ADC yaahidi kuondoa kodi zana za uvuvi, kilimo

Mwanza. Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema kikipewa ridhaa ya kuongoza nchi kitaondoa kodi na ushuru kwenye zana za uvuvi na pembejeo za kilimo, hatua inayolenga kurahisisha uzalishaji na kuongeza kipato cha wavuvi pamoja na wakulima wadogo.

Akinadi sera za chama hicho leo, Jumatatu, Septemba 8, 2029, kwa wakazi wa Buchosa, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya ADC, Wilson Mulumbe, amesema kodi zilizowekwa na Serikali kwenye zana za uvuvi zimekuwa mzigo mkubwa kwa wavuvi wadogo na kuongeza gharama kwa mlaji wa mwisho wa samaki.

Amesema chama chake kikiingia madarakani kitaondoa kodi zote zinazohusu sekta hiyo, kumsaidia mvuvi mdogo kupata zana kwa bei nafuu na kuongeza uzalishaji.

Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shabani Itutu akizungumza na wakazi wa Buchosa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wakati akiwaombea kura wagombea urais na ubunge wa chama hicho. Picha na Saada Amir



Mulumbe amesema mpango huo pia utapunguza gharama za maisha kwa wananchi, kwani samaki na mazao mengine ya uvuvi yatauzwa kwa bei nafuu sokoni.

“Wavuvi wetu wengi ni wadogo, lakini kodi nyingi zimewekwa kwenye zana zao za uvuvi, jambo linalosababisha maumivu makubwa kwa wananchi, hasa mlaji wa mwisho wa samaki,” amesema.

Ameongeza kuwa ADC itatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wavuvi wadogo, ili kubadilisha maisha yao, kwani wengi bado wanaishi katika umaskini licha ya sekta hiyo kuwa na fursa kubwa ya kiuchumi.

Aidha, amesema chama chake kitalenga sekta ya kilimo kwa kuondoa ushuru kwenye zana zote za kilimo na kuhakikisha pembejeo muhimu zinapatikana bure kwa wakulima.

“Zana zote za kilimo zitakuwa hazina ushuru, na pembejeo zote za kilimo zitakuwa bure,” ameeleza Mulumbe.

Amesema hatua hiyo inalenga kumwezesha mkulima kuzalisha zaidi na kuongeza tija katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara.

Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shabani Itutu, amesema chama chake kimeweka kipaumbele cha kujenga mifumo ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali ya kilimo, ili wakulima wavune mara kwa mara bila kutegemea mvua.

Amesema wakulima wa Tanzania wamekuwa wakilima kwa mazoea na kutegemea mvua, jambo linalosababisha kutopata faida ya uhakika.

Itutu amesema ADC ikipewa ridhaa ya kuongoza nchi itahakikisha kila kijiji kinapatiwa trekta la Serikali litakalotumika kwa kilimo cha pamoja, huku wakulima wakibeba jukumu la kuchangia mafuta pekee.

Amesema lengo ni kuwaondoa wananchi kwenye kilimo cha mikono na kuwapeleka kwenye kilimo cha kisasa chenye tija.

Baadhi ya wakazi wa Buchosa wakisikiliza sera za Chama cha ADC wakati kikinadi wagombea wake. Picha na Saada Amir



Pamoja na hilo, amesema chama chake kitaunganisha wavuvi wote wanaojihusisha na uvuvi kwa njia ya vizimba, ili kunufaika zaidi kupitia vikundi na mashirikiano ya karibu.

Ameeleza pia ADC itahakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa, ili kupunguza vifo vinavyotokana na ukosefu wa huduma hizo.

Mgombea mwenza wa urais kupitia ADC, Shoka Khamis Juma, amesema chama hicho kikiwa madarakani kitaleta maendeleo kwa wananchi wote kwa kuhakikisha kila mmoja anafaidika na rasilimali za nchi bila upendeleo.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Buchosa kwa tiketi ya ADC, Komanya Atanas, amesema akipata ridhaa ya wananchi atahakikisha barabara ya Sengerema-Nyehunge inajengwa kwa kiwango cha lami.

Amesema barabara hiyo imekuwa ikiahidiwa kwa muda mrefu na marais wanne kwa nyakati tofauti, akiwemo hayati Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na hayatio Dk John Magufuli, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji wa dhati uliofanyika.