KOCHA wa Yanga, Romain Folz ni kama kashindikana katika ishu ya kucheka, kwani mapema leo asubuhi amekuwa gumzo katika mkutano mkuu wa klabu hiyo, baada ya kugoma kabisa kutabasamu kwenye majaribio mawili tofauti aliyofanyiwa na wanajangwani.
Iko hivi. Folz ametua na benchi la ufundi katika mkutano mkuu huo unaofanyika kwenye Ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam ambapo wakati wa utambulisho unaendelea ikafika hatua ya kutambulishwa kwa Mfaransa huyo.
Utambulisho huo ukafanywa na Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe ambapo akawaomba wajumbe wa mkutano mkuu kuhakikisha wanashangilia mpaka kocha huyo atabasamu kwa mara ya kwanza.
Kocha huyo hajawahi kuonekana akicheka wala kutabasamu katika pixcha zake tangu akiwa anafanya kazi Afrika Kusini na Kamwe alitaka kumlazimisha kiaina atabasamu, lakini alichomoa.
“Ndugu zangu wanachama, nawaletea jukumu hili nyie sisi tumeshindwa hebu Leo nataka mpige makofi na kumshangilia mpaka atabasamu,” amesema Kamwe.
Hata hivyo, licha ya shangwe kubwa la wanachama lakini Folz aliishia kupiga makofi pekee akiwageukia wanachama hao.
Kamwe hakuishia hapo akawapa nafasi ya pili wanachama hao kujaribu tena kumshangilia kocha huyo akisimamisha, lakini bado Folz alishindwa kutabasamu.
Baada ya tukio hilo Kamwe akasema: “Wanachama na nyie pia mmeshindwa? Basi hiki chuma kitatabasamu Septemba 16, tutakaposhinda mchezo wetu.”
Yanga itacheza na Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni wa kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2025-26, huku wababe hao wakiwa watetezi wa taji hilo walilolitwaa msimu uliopita kwa kuifunga Azam FC kwa mabao 4-1 baada ya awali kushinda 1-0 katika nusu fainali ilikutana na Wekundu wa Msimbazi. Bao lililofungwa na Maxi Nzengeli.