Kuelekeza kupita kiasi kikwazo kwa mtoto kujifunza

Jumamosi asubuhi, Mariam hupewa jukumu la kufagia sebuleni na mama yake. Kila anaposhika ufagio, mama haishi maagizo.

“Anzia pale kona, shika ufagio vizuri, pitisha ufagio kama hivi, usisahau chini ya meza, sasa pindua kiti, hapana, usifagie kwa haraka hivyo. Mtoto wa kike usiwe na haraka unaposafisha nyumba.”

Mara nyingine, anapokuwa anaosha vyombo, mama haishiwi maagizo: “Shika kikombe kwa namna hii, hakikisha sahani inang’aa, osha sufuria kwanza, sasa sugua vizuri.”

Ungekuwa Mariam ungejisikiaje? Kwa nini mama anaona ni sawa kutoa maagizo mengi kiasi hiki? Je, maelekezo mengi kama haya yanamsaidia mwanawe au ni namna tu ya kujiridhisha mwenyewe?

Mariam alianza kuchukia kazi za mikono. Ilifika wakati akawa hafanyi kitu mpaka apate maelekezo mengine. Mariam akaanza kuamini chochote anachofanya lazima kitarekebishwa.

Hali kama hii ni ya kawaida sana katika familia zetu. Wazazi wengi huamini kwamba kutoa maagizo ya kila kinachopaswa kufanya ni sehemu ya kuhakikisha mtoto anajifunza “njia sahihi” ya kufanya kazi. Wengine huchochewa na hofu ya aibu mbele ya jamii.

Mzazi anapomwona mtoto hakufanya kinachotarajiwa hujihisi kashindwa malezi. Pia, baadhi ya wazazi hufikiri malezi ni ukamilifu—mzazi anataka mtoto afanye kazi kwa kiwango kile kile anachokiona kuwa ndio usahihi. Maagizo mengi, kwa maana hiyo, ni kumjenga mtoto kuwa mwadilifu na mwenye nidhamu.

Matokeo ya hali hii ni mtoto kukosa kujiamini na kutofanya uamuzi. Mtoto anapojua kila hatua itakosolewa au kurekebishwa, kama ilivyo kwa Mariam, huanza kuogopa kufanya makosa. Hofu ya makosa inamnyima ubunifu na kuondoa ari ya kujifunza.

Kwa upande mwingine mawasiliano ya kihisia kati ya mzazi na mtoto hupungua. Mtoto anapojua kila anachosema au kufanya kitakatishwa na kurekebishwa, hujifunza kunyamaza au kujiweka mbali.

Wapo watoto wanaokosa kuongea na wazazi wao kwa sababu wanahisi kila wanachosema kitageuzwa kuwa maelekezo. Badala ya mawasiliano, panabaki sauti ya mamlaka ya mzazi.

Ushauri kupita kiasi, aghalabu, huzalisha tabia ya uasi. Mawazo ya “sifanyi tena,” huanza kuchanua na hatimaye mabishano yataanza. Kwa nini? Kila binadamu ana hitaji la kusikika.

 Unapoanza kuhisi husikiki, utatafuta namna ya kusikika hata ikibidi kwa kupishana na mzazi. Kwa lugha rahisi, maagizo mengi kwa mtoto humgeuza mtoto kuwa mpinzani anayepigania uhuru wake.

Aidha, mtoto anayekuzwa katika mazingira ya amri zisizoisha, hujenga mtazamo kwamba thamani yake inategemea uwezo wake wa kufuata maagizo kama yalivyo.

Hii inaweza kuchukuliwa kama nidhamu lakini kimsingi ni maigizo yanayotokana na kunyimwa kujiamini. Hali kama hii humfanya mtoto akaingia utu uzima akishindwa kufanya uamuzi unaojitegemea.

Hata hivyo, kusema hivi hatumaainishi ushauri na mwongozo wa mzazi hauhitajiki. Changamoto inakuja pale mzazi unapoanza kuonekana huna imani na uwezo wa mtoto kujifunza na huvumilii makosa.

Je, kila kosa lina madhara? Kukosea kufagia kuna hatari gani inayoleta udharura wa kuingilia anachofanya mtoto? Kwa nini, kwa mfano, badala ya maelekezo mengi, mzazi asiulize swali linalochochea uamuzi?

Badala ya kukosoa wakati shughuli ikiendelea, kwa nini mzazi asimwache mtoto amalizie kazi na kisha kuzungumza naye kwa upole namna ya kuboresha?

Malezi, kimsingi, ni mchanganyiko wa mwongozo unaoenda sambamba na kukuza uhuru—kumsaidia mtoto bila kuminyia nafasi ya kukua na kujifunza kufanya uamuzi wake mwenyewe.

Jean Piaget, mshunuzi nguli wa kale, anayachukulia malezi kama uwezo wa kumwamini mtoto, kwa kumpa fursa ya kuchunguza, kujaribu, kukosea, kudadisi, kujirekebisha na hatimaye yeye mwenyewe agundue namna ya kutendaa bila kuingiliwa sana na mzazi. Piaget anaamini kosa hufundisha vizuri zaidi kuliko maelekezo.

Kinyume na tunavyoamini wengi, watoto huzaliwa na uwezo wa kujifunza wenyewe. Watoto wanaweza kujifunza vizuri zaidi kwa makosa wanayofanya wenyewe.

Hata uelewa wa mtoto haujengwi kwa maelekezo ya kiutu uzima bali kwa kuaminiwa na kupewa nafasi ya kujaribu.

Kwa maana hiyo mzazi anapompa nafasi mtoto kushughulika na kazi kwa uhuru—kama vile kufagia, kupika au kuosha vyombo—anachangia si tu katika kujifunza stadi za maisha, bali pia katika kukuza uwezo wa kufikiri kwa kina na kujiamini.

Kwa maneno mengine, ushauri bora ni ule unaoweka msingi wa kujitegemea, na si ule unaofunika kila hatua ya safari ya mtoto kujifunza.

Ujumbe kwako mzazi ni kumwacha mtoto ajaribu. Acha afagie hata kama hajaanza vizuri, acha apike hata kama ugali unakuwa mgumu, acha aoshe vyombo hata kama baadhi havijang’aa. Baada ya hapo, unaweza kumpa mwongozo wa kuboresha bila kumvunja moyo.

Kwa njia hiyo, mtoto anajenga ujasiri, anajifunza kuchukua hatua na hatimaye anakuwa mtu mzima anayejiamini na kujitegemea.