Kasi ya mikopo inapungua, sekta nyingine zinakua

Dar es Salaam. Wakati ukuaji wa mikopo kwa shughuli za kiuchumi ukiendelea kuwa chanya, takwimu mpya zinaonesha kasi yake inapungua, huku baadhi ya sekta zikionekana kupata mwendo wa kasi na nyingine zikibaki nyuma.

Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa katika mwaka ulioishia, mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 15.9, ikipungua kutoka asilimia 17.1 iliyorekodiwa Mei.

Sekta ya viwanda inaongoza katika kupungua kwa kasi hiyo, baada ya kushuhudia ongezeko kubwa la mikopo mwaka jana, lakini sasa hali ni tofauti. Kilimo, ambacho kwa muda mrefu kimekuwa kinara wa mikopo ya sekta binafsi, pia kinaonesha kupungua kwa kasi ingawa kinavutia mikopo kwa wingi.

Kwa upande mwingine, sekta ya madini, ujenzi na utalii vinaonesha matumaini mapya, huku benki zikielekeza fedha kwenye shughuli hizi kwa kasi inayoendelea kuongezeka.

Wachambuzi wanasema muundo huu usio sawa wa ukuaji wa mikopo unaonesha udhaifu wa kimuundo kwenye soko la mikopo, ambapo ukopaji wa Serikali unaziba nafasi ya sekta binafsi, na hatari za kimfumo kwenye kilimo zinapunguza hamasa za benki kukopesha.

Mei 2024, mikopo kwa wenye viwanda ilikuwa ikikua kwa karibu asilimia 30 kwa mwaka, na Juni 2024 ilikuwa asilimia 22.6. Mwaka mmoja baadaye, ukuaji uliporomoka hadi asilimia 7.3 Mei 2025 na asilimia 2.5 Juni.

Kilimo, ambacho kinajiriwa na Watanzania wengi, kiliendelea kuvutia mikopo mikubwa, lakini hata hapa kasi inapungua. Ukuaji wa mikopo ulipungua kutoka rekodi ya asilimia 53.1 Juni 2024 hadi asilimia 30.2 Juni 2025.

Ingawa bado kiko mbele ya sekta nyingi, kupungua huko kunaonesha hatari ambazo benki bado zinahisi zinapokopesha wakulima. Hali ya hewa isiyotabirika, mabadiliko ya bei za mazao, na wadudu wanafanya kilimo kiwe hatarishi bila msaada wa bima.

Mchumi wa Biashara ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano, anaamini ukosefu wa bima ya kilimo ya kuaminika ndiyo kikwazo kikubwa.

“Tukitaka kufungua mikopo kwa wakulima, bima haiwezi kuepukika. Bila bima, benki huona kilimo kama Kamari, lakini kikiwa na bima, wanakiona kama biashara inayostahili kufadhiliwa,” anasema.

Dk Mwinuka anasisitiza njia ya mbele ni kuboresha kilimo kwa kisasa. Kutumia mashine, umwagiliaji, mbegu bora na teknolojia za kidijitali vyote vinahitaji mtaji, lakini pia vinageuza kilimo kuwa biashara inayoweza kukopesheka.

Wakati sekta ya viwanda na kilimo zikionesha kupungua kwa kasi, sekta nyingine zinafurahia ongezeko. Madini na machimbo, yaliyopungua kwa asilimia 3.1 Juni 2024, yalipanda kwa asilimia 21.3 Juni 2025.

Mabadiliko hayo yanatokana na ongezeko la mahitaji ya dhahabu na madini mengine katika soko la dunia, sambamba na sera za Serikali zinazohamasisha uongezaji thamani.

Mtaalamu wa Ununuzi na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi, Humphrey Simba, aliambia gazeti dada la The Citizen kuwa maendeleo katika sekta ya madini yametokana na majadiliano yanayoongezeka kati ya sekta ya madini na benki yaliyosababisha kuelewana kwa pamoja.

Simba, ambaye pia ni mshauri mzoefu wa madini, anasema zamani uelewa kati ya pande hizo mbili ulikuwa mdogo mno.

“Hivi karibuni Serikali imekuwa ikihimiza sekta ya fedha kuona namna ya kukopesha sekta ndogo na ya kati ya madini inayokua,” anasema.

Anaongeza kuwa ushiriki wa serikali kupitia kanuni na ushawishi pia umesaidia, akitaja kamati iliyoundwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, kushughulikia changamoto za fedha kwa kampuni ndogo na za kati za madini.

Sekta ya ujenzi, ikisaidiwa na miradi mikubwa ya miundombinu na mahitaji ya makazi, pia imepiga hatua. Ukuaji wa mikopo uliruka kutoka asilimia 16.2 Juni 2024 hadi asilimia 25.7 Juni 2025, ukionesha hamasa ya sekta hiyo kubaki kubwa.

Hoteli na migahawa, ambavyo vilikumbwa na athari kubwa wakati wa janga la Uviko-19 na kupoteza mikopo kwa kiwango kikubwa, sasa vipo kwenye njia ya kupona. Mikopo kwa sekta hiyo ilikua kwa asilimia 20.8 Juni 2025, ikilinganishwa na upungufu mkubwa wa zaidi ya asilimia 30 mwaka uliopita. Kuimarika kwa idadi ya watalii kumeongeza imani na kuzifanya benki zikopeshe zaidi biashara za ukarimu.