ALIYEKUWA mfanyabiashara na mdhamini wa Yanga, Yusuf Manji amepewa heshima katika mkutano mkuu wa klabu hiyo unaoendelea kwenye Ukumbi wa Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa kawaida wa mwaka unafanyika leo ukiwa na ajenda 10, lakini kubwa ni mipango mkakati kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano kwa mwaka 2025-26.
Manji aliyejizoelea umaarufu mkubwa akiwa kiongozi wa Yanga, alifariki dunia Jumamosi ya Juni 29, 2024 saa 6 usiku akiwa Florida jijini Marekani.
Akizungumza katika mkutano huo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliwataka wanachama wa kikosi hicho kusimama kidogo ili kuwakumbuka baadhi ya watu mbalimbali waliofariki kwa msimu wa 2024-25.
Miongoni mwa baadhi yao ni Manji aliyejizoelea umaarufu mkubwa katika uongozi wake na aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Iman Omary Madega aliyefariki dunia Februari 10, 2024.
Kiongozi mwingine aliyekumbukwa ni aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Nyasebwa Mafuru aliyefariki dunia Novemba 9, 2024 akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Apollo, India pamoja na wengine waliowahi kuiongoza klabu hiyo kama Rashid Ngozoma Matunda, Lawrance Mwalusako na wanachama maarufu wa Yanga waliotangulia mbele ya haki.