NRA yaahidi mashine za EFD bure kwa wafanyabiashara

Tabora. Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketiya Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Almas Kisabya, amesema endapo atapata ridhaa ya kuliongoza Taifa, ndani ya siku 30 baada ya kuunda Baraza la Mawaziri, kipaumbele chake kitakuwa kuhakikisha mashine za kukusanyia mapato (EFD) zinatolewa bure kwa wafanyabiashara wote nchini.

Kisabya amesema hayo leo Jumapili, Septemba 7, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika katika eneo la Soko la Matunda, Kata ya Chem Chem, Manispaa ya Tabora.

“Ikiwezekana, tutatumia pia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kusaidia katika ukusanyaji wa mapato, kwa kuwa wao wameweza kudhibiti makusanyo bila kuingia kwenye migongano na wafanyabiashara,” amesema.

Aidha, ameongeza kuwa chama pia kitahakikisha wananchi wanapata huduma ya maji bure kwa kuweka mitambo ya usambazaji inayotumia nishati jadidifu kama sola na upepo.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Tabora wakimsikiliza mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NRA, Almas Hassani alipokuwa akinadi sera za chama hicho katika soko la matunda, leo Septemba 7, 2025. Picha na Hawa Kimwaga.



“Utaalamu upo kabisa, na tukitumia mfumo huu, wananchi watapunguza gharama za maji kwa kuwa mitambo ya kuvuta na kusambaza maji itatumia umeme wa jua au upepo. Hii inawezekana kabisa tukiwashirikisha wataalamu wetu,” amebainisha Kisabya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa NRA, Faridi Ramadhani, amesema chama hicho hakiwezi kususia uchaguzi kwa kuwa ni lazima kishiriki ili kuleta mabadiliko kwa wananchi na kuwapa haki zao.

“Uchaguzi haukimbii. Ni lazima tutafute haki kwa ajili ya wananchi. Mabadiliko hayatakuja bila kupiga kura na kumchagua kiongozi ambaye sera zake zinagusa maisha ya watu moja kwa moja,” amesema.

Naye mgombea ubunge kwa tiketi ya NRA Jimbo la Sikonge, Grace Kitundu, amesema ameamua kugombea kwa kuwa ana uwezo wa kuzungumzia changamoto za makundi yote katika jamii, likiwamo la watu wenye ulemavu.

“Nipeni ushirikiano, na mimi naweza kuleta mabadiliko katika maisha ya Watanzania, hususan wananchi wa Tabora. Mtu mwenye ulemavu anaishi changamoto nyingi, hivyo ni rahisi kuguswa na matatizo ya watu wengine,” amesema Kitundu.