Same. Mgombea mteule wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri, amewataka wanachama wa chama hicho katika Jimbo la Same Mashariki kuvunja makundi na kuungana kwa pamoja ili kuhakikisha wagombea wa CCM wanashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Bushiri ametoa wito huo alipozungumza katika mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge wa Same Mashariki, Anna Kilango Malecela, uliofanyika katika Kata ya Maore.
Amesema, katika kipindi cha kura za maoni ndani ya chama, kila mmoja alikuwa na timu yake, lakini sasa makundi hayo yanapaswa kuunganishwa kwa lengo la kushinda uchaguzi.
“Sisi tunajua kila mtu alikuwa na mtu wake kwenye kura za maoni, lakini sasa tumeshapata mgombea urais, ubunge na udiwani. Ni wakati wa kusimama pamoja, kuvunja makundi na kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo ili kujihakikishia maendeleo ya kweli,” amesema Bushiri.

Aidha, amewataka wananchi kuepuka kudanganywa na wanasiasa aliowaita “wasanii wa siasa”, akisema wamekuwa wakieneza maneno ya uongo ili kujipatia kura bila kuwa na uwezo wa kuwaletea maendeleo.
Amesisitiza kuwa CCM ndicho chama pekee kinachoweza kuwaletea maendeleo ya kweli na kuwaomba wananchi kutofanya makosa kwenye uchaguzi huo.
Katika mkutano huo, Bushiri pia amewaomba wananchi wa Same Mashariki kumchagua tena Anna Kilango, akisema ni kiongozi mwenye rekodi nzuri ya kupigania miradi ya maendeleo ya jimbo hilo.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Same Mashariki, ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwemo maboresho katika sekta ya elimu, afya na miundombinu ya barabara.
Kilango amesema Serikali imekubali kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kisiwani–Mkomazi–Same yenye urefu wa kilometa 101, hatua ambayo itaboresha uchumi wa wananchi, hasa wakulima wa zao la tangawizi.
Pia, ameahidi kusimamia ujenzi wa barabara ya Mwembe–Miamba–Ndungu yenye urefu wa kilometa 90.1.
“Niwahakikishie, mkinipa nafasi nitahakikisha tunaendelea kusimamia ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafiri na biashara za wananchi. Pia, shule nyingi zimechakaa na zinahitaji kujengwa upya. Serikali imeanza kutoa fedha kwa ajili ya kuziboresha, nami nitasimamia kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati,” amesema Kilango.
Ameongeza: “Niwaombe wananchi mnipe nafasi ili niendelee kuwa msemaji wenu bungeni na kuhakikisha Same Mashariki inasonga mbele kimaendeleo.”