Dar es Salaam. Watoto ni zawadi ya kipekee kutoka kwa Mungu na ni hazina ya jamii yoyote ile. Ndani yao kuna ndoto, matumaini na mustakabali wa kizazi kijacho.
Watoto wanapozaliwa, huja na mioyo isiyo na chuki, malengo ya maisha ambayo bado hayajachafuka na uwezo mkubwa wa kujifunza na kuleta mabadiliko.
Kwa msingi huo, ni wajibu wa kila mtu, mzazi, mlezi, jamii na serikali kuhakikisha kuwa watoto wanaenziwa, wanalindwa, na wanatunzwa ili wakue katika mazingira bora yatakayowawezesha kufikia ndoto zao.
Watoto ni tunu kwa sababu wanabeba maisha ya baadaye. Taifa lisiloenzi watoto wake halina hakika ya kesho.
Misingi ya utu, maadili na maendeleo hujengwa mapema kabisa katika maisha ya mtoto. Pale mtoto anapopewa malezi bora, elimu nzuri, lishe sahihi na upendo wa kweli, basi tunakuwa tumewekeza katika kizazi kitakachokuwa na maadili, akili timamu na uwezo wa kuchangia maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
Katika tamaduni nyingi za Kiafrika, watoto walionekana kama kiungo cha jamii, na kila mtu alikuwa na wajibu wa kuchangia katika makuzi yao. Walikuwa ni kielelezo cha furaha, baraka na ustawi.
Hata leo, tunapaswa kuendeleza fikra hizi na kuhakikisha kuwa watoto hawabaguliwi, hawadhulumiwi wala kutelekezwa.
Kuwaenzi watoto kunaanza kwa kuwaheshimu kama binadamu wenye hisia, mahitaji na haki zao. Ni kosa kudhani kwamba kwa sababu mtoto ni mdogo, basi hana maamuzi au maoni ya kuchangia.
Tunapowaenzi watoto, tunawahusisha katika maamuzi yanayohusu maisha yao, tunawasikiliza na kuwathamini. Tunaacha lugha na matendo ya kuwavunjia heshima kama vile kuwatukana, kuwapiga hovyo au kuwadhalilisha mbele za watu.
Kuwaenzi watoto pia kunahusisha kuwatambua kama watu muhimu na kuwawekea mazingira bora ya kujifunza, kucheza na kukuza vipaji vyao. Tunaenzi watoto kwa kusherehekea mafanikio yao, hata yale madogo, na kwa kuwajenga kisaikolojia kuwa watu wanaojiamini.
Ulinzi wa watoto ni jukumu la kila mmoja wetu. Leo hii, watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi kama ukatili wa kijinsia, ajira ya utotoni, ndoa za utotoni, na mifumo ya malezi isiyo rafiki.
Tunapaswa kusimama kidete dhidi ya aina yoyote ya ukatili kwa watoto, iwe inafanyika nyumbani, shuleni au mitaani.
Jamii inapaswa kuwa macho na kutoa taarifa kwa vyombo husika pale wanaposhuhudia mtoto akidhulumiwa.
Vilevile, wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha kwamba watoto wao hawatumbukii kwenye makundi mabaya au mazingira hatarishi kama vile uraibu wa dawa za kulevya au ukahaba wa mtaani.
Sheria na sera zinazolinda haki za watoto zinapaswa kutekelezwa kwa vitendo. Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya kijamii, inapaswa kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto kwa kutoa elimu, misaada na msaada wa kisaikolojia kwa watoto waliotendewa vibaya.
Kuwatunza watoto kunamaanisha kuwapa mahitaji yao ya msingi kama chakula bora, mavazi, malazi salama, huduma za afya na elimu. Watoto wanaohitaji huduma maalum, kama watoto wenye ulemavu, wanastahili huduma bora zaidi na zenye kuzingatia hali yao.
Malezi ya upendo, huruma na msamaha huwajenga watoto kuwa watu wema. Watoto wasipotunzwa vyema, huweza kuwa watu wakorofi, wenye hasira, chuki na kukosa mwelekeo maishani.
Kinyume chake, watoto wanaopata malezi mazuri hukua kuwa viongozi bora, waadilifu na wachangiaji wakubwa katika jamii.
Watoto ni taa ya kesho, ni zawadi ambayo hatupaswi kuichukulia kawaida. Tukiwalea vizuri leo, tumejihakikishia taifa imara kesho. Tuwaenzi, tuwalinde na kuwatunza watoto kwa moyo mmoja.
Kwa kufanya hivyo, mzazi utakuwa umetimiza wajibu wako sambamba na walezi, walimu na raia wema wa taifa. Watoto ni tunu, tuwaheshimu, tuwapende na tuwalee vyema.