Kampeni za Ubunge katika Jimbo la Mchinga, Kata ya Rutamba, zimezinduliwa rasmi leo kwa kushirikisha viongozi mbalimbali wa Kitaifa na Mkoa, kampeni hizo zimezinduliwa rasmi kupitia Mbunge wa Jimbo hilo, Mama Salma Kikwete, akiambatana na mumewe, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya nne Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na wabunge kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Lindi.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), ambaye alikabidhi Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Mbunge pamoja na madiwani wote wa Jimbo la Mchinga.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Majaliwa alisisitiza kuwa Ilani hiyo imeeleza kwa kina changamoto na fursa zilizopo katika kila kata ya Jimbo la Mchinga, na kuwataka viongozi waliopokea Ilani kuhakikisha wanazifanyia kazi kwa vitendo ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha, tukio hilo limehudhuriwa na wananchi kwa wingi, kutoka sehemu mbalimbali ndani ya Mkoa na nje ya Mkoa wa Lindi ambapo walionesha hamasa kubwa ya kuunga mkono juhudi za kuimarisha ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi kupitia utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala(CCM).