KIUNGO mkabaji wa zamani wa Yanga, Said Juma ‘Makapu’ ametua Mbuni FC kwa mkataba wa miezi sita, huku akisema anatarajio ya kufanya makubwa akiwa na timu hiyo kwa vile ameshaizoea Ligi ya Championship inayoshiriki timu hiyo.
Kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars msimu uliopita aliichezea Geita Gold katika Ligi ya Championship kitu alichosema ligi hiyo kwa sasa imebadilika na imekuwa na ushindani mkali unaohitaji mchezaji awe ufiti zaidi.
“Utofauti wa Ligi Kuu inatumia mbinu za makocha, nguvu na akili kubwa, ila Championship inahitaji utimamu wa mwili zaidi maana inachezwa kwa nguvu, awali ilikuwa ngumu kwangu ila kwa sasa nimezoea,” alisema Makapu na kuongeza;
“Japo wachezaji ambao tumecheza Ligi Kuu tupo wengi katika Ligi ya Championship, lakini kuna vipaji vikubwa ambavyo vikipata nafasi ya kuonekana vitafanya vizuri zaidi.”
Kuhusu kucheza Ligi Kuu alisema anaweza akarejea muda wowote endapo akipata timu itakayokuwa na maslahi kwake:
“Kikubwa kwa mchezaji ni maslahi yake, kabla sijasaini Mbuni, zilikuwapo timu nyingi zilizokuwa zinahitaji huduma yangu, ila kila kitu kina muda wake.”