Yanga yapeleka jambo lao ushuani

YANGA inaendelea kupiga hesabu za kuanza kwa gia ipi msimu mpya wa mashindano, lakini kuna kitu mabosi wamekifanya kutimiza malengo kwa kuwaita wanachama wa klabu hiyo eneo la ushuani lililopo Masaki, Dar es Salaam ili kujadili kwa kina mikakati yao

Pale, Jangwani bado mashabiki wanatembea na kumbukumbu ya kubeba makombe yote msimu ulio-pita hapa nchini, lakini hiyo siyo ishu sana kwao, kwani leo kuanzia saa 2:00 asubuhi, wameitana ili kuyajenga waanze vipi mashindano ya msimu huu pamoja na mikakati mingine ya kuijenga klabu yao.

Mabosi hao wa Yanga wamewaita wanachama katika Mkutano Mkuu wa kawaida ambao awali uli-pangwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) uliopo eneo la Posta, Dar es Salaam, lakini ghafla wameuhamishia katika Ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki. Eneo hilo la Masaki linatajwa ni miongoni mwa maeneo ya watu wenye nazo na lenye utulivu.

Mkutano mkuu huo umeitishwa kwa mujibu wa Ibara ya 20 ya katiba ya klabu hiyo ya 2021, huku ukiwa na ajenda 10 ikiwamo ishu ya bajeti ambayo ndio inayosubiriwa kwa hamu na wadau kutaka kuona kama itaizidi ile ya mwaka jana na Yanga ilibeba mataji matano kwa mpigo.

Ajenda 10 za mkutano huo ambao awali ulitangazwa na rais wa klabu hiyo, Hersi Said mapema Agosti 8, mwaka huu, ni pamoja na ile ya ufunguzi, uhakiki wa wajumbe, kuthibitisha ajenda na kumbukumbu za mkutano uliopita.

Nyingine ni yatokanayo na kumbukumbu za mkutano uliopita, hotuba ya rais, kupokea na kujadili taa-rifa za kazi kutoka Kamati ya Utendaji, kuthibitisha hesabu za fedha zilizokaguliwa za mwaka uliotangu-lia pamoja na kusomewa mapato na matumizi ya klabu, kuthibitisha bajeti kwa mwaka unaofuata na kufunga mkutano.

Ajenda ya bajeti huenda ndiyo inayosubiriwa kwa hamu ili kuona kama itavuka ya msimu uliopita iliyo-pitishwa na mkutano uliofanyika Juni 9, mwaka jana, ambayo ilikuwa ya Sh24.5 bilioni.

Katika mkutano wa mwaka jana, Mkurugenzi wa Fedha, Sabri Sadick alinukuliwa akisema ongezeko hilo ni kubwa zaidi tofauti na msimu wa 2023-2024 ilipopitisha bajeti ya Sh20.8 bilioni katika mkutano wa Juni 24, 2023. Hata hivyo, licha ya ongezeko hilo, Yanga ilipata pia hasara ya Sh1 bilioni, kwani mapato yalikuwa Sh21 bilioni tofauti na matumizi yaliyokuwa Sh22 bilioni, japo mashabiki waliendelea kufurahia baada ya kutwaa mataji yote ya ndani ya nchi.

Msimu uliopita Yanga ilitetea mataji matatu ya Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu pia Kombe la Muungano na lile la Toyota kule Afrika Kusini, lakini ikacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa pili mfululizo.

Msimu huu timu hiyo imeshatwaa taji moja Rwanda baada ya kuifunga Rayon Sports kwa mabao 3-1 katika mechi  ya kimataifa ya kirafiki iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amahoro Rwanda ilikokuwa imealikwa.

Kwa sasa timu hiyo inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Septemba 16 dhidi ya Simba pamoja na mechi za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola kabla ya kuanza kutetea taji katika Ligi Kuu Bara, Septemba 24, mbele ya Pamba Jiji.