HADI sasa mshambuliaji kinda wa JKT Queens, Jamila Rajabu anashikilia rekodi ya kufunga hat-trick kwenye michuano ya CECAFA kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake, baada ya chama lake kuitandika JKU mabao 5-0.
Rekodi hiyo inamfanya kuanza kujiwekea nafasi ya kukitafuta kiatu cha ufungaji bora ambacho hadi sasa kinashikiliwa na Fazila Ikwaput wa Kampala Queens.
Kinda huyo tangu amepewa nafasi na kocha wa zamani wa JKT Queens, Ester Chabruma amekuwa kwenye kiwango bora, msimu uliopita alicheza mechi 10 za Ligi Kuu akifunga mabao sita.
Kama atanyakua kiatu msimu huu itakuwa mara ya kwanza kwa timu kutoka Tanzania, nyota wake kubeba tuzo hiyo licha ya misimu minne kushiriki kwenye mashindano hayo.
Mchezaji wa zamani wa CBE, Loza Abera ndiye anashikilia rekodi ya kuchukua kiatu hicho mara nyingi, akinyakua mara mbili na mara moja akiishia nafasi ya pili kwenye ufungaji.
Msimu wa kwanza wa mashindano hayo 2021 ambayo yalifanyika Kenya na Vihiga Queens kunyakua ubingwa, Abera alikuwa mfungaji bora akiweka kambani mabao 13, mwaka uliofuata akafunga 11, mwaka 2023 mabao matano mbele ya Ikwaput aliyeweka nane.
Kama Jamila ataendelea kupata nafasi ya kucheza na kufunga basi huenda hatua ya makundi akafikia mabao ya Senaf Wakuma aliyekuwa mfungaji bora msimu uliopita akiweka kambani mabao sita hivyo ili aifikie yamebaki matatu.