Mtanzania asalia Misri mwaka mmoja

MSHAMBULIAJI wa Makadi FC, Oscar Evalisto, amesema ameamua kusalia klabuni hapo kwa msimu mmoja ili kusikilizia ofa za Ligi Kuu nchini humo ambazo hazikufikiwa awali.

Huu ni msimu wa pili kwa mshambuliaji huyo kuitumikia Makadi. Msimu uliopita alicheza miezi sita akitokea Mlandege na aliwahi kupita Paje Star ya Zanzibar na Lipuli U-20.

Akizungumza na Mwanaspoti, Evalisto alisema kulikuwa na ofa za Ligi Kuu Bara na mbili kutoka Misri, lakini aliamua kusalia kwenye timu hiyo ili kuangalia uwezekano wa kukamilisha zile za awali ambazo hawakufikia makubaliano kutokana na ofa ndogo waliyoweka.

“Hatuwezi kujifungia, kwa maana kuna ofa pia katika timu nyingine za madaraja ya juu, kwa hiyo tunasikilizia kwanza. Japo walitaka tusaini miwili, lakini wakala wangu ameamua tusaini mmoja,” alisema Evalisto na kuongeza:

“Naamini kama nitaendelea kupata nafasi kama ya msimu uliopita, inawezekana wakaongeza ofa kwenye hiyo timu kwa sababu walinihitaji sana, lakini ofa ilikuwa ndogo tukaachana nao.”

Mshambuliaji huyo, aliyeondoka Tanzania wiki iliyopita kujiunga na kambi ya timu hiyo, aliingia dirisha dogo akicheza mechi tatu na kufunga mabao mawili.

Kiujumla, Ligi ya Misri hadi sasa ina wachezaji watatu wa Kitanzania wanaocheza Ligi Kuu: Evalisto, beki wa kushoto Raheem Shomari (Ghazl El Mahalla) na Arafat Masoud ‘Konde Boy’ aliyetambulishwa hivi karibuni na ENNPI.