Mulumbe wa ADC azindua kampeni akiahidi kuanza na nyumba za polisi

Mwanza. Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Elias Mulumbe, ameahidi kuvunja nyumba zote za askari wa Jeshi la Polisi nchini na kujenga makazi ya kisasa atakapochaguliwa, ili kuhakikisha watumishi hao wa umma wanaishi katika mazingira bora.

Mulumbe ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Septemba 7, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika katika viwanja vya stendi ya magari Pasiansi, wilayani Ilemela, Mkoa wa Mwanza.

“Nimefanya utafiti nchi nzima na kugundua askari wetu hawana makazi mazuri. Punde tu nitakapochaguliwa, nitahakikisha navunja nyumba zote na kujenga nyumba mpya za kisasa.

Baadhi ya wananchi wakifuatilia uzinduzi wa kampeni ya chama cha ADC Pasiansi jijini Mwanza. Picha na Saada Amir



“Naomba mnichague mimi kwa kuwa ni kijana mwenye nguvu na nitabadilisha mambo mengi katika nyanja zote,” amesema Mulumbe.

Hata hivyo, amesema kipaumbele cha kwanza cha ADC ni sekta ya elimu, akisema chama hicho kinalenga kuhakikisha walimu wa shule za umma ni wenye shahada za kwanza na shahada za uzamili, ili kuboresha viwango vya elimu nchini.

“Sisi ADC tuna jawabu la kurudisha elimu katika hadhi yake. Njia bora ni kuajiri walimu wenye shahada kutoka vyuo vikuu na kuwaboreshea maslahi yao. Tunataka watoto wetu wafundishwe na walimu wenye kiwango cha juu cha elimu, ili tuweze kushindana na wenzetu wa Kenya,” ameongeza.

Mbali na elimu, Mulumbe ameahidi huduma bora za afya, umeme, na maji kwa wananchi. Amesema huduma za afya zitakuwa bure, dawa zitapatikana hospitalini bila malipo, na biashara ya dawa hospitalini itakomeshwa.

“Huduma za uunganishaji wa umeme zitakuwa bure, hata vijijini. Ile ada ya Sh27,000 mnayoambiwa italipwa, mkitupatia ridhaa ya kuongoza nchi, haitakuwepo. Lengo letu ni kuhakikisha asilimia 100 ya Watanzania wanapata huduma bora,” amesema mgombea urais huyo.

Akizungumzia maji, Mulumbe amesema wananchi wataunganishiwa bure, ila watalipa gharama ndogo za matumizi ili kusaidia uendeshaji wa huduma hiyo.

Aidha, ameahidi kufufua viwanda vya umma vilivyoshindwa kuzalisha, pamoja na kushusha bei ya samaki wa Ziwa Victoria ili kuwawezesha wananchi kupata chakula hicho kwa urahisi.

Baadhi ya wananchi wakifuatilia uzinduzi wa kampeni ya chama cha ADC Pasiansi jijini Mwanza. Picha na Saada Amir



“Tutafufua viwanda vyote vilivyokufa na kuvirejesha serikalini, lakini pia tutawachukulia hatua kali za kisheria wawekezaji waliopewa viwanda hivyo na kuviua, ikiwemo kuwaondoa nchini mara moja,” amesema Mulumbe.

Mwanza kuwa kitovu cha uchumi

Akizungumzia Jiji la Mwanza, Mulumbe amesema watalifanya si tu paradiso ya maisha bora, bali kitovu cha uchumi na maendeleo nchini.

“Tutakapopewa ridhaa ya kuongoza nchi hii, Jiji la Mwanza litakuwa paradiso. Tutabadilisha hali ya maisha ya wananchi na Mwanza itakuwa kitovu cha maendeleo ya kiuchumi Tanzania. Ninaomba mnichague mimi Oktoba 29, lakini pia mumchague mgombea wetu wa ubunge wa Ilemela,” amesema Mulumbe.

Mgombea huyo pia amemuombea kura mgombea ubunge wa Ilemela kupitia ADC, Shaabani Itutu, akisema atashughulikia changamoto za wananchi, zikiwemo upatikanaji wa mikopo kwa wanawake.

“Kama tukiingia madarakani, tutawapatia mikopo yenye masharti nafuu kabisa. Pia tutaboresha elimu katika shule za Serikali, ili hata wahitimu wa vyuo vikuu waweze kufundisha katika shule zetu za msingi,” ameongeza.

Kwa upande wake, Itutu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa ADC, amesema chama hicho kikishinda kitatumia rasilimali nyingi za nchi kuboresha huduma za jamii, ikiwemo afya na maji.

“Haiwezekani kuishi Mwanza wiki nzima bila maji wakati ziwa lipo umbali wa kilomita mbili. Haiwezekani pia kinamama wajasiriamali kutozwa ushuru wakati wanafanya biashara ndogo ndogo ili kusaidia familia zao.

“ADC ikishinda tunaondoa ushuru wa aina yoyote. Tunataka mtu atakayelipa kodi aanze na mtaji wa Sh5 milioni. Tofauti na sasa, hata ukiwa na duka la Sh5 milioni, unatozwa leseni na ushuru,” amesema na kuongeza:

“Tutakuwekea utaratibu mzuri ili kukupandisha kiuchumi. Haiwezekani mkawa maskini kila siku, kila siku mnanyanyaswa na mnanyang’anywa fedha zenu.”

Itutu ameongeza kuwa ADC ikichukua madaraka, huduma za afya zitakuwa bure kwa wote kama ilivyo Zanzibar.

“Zanzibar uchumi wake unategemea zaidi bahari, lakini wananchi wake wanapata huduma ya afya bure. Bara tuna madini, ziwa, ardhi yenye rutuba, na rasilimali nyingi zaidi, kwa nini tushindwe?” amehoji.

Naye mgombea mwenza wa urais kupitia ADC, Shoka Khamis Juma, amewataka wananchi wa Ilemela kufanya mabadiliko kwa kuchagua chama hicho.

“Msifanye makosa ndugu zangu. Miaka yote mnawachagua watu hawa hawa wanaowasumbua? Mtu anakwenda kule anakaa wee kwenye kiti chake, anasubiri posho zake, hana habari ya kuangaika na watu wa jimbo lake,” amesema.