Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Jimbo la Mbagala kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hadija Mwago, ameahidi kubadilisha sura ya elimu kwa kujenga shule moja katika kila mtaa wa jimbo hilo, ili kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuhakikisha watoto wanapata elimu bora karibu na makazi yao.
Ametoa kauli hiyo leo, Septemba 7, 2025 katika mkutano wa uzindizi wa kampeni za jimbo hilo katika kiwanja cha Kwaserenge, Mbagala.
“Wazazi hawatateseka tena kusafirisha watoto umbali mrefu kutafuta shule. Tukiweka shule kila mtaa, tutakuwa tumepunguza changamoto kubwa ya elimu na kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi,” amesema.
Pia, mgombea huyo ameahidi kuwekeza kwenye huduma za afya kwa kuongeza miundombinu ya zahanati na vituo vya afya, sambamba na kusimamia mifuko ya mikopo ya vijana na kinamama ili kukuza ajira na kujikwamua kiuchumi.

Mwago amewataka wakazi wa Mbagala kuhakikisha wanachagua madiwani na Rais wa Chaumma, akisisitiza kuwa chama hicho ndicho mbadala wa kweli wa CCM, ambacho kimedumu madarakani kwa muda mrefu bila kuleta suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wananchi hao.
“Wana-Mbagala, kura zenu safari hii zinapaswa kuwa za ukombozi. Tukipewa nafasi ya kuunda serikali, tutaleta maendeleo yanayomgusa kila mmoja wenu moja kwa moja,” amesisitiza Mwago.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kampeni na Uratibu wa Kitaifa wa Chaumma, Kangeta Ismail, ametumia jukwaa hilo kuwaombea kura wagombea wote wa chama hicho kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani.
Kangeta amesema sera kuu ya Chaumma ni kujenga uchumi wa mlengo wa kulia, ambapo uchumi wa nchi unamilikiwa na wananchi badala ya Serikali.
Amedai mfumo huo utapunguza umaskini na kuwajengea wananchi mazingira ya kufaidi rasilimali za taifa lao.
“Hatutaki Serikali inayowaacha wananchi wake nyuma. Tunataka Serikali ya wananchi, inayomilikiwa na wananchi, na itakayopigania masilahi ya wananchi,” amesema Kangeta.