Jipya lingine la Fadlu hili hapa

KWA mashabiki huko mitaani tambo ni nyingi, lakini katika kikosi cha Simba, mambo yanaendelea kusukwa taratibu, kwani timu iko kambini kujiwinda na Simba Day wiki ijayo, huku uongozi mpya nao ukiweka mambo sawa kwa ajili ya kujipanga na msimu mpya wa mashindano.

Lakini, katikati ya yote hayo, kocha wao, Fadlu Davids anaendelea kutesa tu msimbazi akifikisha siku 427 tangu alipopewa mikoba ya kuinoa timu hiyo na habari zikufike kwa sasa anafukuzia rekodi ya Patrick Aussems ya kudumu muda mrefu zaidi klabuni hapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Fadlu, raia wa Afrika Kusini, alichukua mikoba Julai 5, 2024, akirithi nafasi iliyoachwa na Abdelhak Benchikha aliyedumu siku 149 (sawa na miezi mitano) kabla ya kuachana na Wekundu wa Msimbazi na tangu wakati huo kocha huyo mwenye mwaka mmoja na miezi miwili Simba, ameonyesha anaweza kuifikisha timu hiyo katika nchi ya ahadi kiasi cha kuendelea kuaminiwa kwa ajili ya msimu mwingine kulingana na kile alichofanya wakati ambao kikosi hicho kinajenga timu upya.

Licha ya hilo, Fadlu aliipeleka Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, ingawa alikumbana na maumivu ya kupoteza mbele ya RS Berkane kutoka Morocco kwa mabao 3-1.

Katika Ligi Kuu Bara alimaliza nafasi ya pili nyuma ya Yanga, jambo lililompa changamoto mpya ya kurejea kwa nguvu zaidi msimu huu.

Katika miaka 10, Aussems ndiye aliyekaa muda mrefu zaidi katika kikosi hicho (siku 499) sawa na mwaka mmoja na miezi minne na nusu na kocha huyo Mbelgiji aliiongoza Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kung’olewa na TP Mazembe kwa mabao 4-1.

Baada ya msimu huo wenye mafanikio, Aussems alipewa mkataba mpya wa mwaka mmoja msimu wa 2019/20, ikiwa ni ishara ya uongozi wa Simba kuthamini mchango wake. Hata hivyo, Novemba 2019, klabu hiyo ilithibitisha kuachana naye kwa makubaliano ya pande mbili hatua iliyoashiria mwanzo wa zama mpya za kusaka kocha atakayejenga uimara wa timu wa muda mrefu.

Katika historia ya hivi karibuni ya Simba kumekuwa na mzunguko mkubwa wa makocha, lakini kwa sasa huenda Fadlu akafikia au hata kuvuka rekodi ya Aussems endapo ataendelea kufanya vizuri. Kwa jumla, kocha aliyeweka rekodi kubwa zaidi ya kudumu Simba tangu 2000 ni Patrick Phiri.

Kocha huyo raia wa Zambia aliiongoza Simba kuanzia 2009 hadi 2011 akidumu kwa siku 830 (sawa na miaka miwili na miezi mitatu) – rekodi ambayo hadi sasa haijavunjwa. Phiri anabaki kuwa mfano wa kocha aliyepewa muda wa kutosha kujenga kikosi cha ushindani katika klabu hiyo.

Akizungumzia suala la makocha kudumu katika timu, kocha wa zamani wa Gwambina na Mtibwa Sugar, Mohamed Badru alisema ni vigumu kwa kazi zao kuwa na uhakika wa kukaa sehemu moja kwa muda mrefu kwa sababu lolote linaweza kutokea, lakini kwa Fadlu ni muhimu aendeleze kile ambacho amefanya katika msimu wake wa kwanza.

“Amefanya kazi nzuri pamoja na kwamba ulikuwa msimu wake wa kwanza. Simba ni timu ya mataji, kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha anawapa ubingwa wowote msimu huu, hilo linaweza kumfanya kuendelea kusalia zaidi ikiwemo kuwafunga watani zao (Yanga) ambao wamekuwa wakiwasumbua,” alisema.

Kwa upande wake, Credo Mwaipopo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga, alisema:

“Hakuna kitu kingine ambacho kinaweza kumfanya kocha akasalia kwenye timu kwa muda mrefu zaidi ya matokeo.

“Kwa wenzetu Ulaya ni tofauti wanaweza kumpa muda kocha kujenga timu kabla ya kumhukumu, lakini kwetu lolote linaweza kutokea muda wowote.”