Mwenza wako ana haki kukuchunguza

Canada. Tufuatane katika kisa cha kufikirisha na kusisimua hata kuogopesha japo kinafundisha kitokanacho na upendo wa kweli.

Kawaida, wanandoa, hulala pamoja. Hili haliepukiki wala kujadilika katika maisha ya ndoa.

Siku moja, baba alikosa usingizi lakini akakaa kimya kuchelea kumuamsha mwenzie. Alistuka. Akiwa hana hili wala hili, mkewe aligutuka usingizini. Alianza kumnusa vidole.

Baba aliamua kukaa kimya akajifanya yuko fofofo ili kuona nini kitafanyika. Kwa vile hakujua lengo la mwenziwe, alitaka kujua mwisho na sababu zake. Mwanzoni, alidhani mkewe alikuwa mwanga au alikuwa akiota akiwa macho. Mama alimnusa vidole hata masikio akatabasamu na kulala.

Jambo hili, licha ya kumstua mume, lilimchanganya na kumwachia fikra nyingi asijue cha kufanya. Je, tukio hili au kitendo hiki, kama ungekuwa wewe, ungechukuliaje? Ungechukia? Ungefurahia? Ungechanganyikiwa au? Je, linakufundisha nini?

Kimsingi, binadamu anapolala, licha ya kuota, anaweza kuwa macho kwa kiwango fulani kwa vile ubongo wake huwa haulali.

Hivyo, kuna mambo mhusika anaweza kuwa akifikiria yakamrejea na akayafanya ama akiwa nusu usingizini au akiwa macho kama  alivyofanya mwanandoa huyu.

 Japo, hatuwezi kujua sababu za mama kumnusa vidole na masikio mumewe, tunajifunza mambo yafuatayo:

 Mosi, mwenza wako anafuatilia karibu kila jambo unalofanya, liwe kubwa au dogo, la maana, hata lisilo la maana. Licha ya kuwa haki yake, ni ishara kuwa anakujali na kukupenda vilivyo.

Pia, inaonyesha kuwa yuko tayari kukukosoa, kukurekebisha, hata kukuboresha inapobidi. Hivyo, usimuelewe vibaya wala kuhamanika, kwani, hakuna aliye mkamilifu hasa katika masuala yahusuyo miili yetu.

Pili, anaweza kuwa kanusa kitu, hivyo, anatafuta kukielewa na kukirekebisha. Muhimu, anafanya hivyo si kwa nia mbaya bali kukujua vizuri hata wakati mwingine kutokujua vizuri, kukushuku, kuhisi, au kujifurahisha.

 Tatu, hata kama hakwambii, kuna uwezekano mkubwa kuwa si kila anachokufanyia anakijua sawa nawe unavyomfanyia. Hivyo, baadhi ya vitendo, ama ni mrejesho au mwitikio wa matukio na matendo yako au hata yake.

Nne, anakufuatilia wakati mwingine kuliko unavyomfuatilia. Katika hili, kina mama wako mbali kuliko kina baba. Kimsingi, mkeo anakutunza kama vile ajitunzavyo au atunzavyo watoto wenu.

Wakati mwingine, anafanya mambo kama haya bila kuhiari au kupanga. Hivyo, ujue mkeo si mnoko wala mwanga.

Ni wanandoa wangapi limewahi kuwatokea hili au jingine lifananalo na hili? Mbali na hili, je, ni wangapi wanaangalia simu za wenzao kujua namna wenzao wanavyozitumia?

Uzoefu unaonyesha kuwa kina mama ndiyo mabingwa wa kufuatilia matumizi ya simu za wenza wao japo, pia, wapo kina baba wanaofanya hivyo.Tuliwahi kujadili namna simu zinavyoharibu ndoa na namna ya kuzuia balaa hili. Hivyo, wahusika wajue wajibu huu na kuukubali hata kama unaweza kuwa na ukakasi fulani hasa kwa wale wenye “mambo yao.”

Wangapi wanawaruhusu au kutowaruhusu wenzao wasiguse, achia mbali kuziangalia hata kuzipekua simu za wenzao? Wangapi wanawaficha wenzao simu zao? Japo unaweza kuona kama uchimvi, mwenzio angependa kujua wote unaowasiliana nao na anaweza kutaka hata nywila za baruapepe na simu zako. Je, ni busara, salama, au hatari kumpa mwenzio nywila za baruapepe na simu yako?

Japo unaweza kuona kama uchimvi, mwenzio ana lengo zuri la kukulinda wewe na ndoa yenu. Hivyo, usijisikie vibaya akitaka kukujua kama ilivyo kwenye kisa tulichoanza nacho.

Anakuwa na nia nzuri ya kutaka kuhakikisha usalama wenu wote. Kama tulivyobainisha pale juu, anakulinda kama kichanga japo wewe si kichanga.

Kama hujui, japo si wote, mwenzio anakuchunguza kila sekunde, saa, na siku. Yote ni kwa nia nzuri. Kwa wanandoa wanaopendana na kuaminiana vilivyo, wewe ni mali yake naye ni mali yako.

Tusisitize. Hafanyi hivyo kwa nia mbaya au kutokuamini ingawa wengine ni tofauti. Wakati mwingine, hata hajui kama anafanya haya.

Tusikutishe. Tumalizie kwa kusema kuwa unachopaswa kujua  na kuzingatia ni ukweli mchungu kuwa saa zote uko kwenye mawazo yake na uko chini ya uangalizi na uchunguzi muda wote katika maisha yako.

Kama huna “mambo yako” usiogope mwenzio kupitia mitandao au simu yako. Kuepuka au kuogopa, hata kama huna, kunajenga shaka kuwa una “mambo yako”