Dar es Salaam. Ndoa na uhusiano wa kimapenzi ni safari ya maisha yenye changamoto, mafanikio na mafunzo.
Ili ndoa au uhusiano udumu, kuna mambo ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa na wanandoa au wapenzi, ambayo makala haya itayaangazia.
Mojawapo ya mambo hayo ni mawasiliano. Haya ni moyo wa uhusiano wowote. Wanandoa au wapenzi wanapaswa kuwa na uwezo wa kuzungumza kwa uwazi kuhusu hisia, matarajio, na matatizo yao.
Mawasiliano ya wazi huondoa mashaka na kuleta uaminifu. Kutozungumza hujenga ukuta kati ya wapenzi, huku ukimya ukizaa tafsiri za uongo, mashaka, na hisia za kutengwa.
‘’Mawasiliano si tu kusema, bali kusikiliza kwa makini. Wanandoa wengi huingia matatizoni si kwa sababu ya kutokupendana, bali kwa sababu ya kutoelewana,’’ anasema Dk John Gottman, mtaalamu wa saikolojia ya ndoa na mwanzilishi wa taasisi ya The Gottman.
Mtaalamu mwingine wa saikolojia na uhusiano wa kimapenzi, Esther Perel, anaeleza: ‘’Uhusiano wenye afya unajengwa juu ya msingi wa mazungumzo ya kweli na ya wazi. Bila mawasiliano, hata upendo mkubwa unaweza kufifia.’’
Jingine ni heshima. Kumheshimu mwenza ni pamoja na kumsikiliza, kutomtukana, na kutoonyesha dharau mbele ya watu au hata faraghani.
Heshima pia inahusisha kuthamini mawazo ya mwenza, kuepuka matusi, kejeli au dhihaka na kuonyesha unyenyekevu hata wakati wa kutoelewana.
Kukosa heshima mara nyingi husababisha migogoro mikubwa isiyokuwa na mwisho.
‘’Heshima ni nguzo ya msingi katika mapenzi. Bila heshima, mapenzi hubadilika kuwa mashindano ya nguvu badala ya uhusiano wa upendo, ‘anasema Dk Emerson Eggerichs, mtaalamu wa ndoa na mwandishi wa kitabu Love and Respect.
Upendo ni kitu cha kipekee kinachowapa watu nguvu ya kushinda changamoto za maisha. Upendo wa kweli hauangalii hali au mali bali unaangalia utu na thamani ya mtu.
Katika ndoa au uhusiano, upendo wa dhati hujionyesha kwa vitendo, kusaidiana, kuhangaikia hisia za mwenza, na kutoa msaada bila masharti.
Hakuna mtu mkamilifu. Makosa ni sehemu ya maisha, na katika ndoa au uhusiano, ni lazima kusamehe na kusahau. Chuki, kinyongo, na kutosamehe husababisha kuvunjika kwa uhusiano. Kusamehe hakuonyeshi udhaifu bali ni ishara ya upendo na ukomavu wa kiakili.
Mnapokoseana, ni vyema kuzungumza kwa utulivu, kuomba msamaha, na kuonyesha nia ya kutobadilika. Bila msamaha, hata mapenzi ya dhati hayawezi kudumu.
Katika jamii nyingi, kuhusisha imani au maadili ya kiroho ni jambo la msingi katika uhusiano.
Ndoa zinazomweka Mungu au maadili ya kiroho mbele huwa na utulivu zaidi, kwani maombi na imani huleta msamaha, subira, na hekima ya kushinda mitihani.
Kuomba pamoja, kuhudhuria ibada au kujifunza mafunzo ya kiroho pamoja huimarisha ushirikiano wa kiroho, ambao ni msingi wa kuvumiliana na kutokata tamaa.
Katika maisha ya sasa yenye shughuli nyingi, ni rahisi kusahau thamani ya kuwa na mwenza. Ni muhimu kutenga muda wa kuwa pamoja kama wapenzi, iwe ni kuzungumza jioni, kutembea pamoja, au kupanga matembezi ya kimahaba.
Ndoa au uhusiano si kazi ya mtu mmoja. Kila upande unapaswa kuwa tayari kushirikiana katika majukumu ya kifamilia, kifedha, na kijamii.
Kujua kuwa mwenza wako yupo bega kwa bega huongeza mapenzi, uaminifu na mshikamano. Ikiwa mwanandoa mmoja ana mzigo wote wa kazi au majukumu, huweza kujisikia kuchoka au kuumia kihisia.
Kujifunza na kukua pamoja
Uhusiano mzuri ni ule unaowaweka wanandoa pamoja kiakili, kiroho, kifedha na kihisia. Hili linaweza kufikiwa kwa kujifunza pamoja, kushauriana, kuwekeza pamoja, au kuanzisha miradi ya pamoja. Maisha hubadilika, na watu pia hubadilika, hivyo mnapojifunza na kukua pamoja, mnakuwa na nafasi ya kuendana na mabadiliko hayo bila migogoro.
Wenza wanaojifunza pamoja hujenga uhusiano wa kina unaodumu kwa muda mrefu.
Mapenzi na mvuto wa kimapenzi ni vitu muhimu katika kudumisha moto wa uhusiano. Wanandoa au wapenzi wanapaswa kuendeleza mapenzi ya kimwili kwa njia ya kuheshimiana, kuboresha muonekano wao, na kushirikiana katika matamanio ya kila mmoja.
Kukosa mahaba kunaweza kusababisha hisia za kukataliwa au kupungukiwa, hivyo ni muhimu kulipa jambo hili uzito.
Uhusiano ni kama bustani, unapoipa maji, mwangaza na huduma, inachanua. Lakini ukiiacha tu, hufifia. Kwa hiyo, kila mmoja katika uhusiano, anapaswa kujitahidi kila siku kuwekeza katika uhusiano wake.