Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa usiku wa leo, Septemba 7, 2025, wananchi wataushuhudia mwezi ukipatwa kwa muda wa takriban saa sita.
Kwa mujibu wa TMA, tukio hilo litaanza kwa kupatwa kwa sehemu ya mwezi mara baada ya jua kuzama na kuendelea hadi saa 2:29 usiku.
Baada ya hapo, mwezi utapatwa kikamilifu kuanzia saa 2:30 hadi saa 3:52 usiku, kabla ya kuhitimishwa tena kwa kupatwa kwa sehemu kuanzia saa 3:53 hadi 5:55 usiku.
“Hii ni nafasi adimu ya kushuhudia tukio kubwa la kiastronomia. Anga linatarajiwa kuwa angavu hivyo wananchi wanaweza kuliona kwa macho bila madhara yoyote,” imesema taarifa ya TMA.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa kwa kawaida, mzunguko wa mwezi una uhusiano wa karibu na kupwa na kujaa kwa maji baharini, hivyo kina cha maji kinatarajiwa kuongezeka wakati wa tukio hilo, ingawa hakuna madhara yoyote yatakayotokea.
Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushuhudia kupatwa kwa mwezi kikamilifu tangu mwaka 2022, jambo linalotarajiwa kuwavutia wataalamu wa anga na wananchi wa kawaida.
Endelea kufuatilia Mwananchi