Watu wawili wafariki ajali ya basi na lori Shinyanga

Shinyanga. Madereva wawili wa Fuso na basi aina ya Tata wamepoteza maisha katika ajali iliyotokea barabara kuu ya Tinde–Isaka, eneo la Tarafa ya Itwangi, Kijiji cha Nyashimbi.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo akisema chanzo ni uzembe wa dereva wa basi.

 Amesema ajali hiyo ilitokea Septemba 6, 2025 majira ya saa 12 jioni, ikihusisha Fuso lililokuwa likiendeshwa na Rashid Manyawaza kutoka Shinyanga kwenda Kahama na basi la Tata lililoendeshwa na Samsom Sospeter kutoka Kahama kwenda Bariadi.

“Ajali hiyo ilisababisha vifo vya madereva wote wawili na kujeruhi watu wanne, watu watatu tayari wameruhusiwa kutoka hospitali na mmoja anaendelea na matibabu katika Zahanati ya Itwangi,” amesema Magomi.

Baadhi ya mashuhuda akiwamo, Elisha John wamesema waliona watu wengi wamekusanyika barabarani na walipohoji walielezwa kuwa ajali imetokea. “Niliposogea eneo la tukio niliona gari limebinuka na hali ya watu waliokuwa ndani siyo nzuri,” amesema John.