27 wajitosa mbio za magari za Afrika

MADEREVA 27 wa Tanzania walikuwa wamejiorodhesha kushiriki raundi ya tano ya ubingwa wa mbio za magari barani Afrika hadi kufikia mwishoni mwa juma kabla ya mbio hizo kutimua vumbi katikati ya mwezi huu mkoani Morogoro.

Mbio hizo zinajulikana kama Mkwawa Rally of Tanzania na zitafanyikia kwenye hifadhi ya msitu wa Mkundi mkoani Morogoro kati ya Septemba 17-19, kwa mujibu wa mwenyekiti wa Kamisheni ya Mbio za Magari nchini, Satinder Birdi.

Idadi hii kubwa ya washiriki imekuja baada ya msukumo wa wadau wa mbio hizo wakiongozwa na dereva mkongwe Maisam Fazal, ambaye ametia hamasa kubwa ya kuwapo tena mbio za magari za Afrika nchini Tanzania baada ya nchi yetu kushindwa kuandaa mashindanio ya mwaka jana.

“Tumejitokeza kwa wingi kwa sababu tunataka pia kuwasindikiza na kuwashuhudia Watanzania wenzetu, Yassin Nasser na Prince Charles Nyerere  wakivalishwa mataji ya ubingwa wa Afrika  nchini kwao,” alisema msoma ramani David Matete ambaye ataingia katika mashindano haya na dereva Charles Bicco kutoka timu ya Amapiano.

Wa kwanza kuorodhesha jina lake alikuwa ni Waleed Nahdi wa Morogoro na dakika chache baadaye kufuatiwa na Mohamed Tufail Amin wa Dar es Salaam.

Dereva kutoka Dar es Salaam pia wapo Shehazad Munge ambaye alijiorodhesha wa tatu na kufuatiwa na nduguye Altaf Munge kabla ya Nadeem Zakaria na Arsh Somji kuingiza majina yao saa chache  baadaye.

Wengine ambao tayari wamejiandikisha, kwa mujibu wa orodha ya mtandao wa Rally TZ, ni Merey Talib, Samir Shanto, Ahmed Huwel, Ahmed Vigwaza, Tharia, Harinder Deere, Randeep Singh, Manveer Birdi Gurpal Sandhu  na Charles Bicco.

Pia katika orodha hiyo  wapo Dharam Pandya, Kelvin Taylor, Kartic, Zubeiry Piredina na Hamid Mbatta kutoka Iringa.

Pamoja na madereva hawa wa Kitanzania, wapo pia madereva wanaoshiriki kuwania mataji ya ubingwa wa Afrika, Watanzania Yassin Nasser na Prince Nyerere, wakati kutoka Kenya ni Karan Patel, Samman Vohra na Sultan Chana, huku dereva wa pekee kutoka Burundi ni Rohsnali Momo.

Mtanzania Yassin Nasser anaongoza mbio za magari ubingwa wa  Afrika akiwa mbele ya mpinzani wake wa karibu, Samman Vohra kutoka Kenya kwa pointi 8.