MABINGWA watetezi wa michuano ya CECAFA kwa wanawake, CBE FC ilianza kwa kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda huku kocha wa timu hiyo, Heye Gizaw akileta visingizio.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Ethiopia imepangwa kundi B na Rayon Sports ambayo iko kileleni kwa kundi hilo na Top Girls ambayo hadi sasa haijacheza mechi yoyote.
Gizaw alisema timu hiyo haikufanya maandalizi vizuri kwani waliwasili Kenya siku mbili kabla ya mechi, hivyo baadhi ya wachezaji miili yao haikuendana na hali ya hewa.
Aliongeza kichapo walichopokea wameona eneo lipi lina mapungufu na wanaenda kuweka mpango mkakati ili kuhakikisha mechi moja iliyosalia wanapata matokeo.
Alisisitiza mechi ijayo dhidi ya Top Girls Academy ya Burundi wana kila sababu ya kushinda ili kusogea hatua inayofuata na hawatamani kuishia makundi.
“Msimu huu kila timu imejipanga hakuna timu nyepesi, kama mabingwa watetezi hatutamani kuishia hapa, lengo letu ni kwenda nusu fainali na fainali licha ya ugumu wa mechi hizo tunaamini tutashinda,” alisema na Gizaw kuongeza;
“Ni timu moja itakayokuwa bingwa, ndiyo itawakilisha Ligi ya Mabingwa Afrika na tunatamani kupata nafasi hiyo na tunaamini tuna huo ubora wa kuchukua taji.”