Karatu. Wabunge waliomaliza muda wao, Cecilia Paresso (Viti Maalumu, Arusha) na Daniel Awack (Karatu), wamesema hawana tofauti binafsi, bali ushindani uliokuwapo awali ulikuwa wa kidemokrasia kwa lengo la kuwatumikia wananchi.
Kauli hizo zimetolewa leo Jumapili, Septemba 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Mang’ola.
Paresso amesema mwaka 2020 aligombea ubunge wa Karatu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mshindani wake mkuu alikuwa Awack wa Chama cha Mapinduzi (CCM), aliyekuwa mshindi.
Baada ya kuhamia CCM, Paresso alishiriki kura za maoni dhidi ya Awack, ambapo vikao vya juu vya chama vilimteua Awack kugombea ubunge kwa mara ya pili.

Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Arusha aliyemaliza muda wake, Cecilia Paresso akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni za mgombea ubunge wa Jimbo la Karatu kupitia Chadema, Daniel Awack uliofanyika leo Septemba 7, 2025 katika Kata ya Mang’ola, mkoani Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu.
“Mwaka 2020 nilisimama kwenye majukwaa nikisema, ‘Msimchague Awack, mnichague mimi.’ Leo nipo mbele yenu namwombea kura nyingi. Ushauri wangu ni kuwa siasa isiwekwe moyoni, utaumia. Iwekeni kwenye mapafu, ili ikipumuliwa itoke,” amesema Paresso.
Ameeleza kuwa atafanya kampeni za kimkakati kuwaombea kura wagombea wa CCM, kuanzia mgombea kiti cha urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, hadi wabunge na madiwani, hususan katika Kanda ya Kaskazini.
Kwa wakulima wa vitunguu wa Bonde la Eyasi, Paresso amesema Serikali imetenga Sh21 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa bwawa kubwa katika Kijiji cha Qanded, litakalosaidia wakulima na wafugaji.

Ameongeza kuwa bajeti ya kilimo imeongezeka hadi Sh1.2 trilioni, jambo lililosaidia kuimarisha upatikanaji wa mbolea ya ruzuku na kusambazwa tani milioni 1.2 zenye thamani ya Sh693 bilioni kwa wakulima zaidi ya milioni nne nchi nzima.
Kadhalika, amesema eneo la kilimo cha umwagiliaji limeongezeka kutoka hekta 694,715 hadi 727,280 kufuatia kukamilika kwa skimu mpya 16, ukarabati wa skimu 48, na ujenzi unaoendelea wa skimu 50, ikiwemo ya Mang’ola.
“Nimeamua kuwaombea kura wagombea wa CCM kutokana na uwezo aliouonesha Rais Samia. Ninaamini ataendelea kufanya makubwa zaidi iwapo tutampigia kura nyingi za kishindo. Tayari masoko ya kisasa 33 yamejengwa nchi nzima katika kipindi chake,” amesema.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Karatu, Daniel Awack, amewahakikishia wananchi kuwa ataendeleza kasi ya maendeleo iwapo watampa ridhaa kwa mara ya pili.
Amesema kipaumbele chake kitakuwa kuboresha huduma za afya kwa kununua gari la kubebea wagonjwa, litakalosimamiwa na ofisi ya mbunge.
“Ninawaomba mniamini, kwa awamu ya pili tushirikiane kusukuma mbele kasi ya maendeleo. Tumchague Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwaletea wananchi wa Karatu maendeleo ya kweli,” amesema Awack.