Namungo, City FC Abuja kufunga Tanzanite Pre-Season International leo

MCHEZO wa fainali ya mashindano ya Tanzanite Pre-Season International, unatarajiwa kuchezwa leo Septemba 7, 2025 kati ya Namungo kutoka Ruangwa nchini Tanzania dhidi ya City FC Abuja ya Nigeria.

Fainali hiyo itakayofanyika kuanzia saa 9:00 alasiri, itachezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara.

Namungo ilikuwa ya kwanza kufuzu fainali ya michuano hiyo baada ya kuiangushia Tabora United kichapo cha mabao 2-1, kisha City FC Abuja ikaichapa Dodoma Jiji kwa penalti 5-4 kufuatia dakika tisini matokeo kuwa 0-0. Mechi hizo za nusu fainali zilizochezwa jana Jumamosi uwanjani hapo.

Fainali hii inatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kwani inazikutanisha timu zilizokuwa Kundi C na zilipokutana matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.

Safari ya Namungo hadi kufika fainali, ilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya City FC Abuja, ikaichapa TDS mabao 3-1, ikamalizia makundi kwa kuifunga JKU 3-2 na kuwa kinara Kundi C. Ikatinga nusu fainali na kuiondosha Tabora United kwa mabao 2-1.

City FC Abuja nayo ilianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Namungo, ikaifunga JKU bao 1-0, kabla ya kufungwa 1-0 na TDS mchezo wa mwisho hatua ya makundi. Ikamaliza nafasi ya pili Kundi C na kufuzu nusu fainali ilipokwenda kuifunga Dodoma Jiji kwa penalti 5-4.

Akizungumzia mashindano hayo, Rais wa Fountain Gate FC ambaye ni mmiliki na mwanzilishi wa Fountain Gate School na Fountain Gate Sports Academy, Japhet Makau amesema msimu ujao wanatarajia kuwa na mashindano bora zaidi.

“Wazo la kuanzisha mashindano haya inatokana na changamoto ilizonazo timu za madaraja ya kati katika kupata mechi za kimashindano na kirafiki kabla ya ligi haijaanza.

“Tukaona kuna haja ya kuanzisha mashindano ambayo yatasaidia hizi timu za madaraja ya kati kupata mashindano.

“Huu umekuwa msimu wa kwanza na tunashukuru licha ya changamoto kadhaa tulizopitia kufuatia uwepo wa mashindano mbalimbali, unajua tumekuwa na CHAN halafu ligi yetu inakaribia kuanza, kwa hiyo tukawa tunaangalia tarehe gani tunaweza kufanya mashindano yetu ili iweze kufana vizuri.

“Mapokeo yamekuwa makubwa na huu ni msimu wa kwanza, tunaamini tutaboresha changamoto zilizojitokeza kuhakikisha msimu ujao tunakuwa na mashindano bora zaidi kwa idadi ya timu kuongezeka na hata kuongeza viwanja kwa sababu tumeona mahitaji ni makubwa, timu nyingi zimeonesha nia ya kushiriki na hizi zilizokuja zinasema msimu ujao tusiziache,” amesema Makau.

Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International, yalianza Agosti 31, 2025 na tamati yake ni leo Jumapili Septemba 7, 2025 ambapo utapigwa mchezo wa fainali.

Kabla ya mchezo wa fainali, uwanjani hapo itapigwa mechi ya hisani kati ya Fountain Gate dhidi ya JKU kuanzia saa 6:00 mchana.

Jumla ya timu kumi zimeshiriki ambapo sita zinatarajiwa kucheza Ligi Kuu Bara 2025-2026 ambazo ni wenyeji wa mashindano Fountain Gate, Namungo, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Coastal Union na Tabora United. 

Timu zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A limeundwa na timu za Fountain Gate, Tabora United na Eagle FC kutoka mkoani Manyara.

Kundi B ni Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union, huku Kundi C kuna Namungo, JKU ya Zanzibar, City FC Abuja kutoka Nigeria na TDS iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa inaibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.