Thamani ya Yanga yaizidi hadi Al Ahly

MWENYEKITI wa Kamati ya Mabadiliko ya Mfumo wa Uendeshaji wa Klabu ya Yanga, Alex Mgongolwa, amesema kwa sasa thamani ya timu hiyo imefikia kiasi cha Sh100 bilioni.

Thamani hiyo ni kubwa kuliko hata iliyo nayo klabu ya Al Ahly ambayo ni Euro 30 Milioni ambao ni zaidi ya Sh 88 bilioni) ikiwa ni zaidi ya Sh 12 bilioni na kuifanya Yanga sasa kuwa klabu yenye thamani kubwa zaidi barani Afrika kwa muktadha huyo uliotangazwa mkutanoni.

Mgongolwa amezungumza hayo leo Septemba 7, 2025, katika mkutano mkuu wa klabu hiyo unaofanyika kwenye ukumbi wa Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam.

“Nichukue nafasi hii kuwaambia rasmi wanachama wa Yanga, thamani ya timu yetu imefikia Sh100 bilioni,” amesema Mgongolwa.

Mgongolwa amezungumza hayo baada ya kupewa nafasi na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Saidi kwa ajili ya kutoa ripoti ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.

Katika mkutano wa leo, umehudhuriwa na jumla ya wanachama 627 kutoka katika matawi mbalimbali 163 ya timu hiyo.

Mkutano huo ukiwa ni wa mikakati mipya ya klabu hiyo kwa msimu mpya wa mashindano wa mwaka 2025-2026 ikiwa ina kazi ya kutetea mataji ya Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho, Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano, lakini ikiwa na kibarua cha Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga imepangwa kuanza mechi za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola siku chache baada ya kumalizana na Simba katika Ngao ya Jamii itakayochezwa Septemba 16.