Majaliwa aitaja miradi mitano mikubwa akizindua kampeni Mchinga

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewahakikishia wananchi wa Lindi kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo itaendelea kutekelezwa endapo watamchagua mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.

Amesema miradi hiyo ni pamoja na gesi, bandari ya uvuvi Kilwa, ujenzi upya wa barabara ya Dar es Salaam–Lindi, maboresho ya uwanja wa ndege wa Lindi, ujenzi wa reli ya Kanda ya Kusini na kuunganisha mkoa wa Lindi kwenye Gridi ya Taifa ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.


Majaliwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema hayo leo Jumapili, Septemba 7, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM za ubunge Jimbo la Mchinga uliofanyika katika kijiji cha Rutamba, mkoani Lindi.

Ameeleza kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM 2025/2030 imejielekeza katika kuendeleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo kote nchini, ikiwemo katika Jimbo la Mchinga.

Aidha, amesema mgombea urais wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Samia tayari amepeleka mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika mkoa wa Lindi.

“Katika kipindi kilichopita, Rais Samia ameleta hapa miradi mikubwa na ya kati pamoja na midogo, akitambua kuwa wananchi wanapaswa kuhudumiwa. Hata ilani hii imeonesha maeneo mapya yatakayotekelezwa katika mkoa huu wa Lindi,” amesema Majaliwa.


Ameongeza kuwa ilani ya uchaguzi imetamka bayana kuwa barabara za Ngongo–Ng’apa na Mandawa–Chikundi zitajengwa kwa kiwango cha lami, jambo litakalofungua uchumi wa wananchi wa Lindi.

Katika mkutano huo, Majaliwa pia alimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Mchinga, Salma Kikwete, kwa kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, ikiwemo upatikanaji wa magari manne ya wagonjwa na ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, hatua zilizosaidia kuboresha huduma za afya.


“Mheshimiwa Salma Kikwete amejikita katika kuwahudumia wananchi. Kwa namna jimbo hili lilivyo, linahitaji mtu mahiri na mwenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wake. Ameonesha anaweza, mchagueni tena,” amesema Majaliwa.

Kwa upande wake, Salma Kikwete amesema amefanikisha miradi kadhaa kwa kushirikiana na wananchi wa Mchinga, ikiwemo sekta za afya, elimu, nishati, maji, miundombinu na uwezeshaji wananchi kiuchumi. Amebainisha pia kuwa ametekeleza mradi wa maji kutoka Ng’apa, utakaowafikia vijiji vingi katika jimbo hilo.

“Tumeweza kupiga hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto zilizokuwepo. Hali ya sasa siyo ile tuliyokuwa nayo awali. Nikipata ridhaa tena, tutafanya makubwa zaidi,” amesema Salma.


Naye Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amesema mgombea urais wa CCM, Samia, ameonesha uwezo wa kuongoza kwa mafanikio, hivyo anapaswa kupewa nafasi ya kuendelea.

“Alipata urais katika mazingira ambayo hakuyatarajia, lakini amefanya kazi nzuri. Tukimpa nafasi tena, tutanufaika mara dufu. Nimeangalia orodha ya ilani na kwa hakika amejiandaa,” amesema Kikwete.

Akizungumza kwa niaba ya wagombea ubunge wa CCM Mkoa wa Lindi, mgombea ubunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, amesema wananchi wa kusini watamchagua Samia kutokana na kazi kubwa aliyoifanya, ikiwemo utoaji wa ruzuku za pembejeo kwa mazao ya kilimo.