Othman afanya mazungumzo ya amani kuelekea uchaguzi mkuu

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (Jumaza), ikiwa ni mwendelezo wa kuhamasisha amani nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika leo, Septemba 7, 2025, ukumbi wa Jamat-Khan Mkunazini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, yameonesha Othman akisisitiza kwamba tunu ya taifa haiwezi kupatikana bila uadilifu wa kweli.

Pamoja na mazungumzo hayo, Othman amewakabidhi ripoti maalumu ya chama chake kuhusu hali halisi ya kisiasa nchini na nafasi yao katika kutafuta amani ya kudumu kuelekea uchaguzi.

“Sisi dhamira yetu ni ya kweli, pamoja na waasisi wa harakati hizi waliotetea maridhiano ya kisiasa nchini, ili kuhakikisha amani ya kudumu inakuwepo, kwa maslahi ya Taifa,” amesema Othman.


Othman, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na mtiania wa kuwania urais wa Zanzibar, ameainisha mambo na mapendekezo yanayofaa kutekelezwa, ambayo yeye na wenzake walikwishayawasilisha na kuyajadili pamoja na viongozi wakuu wa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kulinda amani dhidi ya machafuko kisiasa nyakati za uchaguzi.

Ametaja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa tume huru ya kuchunguza na kurekebisha sheria, marekebisho ya mfumo wa uchaguzi, na kuunda tume ya maridhiano ya kitaifa.

Amefafanua kuwa mapendekezo hayo, ikiwa yatazingatiwa kwa udhati, yanalinda maslahi ya taifa, lakini hayajatekelezwa, badala yake kuna viashiria vya kutendeka mabaya na maovu dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia.

“Tumeingia serikalini, hakuna lolote lililotekelezwa. Wajibu wetu ni kutanabahisha kwamba amani ikipotea, hasara haielekei kwa vyama vya siasa pekee, bali kwa nchi na taifa zima,” ameonya Othman.

Ameeleza kwamba lengo lao ni kudumisha haki na amani ya Taifa, si kulenga maslahi binafsi au kuwapumbaza wananchi.

Aidha, amewaomba viongozi wa dini kuchukua juhudi za makusudi na kutekeleza wajibu wao bila upendeleo, ili kuiponya amani ya Taifa, akisisitiza kuwa wananchi wamechoshwa na maafa na machafuko kila wakati wa uchaguzi.

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, amekumbusha na kushukuru juhudi za taasisi za dini, akisema zimekuwa na mchango mkubwa kwa amani na mshikamano wa watu wa visiwa hivi.

“Sisi nia yetu ni safi, na ndiyo maana tunazidi kuhimiza ujenzi wa amani na kulinda maslahi ya nchi, pamoja na yaliyotokea dhidi yetu na wananchi wetu,” amesema Jussa.

Amewataka viongozi wa jumuiya hiyo kuendelea kupaza sauti ya haki ili kuhimiza amani, kwaajili ya kuinusuru Taifa. Amir wa Jumuiya Maimamu Zanzibar (Jumaza), Sheikh Farid Hadi Ahmed, amesema ni vyema kuwe na amani ya kudumu kama dira ya kila upande, bila upendeleo, sambamba na kuzingatia siasa za haki, zenye maadili, na kuzuia machafuko au fitna.

Sheikh Farid ametoa wito kwa Serikali na viongozi wote kuchunga dhima yao kwa wananchi, wasivunje amani, huku akihimiza dua za kuendeleza maridhiano.

Katibu wa Jumaza, Sheikh Ali Abdalla Amour, naye amekumbusha wajibu wa kila upande kuheshimu haki ili kuhakikisha amani inatamalaki nchini.