Dar es Salaam. Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikiendelea, wagombea urais na wagombea wenza wametumia tatizo la ajira kama turufu ya kuwashawishi wananchi kuwapigia kura katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Kinachofanya ajira itumike kama kete ya ushindi kwa wanasiasa ni uhalisia wa ukubwa wa tatizo lenyewe.
Mathalan, takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha ni watu milioni nne pekee ndiyo wameajiriwa katika sekta isiyo rasmi.
Uchaguzi mkuu wa 2025 unapokaribia, vyama vya siasa vimelazimika kulivalia njuga suala hilo na kujipambanua kupitia ilani zao na ahadi majukwaani.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa madarakani kwa muda wote tangu Taifa lilipopata uhuru, Desemba 9, 1961, kikiibuka na sera na mikakati tofauti kuhusu suala la ajira kila awamu ya uongozi.
Katika ahadi yake inayonadiwa kwenye kampeni zinazoendelea, mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan anaahidi kuzalisha ajira milioni 8.5 kwa miaka mitano ijayo. Ajira hizi zinadaiwa kutokana na fursa mbalimbali kutoka sekta binafsi, miradi ya maendeleo na ajira rasmi serikalini.
NLD yaja na ajira si fadhila, ni haki
Chama cha National League for Democracy (NLD) kupitia ilani yake ya mwaka 2025, kimeweka ajira kwa vijana kama moja ya nguzo kuu za mageuzi yake. Chama hicho kimeunganisha dira yake na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kikieleza bayana kuwa Taifa la kesho litajengwa na vijana wenye maarifa na ujuzi wa vitendo.
Mikakati ya chama hicho inajikita kwenye maeneo makuu matatu, elimu, uchumi na teknolojia.
Chama hicho kimeahidi elimu bure hadi kidato cha sita na vyuo vya kati, sambamba na kurekebisha mitalaa ili iendane na mahitaji ya soko.
Somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ubunifu na stadi za maisha limepewa kipaumbele kwa malengo ya kumtoa kijana wa Tanzania kwenye nadharia za darasani na kumuingiza moja kwa moja kwenye soko la ajira.
Mbali na elimu, NLD imeanzisha Mpango wa Vijana kwa Kazi, unaolenga kutoa mafunzo ya vitendo ya miezi 6–12 kwa kila mhitimu.
Lengo ni kuhakikisha vijana hawabaki na vyeti vya karatasi tu bali wanakuwa na uwezo wa kujiajiri au kuajiri wenzao.
Aidha, chama hicho kimepanga kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Uwezeshaji Vijana utakaotoa mikopo isiyo na riba na vituo vya mjasiriamali katika kila halmashauri. Hatua hii inalenga kuvunja mnyororo wa vijana kutegemea ajira serikalini badala yake kujenga kizazi cha wajasiriamali chipukizi.
Katika uchumi, NLD imeibuka na falsafa ya Kijiji Kimoja, Bidhaa Moja, ikipendekeza kila kata iwe na kiwanda kidogo kinachozalisha bidhaa kwa kutumia rasilimali zilizopo. Hii inalenga kuongeza ajira rasmi na kuimarisha uchumi wa ndani.
Kwa upande wa teknolojia, NLD imetangaza Digital Youth Empowerment Program, mpango maalumu wa kufundisha vijana matumizi ya akili bandia (AI), Tehama na ubunifu katika kilimo, afya na biashara.
Chama kinasisitiza kuwa, mapinduzi ya ajira hayatakuja bila vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali, hata hivyo chama hakioneshi kwa kiwango gani kimedhamiria kupunguza tatizo hilo kitakwimu.
CUF na usawa katika ajira
Chama cha Wananchi (CUF) kupitia ilani yake inayotetewa na mgombea wake wa urais wa Tanzania, Samandito Gombo kimeahidi ajira milioni tano katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
CUF imeweka ahadi kuwa itasimamia misingi ya haki na usawa kwa vijasna na wanawake kwenye fursa za ajira kupitia sekta za kilimo, viwanda na mifumo bora ya ajira nchini itakayowekwa na Serikali ya umoja wa kitaifa ili kunufaisha makundi yote.
Ada-Tadea na mikakati kabambe
Chama cha Ada-Tadea kupitia ilani yake ya 2025–2030, kimekuja na kaulimbiu ya Mapinduzi ya Njano (Yellow Revolution). Falsafa hii inalenga mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kiteknolojia, kuchochea ajira kwa vijana.
Moja ya maeneo yaliyotajwa kuzalisha ajira hizo ni kufufua na kuanzisha viwanda vya kimkakati. Viwanda vilivyokufa kama General Tyre, Mwatex na Mutex vimepangwa kufufuliwa na viwanda vipya kujengwa ili kuzalisha nafasi za ajira kwa vijana.
Serikali itakayoundwa na Ada -Tadea kwa mujibu wa ilani, itawapa vijana nafasi ya kwanza katika ajira za utumishi wa umma ili kuwapa uzoefu.
“Vijana wanahitaji uzoefu wa vitendo, na serikali itawapa nafasi hiyo,” inasomeka sehemu ya ilani hiyo.
Mbinu kubwa ya chama hicho ni ujenzi wa Bongo City, jiji la teknolojia litakalokuwa kitovu cha uvumbuzi wa kidigitali.
Kupitia Bongo City, vijana wabunifu wanatarajiwa kushiriki kwenye miradi ya kiteknolojia kuanzia simu janja, mitandao ya kijamii hadi huduma za kifedha.
Chama hicho kinaamini mpango huo utazalisha ajira mpya za kidigitali na kulibadili Taifa kiuchumi. Chama hicho kinaahidi kuwa vijana watapewa ardhi na kuhusishwa katika sekta za kilimo ili kuondoa utegemezi wa vijana mijini.
AAFP kilimo, ujasiriamali
Kwa upande wake, Alliance for Africa Farmers Party (AAFP) imekuja na sera zinazomlenga kijana wa kijijini.
Ilani yake maarufu ya Darubini ya Uchumi Tanzania, inalenga kugeuza kilimo na ujasiriamali kuwa injini ya ajira.
AAFP imeweka wazi kwamba, kipaumbele chake ni kilimo bora, ufugaji wa kitaaluma na uvuvi wa kisasa. Vijana wanatarajiwa kupewa elimu ya uzalishaji, masoko ya uhakika na teknolojia ya umwagiliaji ili kuongeza tija.
Ikijipambanua kama chama cha wakulima, AAFP imeahidi huduma za msingi kwa wakulima kama pembejeo za kilimo na nishati bure.
Hatua hizi, kwa mujibu wa chama hicho, zitawaondolea vijana mzigo wa gharama na kuwawezesha kujikita kwenye uzalishaji.
Mbali na vyama hivyo, vyama vingine vyote vimesimamia ajenda ya ajira kwa unyeti vikitofautiana mikakati tu.
Chaumma na ajira kwa vijana
Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeweka kipaumbele kikubwa katika ajira kwa vijana kupitia kilimo, rasilimali za taifa na kuvutia uwekezaji.
Kupitia mgombea wake wa urais, Salum Mwalimu anayejinadi kwa sera ya vijana ‘Rais wa masela,’ Chaumma inaweka ahadi yake kuu ya kupigania ajira kwa vijana ndani ya siku zake 100 madarakani.
Pamoja na tofauti za mikakati inayowekwa na vyama na wagombea, vyama vyote vinakubaliana jambo moja kuu kuwa tatizo la ajira kwa vijana ni la dharura na linahitaji hatua za haraka.
Hata hivyo, suala la takwimu katikia mipango ya wagombea linakosekana, wengi wakiweka misingi ya kutatua bila kuwa na makadirio ya kiwango cha utatuzi wanachokusudia.
Tafiti zinaonesha ushiriki wa nguvu kazi ya vijana ukiendelea kushuka kwa kipindi cha hivi kiaribuni, hali ikiwa ni asilimia 83.0 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 75.2 katika maeneo ya mijini.
Kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi wa ILFS, 2021, Tanzania ina nguvu kazi ya watu milioni 25.86 huku asilimia 57 kati yao wakiwa ni vijana. Utafiti huo unaonesha kuwa, nguvu kazi ya vijana imepungua mchango wake kwa takribani asilimia 4.2 kutoka asilimia 84.5 mwaka 2014 hadi asilimia 80.3 mwaka 2021.
Mbali na takwimu hizo, inakadiriwa zaidi ya vijana milioni moja huingia sokoni kusaka ajira kila mwaka huku 200,000 pekee hupata ajira, hivyo 800,000 wanaobaki huendelea kuzunguka bila uhakika wa ajira.
Hii inadaiwa kuvuka wastani wa ukosefu wa ajira wa Taifa wa asilimia nane hadi kufikia asilimia 12.2 ya tatizo.
Mchambuzi mkongwe wa masuala ya siasa na utawala bora nchini, Benson Bana anasisitiza kuwa suala la ajira linahitaji mikakati ya uwekezaji wa miradi ili iweze kutoa nafasi kwa vijana wafanye kazi wapate malipo yao, waendeshe maisha.
“Ajira iwe katika sekta za umma au binafsi, zote zinataka uwekezaji wa miradi na mipango itakayowapa watu nafasi ya kufanya kazi na kujipatia kipato halali, lazima kuwe na miradi na miundombinu kama viwanda, taasisi na mifumo itakayotoa nafasi kwa watu kufanya kazi ili wapate pesa,” anasema.
Mwanazuoni huyo aliyekuwa mhadhiri mwanadamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasisitiza wanasiasa kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu inayotekelezeka kushughulikia tatizo hilo.
“Ajira hazinyeshi kama mvua, wanasiasa waseme mikakati yao ya kila mwaka na ya muda mrefu kuhusu miradi watakayoibua ili iajiri vijana. Wasomi wanaomaliza vyuo wapewe njia za uzalishaji wa ajira, fursa rasmi ya ajira ni uzalishaji mali, uchuuzi siyo ajira,” amesema na kuongeza.
“Mataifa yote yanashida ya ajira, wagombea ni vyema wakaweka wazi ilani zao mitandaoni na kwenye vyombo vya habari, kwani Watanzania wa sasa wanafuatilia mambo si kama wa zamani.”