maadili.

Wengine hukua wakiwa watu wakorofi, wepesi wa kuchukia, au watu wa matatizo. Hii huathiri maendeleo ya kijamii kwa kupunguza idadi ya watu wenye mchango chanya katika jamii.

Ubaguzi pia huendeleza mzunguko wa ubaguzi kwa vizazi vijavyo, kwani mtoto aliyebaguliwa anaweza naye kubagua watoto wake kwa njia ile ile.

Ni muhimu wazazi na walezi watambue kuwa kila mtoto ana nafasi ya kipekee na umuhimu mkubwa. Watoto hawapaswi kulinganishwa wala kupimwa kwa mizani ya upendeleo.

Kila mtoto ana vipaji vyake, udhaifu wake na njia yake ya kuonyesha upendo au kuelewa mazingira. Kila mmoja wao anahitaji upendo wa dhati, uelewa na msaada ili aweze kukua katika hali bora ya kiakili, kihisia na kimwili.

Kuthamini kila mtoto kunajenga msingi wa familia imara. Mtoto anayejua kuwa anapendwa bila masharti hukua akiwa na heshima, kujiamini, na kuwa na mtazamo chanya wa maisha.

Familia yenye mshikamano na usawa huandaa kizazi chenye matumaini, maadili na uwezo wa kujenga taifa bora.

Wazazi wanapaswa kuwa makini na namna wanavyowatendea watoto wao. Kujitathmini mara kwa mara na kujiuliza kama wanawatendea watoto wote kwa haki, ni hatua ya kwanza muhimu.

Pia wazazi wanapaswa kujifunza kuelewa mahitaji ya kipekee ya kila mtoto bila kuhukumu au kulinganisha.

Zaidi ya yote, jamii nzima inapaswa kuelimishwa juu ya athari za ubaguzi na umuhimu wa usawa katika malezi ya watoto.

Shule, makanisa, misikiti na vikundi vya kijamii, vina jukumu la kuhamasisha wazazi na walezi kuacha ubaguzi na kuwalea watoto wote kwa haki.

Ubaguzi wa watoto ni sumu taratibu inayoathiri kizazi na taifa kwa ujumla. Ili kuwa na familia zenye upendo, watoto wenye afya ya akili, na jamii iliyojaa maadili na mshikamano, ni lazima kila mtoto athaminiwe.

Wazazi na walezi wanapaswa kuelewa kuwa kila mtoto ana umuhimu wake, hivyo anastahili mapenzi, msaada, na nafasi ya kustawi.

Hakuna mtoto aliye bora kuliko mwingine, kwani kila mmoja ni hazina isiyofanana na nyingine, na anatakiwa kutunzwa kama dhahabu. Kila mtoto ni thamani, kila mtoto anahitaji kuthaminiwa.

Shekh wa Msikiti wa Rahman, uliopo Buhongwa, jijini Mwanza, Ibrahim Suleyman, anasema: “Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, kuwapenda watoto ni ibada na ni wajibu wa kila mzazi kuwa kielelezo cha upendo na haki, ili kujenga familia yenye mshikamano na malezi bora, kubagua watoto kuna sambaratisha na kujenga chuki.”

Anaongeza; “Mtume (Rehma na amani zimshukie) alisema mcheeni Allah, muwe waadilifu kwa watoto wenu. Ubaguzi kwa watoto unaweza kusababisha chuki, uhasama kati ya ndugu na hata kupoteza heshima ya mzazi machoni mwao. Wazazi wanahimizwa kuonyesha mapenzi na kuwapa watoto zawadi kwa haki, na iwapo motisha ya zawadi inatolewa kwa mtoto mmoja kwa sababu ya bidii yake, ni vyema kuwatia moyo wengine bila kuwadharau.”

Naye Mchungaji wa Kanisa la SDA, Marco Mligwa, anasema biblia inakemea ubaguzi kwa watoto, kwani mafundisho yake yamejaa upendo. 

“Mfano lile neno linalosema mpende jirani yako kama nafsi yako. ..jirani yako ni nani? Jirani yako ni mtu yeyote unayekutana naye na kuhitaji huduma yako.Ni kosa kubwa mzazi kuzaa watoto wake halafu anaonesha mapenzi kwa mtoto mmoja,” anaeleza.

Anaongeza: “Kwa mfano, kwenye familia ya Yacobo tunaweza tukaona ilileta madhara makubwa saba kwa sababu Yacobo alimpenda sana Yusuph kuliko watoto wengine, kitendo kilichowafanya wamchukie ndugu yao na kupanga mbinu za kumuua. Kwa mfano Yacobo alimshonea Yusuph kanzu nzuri lakini watoto wengine hakuwahi kuwafanyia jambo zuri kama lile. Ilitokea tu Mungu aliingilia kati hakuuawa.”