Ombwe la midahalo mjadala | Mwananchi

Dar es Salaam. Licha ya shangwe, shamrashamra na furaha zinazoshuhudiwa katika mikutano ya kampeni za uchaguzi, kukosekana kwa midahalo ya wagombea urais inayorushwa mubashara kunatajwa kuwa ombwe katika demokrasia ya Tanzania.

Hii si ajali ya kisiasa ya msimu huu pekee. Ni utamaduni uliojengeka kwa zaidi ya miongo mitatu tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi na sasa imekuwa sehemu ya taswira ya siasa za uchaguzi nchini.

Licha ya wananchi kuonesha kiu ya mijadala hiyo kuhusu sera, midahalo ya urais imeendelea kusuasua na kushindikana, jambo linalowanyima wapigakura nafasi ya kulinganisha hoja za wagombea na kufanya uamuzi kwa msingi wa sera badala ya nderemo za mikutano ya hadhara.

Safari ya midahalo Tanzania ilianza kwa matumaini makubwa mwaka 1995, pale wagombea wawili wa urais, Augustine Mrema wa NCCR–Mageuzi na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF waliposhiriki mdahalo huo.

Hata hivyo, CCM iliwakilishwa na Dk Juma Ngasongwa badala ya mgombea wake, Benjamin Mkapa.

Matarajio hayo yalikufa ghafla katika uchaguzi wa mwaka 2000. Mkapa, aliyekuwa mgombea urais wa CCM, alikataa kushiriki.

Mpinzani wake mkuu, Mrema (wakati huo TLP), na wagombea wengine wa upinzani waligomea mdahalo, hivyo ukafutika kabla hata ya kuanza. Hapo ndipo ukajengeka mtindo wa Rais aliyepo madarakani hashiriki mdahalo.

Mwaka 2005 hali ikajirudia. Profesa Lipumba (CUF) alisema angejitokeza tu iwapo Jakaya Kikwete wa CCM angekubali mdahalo. Lakini CCM waligoma, mdahalo ukatupiliwa mbali.

Mwaka 2010, nafasi ya midahalo ilizidi kudhoofika. Rais Kikwete, aliyekuwa mgombea tena kupitia CCM, alikataa kushiriki. Baadhi ya wagombea wa upinzani, akiwamo Dk Willibrod Slaa wa Chadema, walijadiliana bila yeye, lakini mdahalo huo ulionekana hauna mashiko kwani mgombea wa chama tawala alikosekana.

Mwaka 2015 kulionekana mwanga mpya. Wagombea wakuu wote, akiwemo John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema, walikubali kushiriki.

Lakini siku chache kabla, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) lilijiondoa, jambo lililofanya kushindikane kupata urushaji wa kitaalam na mdahalo ukafa rasmi.

Wachambuzi wa siasa wanasema mizizi ya hali hiyo ipo katika utamaduni wa siasa za Tanzania unaotegemea zaidi mikutano ya hadhara kuliko mijadala ya sera.

Profesa Makame Ali Ussi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar anasema, “bado tunaamini mikutano ya hadhara ndiyo njia kuu ya kuwasilisha ujumbe. Kuna mtazamo kwamba kuonana ana kwa ana na wapiga kura ni njia bora zaidi ya kuwashawishi.”

Anasema mikutano ya hadhara huwapa wagombea faraja kubwa. Humo wanaweza kutoa ahadi za jumla kama viwanda, elimu bure, barabara na hospitali, bila kuhojiwa kuhusu utekelezaji au changamoto zinazoweza kujitokeza.

“Hapa ukubwa na shangwe za umati wa watu ndizo zinazoonekana kama kipimo cha mafanikio, badala ya uzito wa hoja na sera,” anaongeza Profesa Ussi.

Kwa upande mwingine, kuna mahesabu ya kisiasa baridi na ya makini. Dk Onesmo Kyauke kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema baadhi ya wagombea hukwepa mijadala kwa hofu ya kukutana uso kwa uso na wapinzani wao.

“Wagombea wengi huogopa kwamba kushiriki mdahalo kunaweza kumpa mpinzani umaarufu. Kwa mgombea aliye mbele kwenye mbio, mdahalo ni sawa na mtego, anategemewa afanye vizuri bila kosa, lakini akikosea kidogo anaweza kupoteza mengi,” anasema.

Kwa upande wa mgombea dhaifu, anasema mdahalo ni fursa ya kujitambulisha kwa Taifa zima na kupewa heshima ya kisiasa kwa kushiriki jukwaa moja na vigogo.

Hivyo basi, kiongozi anayetarajiwa kushinda huwa na sababu za mkakati za kutoshiriki midahalo.

Udhaifu wa kampeni zisizo za sera

Kikwazo kingine ni namna ujumbe wa kampeni unavyoundwa. Kampeni nyingi hazijengwi kwenye mijadala ya sera kwa kina, bali kwa ahadi za jumla kama inavyoelezwa na mchambuzi wa siasa, Dk Paul Luisillie.

“Wagombea wengi hawajitengi muda wa kuchambua sera zao kwa undani. Midahalo inahitaji uelewa wa kina wa masuala na uwezo wa kueleza msimamo kwa uwazi, jambo ambalo si rahisi kwa kila mgombea,” anasema.

Anasema kukwepa mijadala ya sera kumejenga mazingira yanayosababisha vyama kushindwa kuandaa ilani zilizohusisha tafiti za kina. Na bila ilani zenye nguvu, kampeni zinabaki bila mijadala ya maana.

“Na bila ilani, tafiti za kina, kampeni zetu kiasili zinakosa nguvu za kuendesha mdahalo wenye tija kwa Taifa,” anasema.