Polisi yaeleza sababu ya kuwashikilia waandishi wawili Arusha

Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia waandishi wa habari wawili kwa tuhuma za kuendesha televisheni za mtandaoni (online TV) ambazo hazijasajiliwa kisheria.

Waandishi hao ni Baraka Lucas, anayefanya kazi na Jambo TV, na Ezekiel Mollel wa Manara TV.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo, Jumapili, Septemba 7, 2025, na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, David Misime, hatua hiyo imechukuliwa baada ya uchunguzi ulioanza mapema, ambao ulikusanya vielelezo kuhusiana na tuhuma zinazowakabili.

“Jeshi la Polisi lingependa kutoa ufafanuzi kuhusiana na waandishi wa habari waliokamatwa na kushikiliwa kwa mahojiano na kukamilisha ukusanyaji wa vielelezo. Wanatuhumiwa kuendesha online TV zao binafsi ambazo hazijasajiliwa, kinyume na Kanuni za Maudhui Mitandaoni za mwaka 2020, zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2022, chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Waandishi hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha tangu jana, Jumamosi, Septemba 6, 2025. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta) Musa Juma, amesema chama kinashughulikia suala hilo kwa karibu ili kuhakikisha waandishi hao wanapewa dhamana.

“Tuko polisi tangu jana tunahangaika na hili suala. Tunaomba wapewe dhamana wakati taratibu nyingine zinafuata,” amesema Juma ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha.

Wakili anayewatetea wandishi hao, Ally Mhyellah, amesema alifika kituoni akibainisha kuwa malengo yake ni kusimamia maelezo ya wateja wake, kusikiliza kutoka kwao kilichotokea, na kushughulikia dhamana.

“Nilikuja kwa ajili ya kusimamia wakiandika maelezo, tayari wameshachukuliwa maelezo. Nilitarajia kuonana nao ili wanieleze kilichojiri, lakini nimeambiwa nisubiri wapelelezi warejee ili tuone suala la dhamana litakavyokuwa,” amesema Mhyellah.