Kigoma. Mzee Hassan Kilanoza mkazi wa kijiji cha Matiazo, Kata ya Simbo mkoani Kigoma, amekuja na ubunifu wa uzalishaji nishati safi kutokana na fursa aliyoiona.
Mzee huyu amebuni mashine maalumu inayozalisha mkaa banifu unaotokana na taka za mabaki ya mafuta ya mawese baada ya kukamuliwa mafuta.
Kwa zaidi ya miongo miwili, Mzee Kilanoza, ameutumia ubunifu wake kujenga maisha. Awali, alijihusisha na ufundi wa uchomeleaji wa vyuma pamoja na matengenezo ya injini za magari na mashine mbalimbali.
Lakini tangu mwanzoni mwa miaka ya 2010 amejikita katika uzalishaji wa mafuta ya mawese, akianzisha kampuni iliyosajiliwa ya Kilanoza Palm Oil Company Investment Limited ili kuvutia wawekezaji na wafadhili.
Umaarufu wake umeongezeka zaidi baada ya kuunda mashine za kipekee zinazotengeneza mkaa mbadala kutoka kwenye taka zinazotokana na mafuta ya mawese.
“Nimekuwa nikizalisha taka na mabaki mengi ya mawese kwenye kiwanda changu,” anasema.
Taka hizi awali alikuwa akizipeleka shambani kama mbolea, akitumia gharama kubwa bila faida. Uthubutu huu wa kuzibadili taka kuwa fursa umemuweka kwenye ramani ya ubunifu wa nishati safi mkoani Kigoma.
“Baadaye nilifikiria namna ya kugeuza taka hizi kuwa mkaa ndipo nilipobuni mashine maalumu ya kuzalisha,”anafafanu.
Safari ya nishati safi haikuanzia hapo
Kabla ya kuanza rasmi biashara ya mkaa mbadala, Kilanoza alianza na mradi wa biyogesi kwa ajili ya kupikia nyumbani.
Alichukua mafuta mabaki yanayojulikana kama mchachiko, ambayo kwa kawaida hutupwa na kuyatumia kuzalisha gesi.
“Baada ya kugundua kwamba mabaki haya ya mafuta yanavimba na kutoa gesi, nilitengeneza mitungi ya kuhifadhia bayogesi na ilifanya kazi kwa ufasaha,” anafafanua.
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, amekuwa akitumia nishati hiyo kwa matumizi ya nyumbani.
Hata hivyo, mradi wa biyogesi haujakuwa kibiashara kutokana na changamoto za kifedha.
Kila siku, anatengeneza gesi lita 40 pekee kutoka lita 15,000 za maji machafu yanayotokana na mawese, huku kiasi kikubwa kikimwagwa bila kutumika.
Anasema kama angepata mtaji, angeweza kuzalisha gesi ya kutosha kukidhi mahitaji ya kijiji kizima.

Kuzaliwa kwa mkaa mbadala
Fursa kubwa ilijitokeza baada ya Kilanoza kushiriki semina ya Shirika la Catholic Relief Services (CRS) kupitia mradi wao wa Voices, unaohamasisha jamii kubadili taka kuwa fursa za kiuchumi. Kupitia mafunzo hayo, alibuni mashine inayozalisha mkaa mbadala kutoka kwenye masalia ya mawese.
“Mkaa wangu unawaka kwa zaidi ya saa 12 bila kuzimika na hauna madhara kwa mazingira. Tofauti na mkaa wa miti, huu mkaa unadumu muda mrefu na hauhitaji kukata miti mingi,” anasema Kilanoza.
Pia, anasema mashine zake alizibuni kwa kutumia vyuma chakavu.
Anasema uchafu anaoutumia kutengeneza mkaa huonekana kama takataka, lakini kwake ni rasilimali yenye thamani.
Mkaa mbadala wa Kilanoza unatajwa kuwa mkombozi wa kiuchumi na mazingira.
Anasema kwa uchunguzi uliofanywa na wataalamu, “mkaa huu ninaotengeneza tani moja ina uwezo sawa na tani 12 za mkaa wa miti kwenye ufanisi na matumizi.”
Anasema hili linadhihisha ufanisi wa mkaa huu na ndio sababu bidhaa hiyo imeteka wateja wengi wakiwamo wachomaji wa mahindi na chipsi, migahawa, pamoja na wazalishaji wa mikate na mandazi.
“Mkaa wangu nauuza kwa bei nafuu ya Sh300 kwa kilo moja. Kilo moja ya mkaa huu inaweza kupika maharagwe mpaka kuiva,” anasema huku akiongeza kuwa mkaa wa miti hugharimu zaidi na huisha haraka.
Mashine alizounda zina uwezo wa kuzalisha hadi tani 30 kwa siku, ingawa kwa sasa huzalisha tani moja pekee kutokana na changamoto za kifedha na miundombinu.
Muuza mahindi Buruani Hilali anasema, “nimeongeza ufanisi kwa matumizi ya mkaa huu. Kwanza ni bei rahisi na unadumu muda mrefu. Mkaa kilo moja naweza kutumia kwa siku mbili.”
Pamoja na mafanikio yake, Kilanoza anakiri kukumbwa na changamoto nyingi ikiwamo ukosefu wa eneo la kutosha kwa kuanika na kutunza mkaa, hana maghala ya kuhifadhia na pia anakosa usafiri wa kusambaza bidhaa kwa wateja.
“Soko lipo kubwa, lakini sina usafiri wa kupeleka bidhaa. Pia, eneo langu ni dogo, wakati mkaa unahitaji siku tatu hadi nne kuanikwa na kukauka. Ningepata msaada wa kifedha ningehama kwenda sehemu kubwa na kuongeza uzalishaji ili nikidhi mahitaji ya Kigoma,” anasema.
Aidha, anashauri Serikali kuweka mkazo zaidi katika kuhakikisha taasisi kama shule, vyuo na jumuiya zenye watu wengi zinatumia nishati safi, badala ya kuendelea kutegemea mkaa wa miti.
Serikali mkoani Kigoma imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa lengo la kufikia asilimia 80 ya familia kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
Machi 2025, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma-Ujiji, chini ya Mkurugenzi Kisena Mabuba aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Kirumbe Ng’enda, iligawa zaidi ya majiko banifu 200 kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali na wanufaika wa mradi wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Hata hivyo, Kilanoza anasema bila msaada wa Serikali na wadau, ni vigumu wajasiriamali wadogo kufikia malengo makubwa.
Anakiri kwamba angeweza kuacha mradi huu kutokana na changamoto za kifedha, lakini msaada na hamasa kutoka CRS umemfanya aendelee.
Roberts Muganzi, msimamizi wa mradi wa Voices kutoka CRS, anasema Kilanoza hakuwa na uelewa kuhusu mkaa mbadala kabla ya kupewa elimu.
“Alikuwa akijihusisha zaidi na mawese pekee. Tulimfundisha namna taka za mawese zinavyoweza kuwa fursa kiuchumi, na leo ni mfano wa ubunifu wa nishati safi Kigoma,” anasema.
Mradi wa Voices una lengo la kuboresha ubora wa maji katika Ziwa Tanganyika kwa kupitia uchumi rejeshi. Taka zinazohatarisha mazingira hubadilishwa kuwa bidhaa zenye thamani.
Mpango huu unatekelezwa katika halmashauri za Kigoma-Ujiji, Uvinza na Kigoma Vijijini; unatarajiwa kuwafikia watu 119,160 kati ya mwaka 2024 na 2028. Tayari zaidi ya watu 30,000 wamenufaika.
Muganzi anaongeza kuwa, CRS inashirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia taasisi kama Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Watumishi kutoka halmashauri hizo walitumwa Moshi kwa mafunzo ili Kigoma ifikie kiwango cha ubora wa mazingira kinachofanana na mji huo.
Kupitia mfuko wa Circular Economy Challenge Fund, CRS inatoa ruzuku hadi Sh3 bilioni kwa wajasiriamali wanaotekeleza miradi ya uchumi rejeshi.
Kiasi kinachotolewa hutegemea tathmini ya uhitaji wa mradi, mfanyabiashara mdogo anaweza kupata kuanzia Sh10 milioni.
Kwa msaada huu, Kilanoza anaamini ataweza kupanua biashara yake na kukidhi mahitaji makubwa ya soko.
“Nikitengewa mtaji, nitaongeza uzalishaji wa mkaa na pia nitaboresha mradi wa biyogesi ili kusambaza gesi ya kupikia kwa kijiji kizima. Pia,nina mpango wa kutafuta mashine ya kusaga plastiki kwa ajili ya biashara,” anasema.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917