Nairobi. Wakulima wa mazao ya viungo Tanzania wamepata neema mpya kufuatia uamuzi wa kampuni ya Aavishkaar Capital kuwekeza Dola milioni 5 za Marekani (Sh12.5 bilioni) kwa ajili ya ukuzaji na uchakataji wa mazao hayo ili kukidhi mahitaji ya soko.
Katika hafla ya kuelezea mpango huo mwishoni mwa wiki hii, ilielezwa kuwa fedha hizo zitawasaidia wakulima zaidi ya 3,000 katika nchi za Tanzania, Nigeria na Madagascar kupitia kampuni ya Horizon Group inayofanya kazi na wakulima wa viungo.
Aavishkaar Capital, inayofanya kazi chini ya mwamvuli wa Aavishkaar Group, imetangaza uwekezaji huo barani Afrika kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji na Maendeleo inayomilikiwa na Serikali ya Ujerumani, KfW.
Uwekezaji huo umewezeshwa na Mfuko wa Dunia wa Kusaidia Mnyororo wa Ugavi (GSCSF), ambao ulitoa mkopo wa fedha hizo kwa Horizon Group Africa. Huu ni uwekezaji mkubwa wa nne kufanywa na GSCSF barani Afrika.
Kampuni ya Horizon Group hujihusisha na utafutaji na uchakataji wa viungo na kuviuza katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU), Asia na Marekani. Kampuni hiyo inafanya kazi kupitia vituo vyake nchini Tanzania, Nigeria na Madagascar, ikinunua na kusaidia katika uzalishaji na uchakataji wa tangawizi, bizari (manjano), iliki, mdalasini, karafuu na pilipili manga.
Mkopo huo utaelekezwa zaidi katika kukuza mtaji wa Horizon Group, hususan katika ununuzi wa malighafi ili kukidhi viwango na mahitaji ya soko la kimataifa.
“Tunafurahi kufanya kazi na Aavishkaar Capital tunapoanza awamu nyingine ya safari yetu ya kukua. Uzoefu wao katika kukuza biashara, kuimarisha mifumo ya uongozi, kuwezesha upatikanaji wa soko na kufungua mitaji utakuwa wa manufaa tunapoijenga Horizon kuwa kampuni inayoongoza katika uchakataji wa viungo,” amesema Jomy Antony, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Horizon Group.
Akitoa maoni yake kuhusu uwekezaji huo, Darren Lobo, Mkurugenzi katika kampuni ya Aavishkaar Capital, amesema: “Tumefurahi kufanya kazi na Horizon Group, ambayo inaleta uzoefu wa zaidi ya miaka 80 ya utaalamu katika uzalishaji na uuzaji wa viungo, ili kujenga moja ya kampuni kubwa ya kuchakata viungo Afrika.”
Naye kiongozi wa Divisheni katika benki ya KfW, Dk Markus Aschendorf, amesema uwekezaji wao katika Horizon Group kupitia Mfuko wa Dunia wa Kusaidia Mnyororo wa Ugavi (GSCSF) unaakisi dhamira yao ya kuimarisha mnyororo endelevu wa ugavi Afrika na Asia.
“Tunaamini kwamba mtaji ukitumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa, utachochea uwekezaji unaozingatia masuala ya mazingira, jamii na uongozi, huku ukifungua ukuaji shirikishi,” amesema.