Polisi walivyoyazima maadhimisho ya Chadema

Dar/Mikoani. Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hayakufanyika, baada ya viongozi wake wa ngazi ya kanda kujikuta mikononi mwa polisi, huku wengine wakizuiliwa kufika eneo la tukio.

Hata hivyo, alipotafutwa Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, kuzungumzia matukio hayo, simu yake iliita bila kupokelewa, na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa.

Maadhimisho hayo yalipangwa kufanyika leo, Jumapili Septemba 7, 2025, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa chama hicho kuwakumbuka mashujaa waliopigania demokrasia nchini.


Shughuli za maadhimisho hayo ziliambatana na masuala mbalimbali, ikiwemo kusafisha makaburi ya makada na viongozi wa Chadema waliotangulia mbele ya haki, lakini pia walikuwa na lengo la kuwatembelea na kutoa misaada ya kibinadamu kwa familia za watu hao waliowaita mashujaa.

Dalili za kukwama kwa maadhimisho hayo zilianza kuonekana jana, Jumamosi Septemba 6, 2025, wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro lilipowazuia na kuwakamata viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), kwa madai ya kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria eneo la Sambarai Kibosho, wilayani Moshi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel, msafara wa viongozi wa Bavicha ulizuiwa na polisi ukiwa njiani kuelekea nyumbani kwa kina Deusdedith Soka kama sehemu ya kumuenzi kiongozi huyo.

“Magari ya polisi yamezuia msafara huo takribani mita 100 kutoka barabara ya Kibosho, Kilimanjaro. Ni dhahiri hatua hii haikuwa ukaguzi wa kawaida, bali ni mahususi ya kuzuia msafara kuendelea na shughuli zake kwa amani,” amesema Welwel.


Soka, aliyekuwa mwenyekiti wa Bavicha wilayani Temeke na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise, walitoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Agosti 18, 2024, hadi sasa bado hawajulikani mahali walipo.

Ikumbukwe kuwa Chadema imezuiwa kufanya shughuli zozote kwa muda, ikiwemo za kisiasa na Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Hatua hiyo inatokana na shauri lililofunguliwa na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutoka Zanzibar, wanaolalamikia mgawanyo wa rasilimali za chama usio sawa kati ya Bara na Zanzibar na upendeleo na ubaguzi.

Mapema leo, askari polisi wakiwa kwenye magari walionekana wakiwa wameimarisha ulinzi katika barabara zinazoelekea kwenye ofisi za Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambako viongozi wa Chadema walipanga kufanya maadhimisho ya Siku ya Mashujaa.

Mkoani Shinyanga nako, Jeshi la Polisi mkoani humo linadaiwa kuwakamata viongozi wakuu wa Chadema wa Kanda ya Serengeti (Shinyanga, Simiyu na Mara) waliokuwa kwenye kaburi la Bob Makani wakifanya usafi.


Bob Makani ni mmoja wa waasisi wa Chadema, na amewahi kuwa mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2003.

Waliokamatwa ni pamoja na Jackson Mnyawami (Katibu wa Chadema), pamoja na viongozi wengine waandamizi wa mkoa wa Shinyanga wakiwemo wenyeviti na makatibu wa wilaya na majimbo.

Mkoani Mwanza, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria (Mwanza, Geita na Kagera), Zakari Obadi na wenzake wanashikiliwa na polisi wakidaiwa kutaka kuadhimisha Siku ya Mashujaa.

Inadaiwa kuwa polisi walizingira Kanisa Katoliki Kirumba, ambako viongozi wa Chadema Kanda ya Victoria walipanga kuadhimisha siku hiyo ya mashujaa wao.

Viongozi wanne wa Chadema mkoani Mbeya wanadaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kuvaa sare za chama hicho kanisani.

Wanaodaiwa kukamatwa leo, Jumapili Septemba 7, 2025, ni pamoja na Katibu wa chama hicho, Hamadi Mbeyale, Mwenyekiti wa Bavicha mkoa na viongozi wawili wa majimbo wa nafasi ya wenyeviti.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Masaga Kaloli amesema viongozi hao wamekamatwa wakiwa kanisani huko Mtaa wa Ndato, Kijiji cha Ndaga wakiendelea na ibada.

Amesema chama hicho kilikuwa kikifanya ibada maalumu ya kuwaombea makada wake waliotekwa na kupotezwa, akiwemo aliyekuwa mwanaharakati, Mdude Nyagali.

“Wamekamatwa na wapo Kituo cha Polisi Tukuyu kwa kosa la kuvaa sare za chama kanisani. Hii siyo kosa, tumeandika maelezo ili kuachiwa, wakikwama tutachukua hatua nyingine kwa kuwa walikuwa katika ibada,” amesema Kaloli.

Hata hivyo, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa, amekiri makada na viongozi wao kushikiliwa na polisi kwenye maeneo mbalimbali wakitaka kufanya maadhimisho ya Siku ya Mashujaa.

Alipoulizwa kama wana kibali, alijibu: “Haya ni mambo ya ndani, hayahitaji kibali, ni tukio tunalolifanya kwenye ukumbi. Hadi sasa bado hatujajua ni wangapi wameshakamatwa, tunaendelea kukusanya taarifa.”