Wiki mbili tu, hati ya uwanja mpya Yanga freshi

YANGA imehakikishiwa kuwa, ndani ya wiki mbili tu itakabidhiwa rasmi hati ya ongezeko la eneo la ujenzi wa uwanja unaotarajiwa kujengwa makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Jangwani.

Eneo hilo awali ndiko ulikokuwa Uwanja wa Kaunda ulioifanya Yanga kuwa klabu ya kwanza kumiliki uwanja kabla ya mambo kuwatibukia na kuhaha kuurejesha, ila kikwazo ilikuwa eneo hilo kuwa dogo na kuchakarika kuiomba serikali iwaongezewe na kufanikiwa hivi karibuni na kufikia ukubwa wa mita za mraba 37,500. 

Akizungumza mbashara kwa njia ya simu katika mkutano Waziri wa Ardhi, Deo Ndejembi amesema wanatambua maombi ya klabu hiyo kwenye ongezeko la eneo hilo.

Ndejembi amewatangazia wanachama wa Yanga kuwa ndani ya wiki mbili hati hiyo itakuwa imekamilika na itakabidhiwa kwa uongozi wa klabu hiyo.

“Nilipata heshima ya kukaribishwa kama Mwananchi mwenzenu, lakini kwa majukumu nimeshindwa kufika,” amesema Ndejembi na kuongeza;

“Kwanza niupongeze uongozi wa Yanga chini ya Rais Hersi, umekuwa mahiri sana kufuatilia mahitaji ya klabu. Kuna hati ambayo tulikuwa tunaishughulikia kwa karibu iweze kutoka niwaahidi ndani ya wiki mbili hizi tutakuwa tumeshaikamilisha na itatoka.”

Aidha, Hersi amemshukuru Ndejembi kwa kufanikisha hilo huku pia akiomba salamu zao njema zifikishwe kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha maombi yao.