Mwanza. Mgombea ubunge wa Ilemela kwa tiketi ya chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Shaban Itutu, amesema akiingia madarakani yeye na chama chake watafanya mapinduzi makubwa kuboresha maisha ya Watanzania, ikiwemo kushusha gharama za gesi ya kupikia, kutatua changamoto ya maji, kujenga uwanja wa soka mkoani Mwanza na kupambana na ufisadi na rushwa.
Itutu amesema hayo leo, Jumapili, Septemba 7, 2025, wakati akiomba kura kwa wakazi wa Ilemela katika viwanja vya stendi ya magari Pasiansi, wilayani Ilemela, Mkoa wa Mwanza, ambapo chama hicho kimezindua kampeni zake za urais.
Amewaomba wananchi wamuamini na kumpa nafasi huku akiahidi chama hicho kuuza mtungi wa kilo 25 ya gesi kwa Sh3,000 na kuondoa ushuru usiokuwa na tija kwa wavuvi.
“Mimi ni kijana wenu, hao wenzangu walioniamini siyo kwa bahati mbaya, wananiamini kwa sababu wanaamini Itutu anaweza kupeleka chama hiki mbele. Naomba mnipeleke bungeni nikapambane na hao majangili wa ufisadi,” amesema Itutu.
Ameongeza: “ADC tukiingia madarakani, mtungi wa gesi wa kilo 25 tutauza Sh3,000, kwa sababu gesi tunayo ni watu tu ndiyo wamekosa fikra. Watanzania hawa wanateswa na umaskini, lakini wangekuwa na maisha bora zaidi ya haya.”
Itutu, ambaye ni Mwenyekiti wa ADC Taifa, amewaomba wananchi kufanya maamuzi sahihi kwa kuchagua wagombea wa chama hicho ili kuwakomboa kwenye umaskini na kifungo cha fikra walichofungwa na chama tawala.
“CCM nawaomba Jimbo la Ilemela wasahau kwa sababu hapa hawana chao, hawana mgombea anayeweza kusimama. Mimi nikiwa washindi, lakini wenzangu wa vyama vya upinzani wasiihangaike. Tuchagueni mimi na mgombea urais tukaondoe shida hizi.
“Ilemela fumbukeni, msifumbwe akili na macho. Nchi yetu hakuna mtu angekuwa maskini kama CCM Mungu angewapa uwezo wa kufikiri vizuri. Nchi ambayo Mungu ameijalia rasilimali za kila aina, tukiingia Ikulu hakuna msaada wa mzungu; nchi inajitosheleza kwa kila kitu,” amesema.
Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Mwalimu Hamad Aziz, amesema chama hicho kimeamua kuzindua kampeni zake katika Jimbo la Ilemela kwani ndipo ngome yao na nyumbani kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Shaban Itutu.
“Tumefanya hapa mkutano wetu kwa sababu kuu mbili, kwanza, ndipo Mwenyekiti wetu Taifa amezaliwa na kukulia hapa, pili pia ni mgombea wa ubunge wa jimbo hili la Ilemela,” amesema Aziz.
Amesema chama hicho kinataka kuhakikisha utawala wa muda mrefu wa CCM unafika mwisho na kuwaondolea wananchi maumivu kwa kuhakikisha wanafaidika na rasilimali zilizopo nchini.
“Sisi ADC tunataka uchaguzi huu uwe mwisho wa utawala wa CCM. Sote tuseme inatosha, maisha yamekuwa magumu kutokana na utawala mbovu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),” amesema Katibu huyo.
Makamu Mwenyekiti wa ADC, Hassan Mvungi, ameshangazwa na changamoto ya maji katika Jiji la Mwanza huku akiahidi kuwa chama chao kitalimaliza tatizo hilo na kuwaomba wakazi wa Ilemela kumchagua Shaban Itutu kuwa mbunge wa jimbo hilo.
“Nasikitika sana kusikia eti Mwanza kuna changamoto ya maji. Hii ni aibu, maji yanatoka hapa yanakwenda mikoa mbalimbali, lakini Mwanza ina shida ya maji. Ifike mahala tuseme inatosha, CCM itupishe.
“Itutu anatosha, Ilemela tumechoshwa na bunge la ndiyo mzee. Haiwezekani miaka 60 ya utawala, leo jiji kubwa kama Mwanza lina shida ya maji, na hadi leo mnaendelea kuchagua wabunge wanaokwenda kugonga meza bungeni. ADC tunasema hapana,” amesema.