Mpango wa Tanzania wa kuhakikisha upatikanaji wa urahisi na unafuu wa nishati safi ya kupikia unategemea ushirikiano wa Serikali na wadau wa sekta binafsi.
Katika toleo la leo mwandishi wetu Halili Letea amefanya mahojiano na Fredrick Tunutu, Meneja wa Mradi wa Tanzania Clean Cooking Project (TCCP) katika shirika lisilo la kiserikali la Africa Enterprise Challenge Fund (AECF) ili kuelewa ushiriki wake unavyosaidia utekelezaji wa mpango huu wa Taifa.
AECF imepokea ufadhili wa Dola 3.75 milioni za Marekani (Sh9.75 bilioni) kutoka Swedish International Development Cooperation Agency (Sida) kusaidia kuendeleza sekta ya nishati safi ya kupikia nchini.
Hapa Tunutu anafafanua zaidi ushiriki wa shirika hilo.
Swali: Shirika lenu linafanyaje kusapoti kwenye utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia?
Tunutu: Programu yetu imeunganishwa kwa karibu na Mpango wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) unaolenga kufikia asilimia 80 ya kaya nchini kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
AECF inachangia kwa njia tatu kuu; kwanza, kwa kuchochea ushiriki wa sekta binafsi na kusaidia kampuni zinazotoa suluhisho kwenye sekta ya nishati safi katika masoko yenye upungufu.
Pili, kwa kuongeza upatikanaji kupitia msaada wa kifedha na kiufundi unaowawezesha wajasiriamali kuibua ubunifu na kupanua shughuli zao na tatu, kwa kuimarisha uratibu wa sekta na kutetea sera na kanuni zinazounda mazingira rafiki kwa biashara.
Swali: Ni hatua zipi mnazochukua kusaidia kufikia lengo la asilimia 80 ya kaya kutumia nishati safi ifikapo 2034?
Tunutu: Hadi sasa, AECF tumetoa Dola 2.18 milioni (Sh5.67 bilioni) kwa kampuni tisa, na kampuni nyingine bado zinaendelea kujiunga. Kampuni hizi tayari zimefikia zaidi ya wanufaika 125,000, zimejenga majiko banifu na imara katika shule na magereza 210, kuzalisha ajira 225, na kusaidia kampuni nyingine ndogo na changa (SME) 774.
Zaidi ya hayo, mradi huu umechochea Dola 1.5 milioni (Sh3.8 bilioni) katika uwekezaji wa sekta binafsi. Kwa kuunga mkono teknolojia kama LPG, majiko yaliyoboreshwa na banifu, na mkaa mbadala, AECF inahakikisha kuna suluhisho mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya kaya na taasisi.
Swali: Ni miradi gani mnaendesha sasa unaohusu majiko banifu, LPG, biogas, eCooking au mkakati wowote wenye kusapoti hili?
Tunutu: Mradi wetu mkuu ni Tanzania Clean Cooking Project (TCCP), mradi wa miaka minne kuanzia 2022 hadi 2026. Unalenga kupanua upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia, kuchochea ushiriki wa sekta binafs, na kuimarisha soko.
Kwa sasa, tunashirikiana na kampuni tisa zinazotoa teknolojia mbalimbali, ikiwamo majiko yaliyoboreshwa, mkaa mbadala, na suluhisho za LPG.
Vilevile, dirisha la ufadhili bado liko wazi, jambo linalotupa nafasi ya kutambua na kusaidia wajasiriamali zaidi ili kufikia lengo la kuunda kanzidata yenye athari kubwa.
Swali: Mnasaidiaje kaya maskini na vijijini kumudu gharama na upatikanaji za nishati safi? Ikiwa hili ndio tatizo kubwa zaidi kwa wengi.
Tunutu: Upatikanaji na nishati zenye ufanisi na gharama nafuu ni kiini cha mkakati wetu.
Moja ya vigezo vyetu vya ufadhili ni kuhakikisha kampuni zinazingatia maeneo ya vijijini na maeneo yanayoanza kukua, mahitaji ni makubwa.
Tunaunga mkono teknolojia mbalimbali, ikiwamo majiko yaliyoboreshwa, LPG, bioethanol, mkaa mbadala, na hata umeme, ili kaya ziweze kuchagua suluhisho linalofaa kipato chao.
Pia, tunasisitiza mfumo wa biashara wa ubunifu kama pay-as-you-go (PAYG), VICOBA-linked financing, na mikopo midogo, ambayo inapunguza gharama za awali na kuwezesha kaya maskini kulipa kwa taratibu, hivyo kuongeza upatikanaji na kutumia suluhisho kwa muda mrefu.
Swali: Mnachangiaje kupunguza pengo la fedha linalohitajika kutekeleza mkakati huu? Tanzania inahitaji Sh4.6 trilioni kutekeleza.
Tunutu: Tunatoa ufadhili wa Dola 50,000 hadi Dola 400,000 (Sh130 milioni hadi Sh1.04 bilioni) kwa kampuni za awali na zinazoendelea. Ufadhili huu unatoa mtaji muhimu wa kufanya kazi na pia kupunguza hatari, jambo linalovutia uwekezaji zaidi, mikopo na ufadhili wa wadau wengine.
Hii inachangia kuongeza mtiririko wa fedha katika sekta ya nishati safi na kusaidia kufanikisha sehemu katika Sh4.6 trilioni zinazohitajika kwa utekelezaji wa mpango wa kitaifa.
Swali: Mnatumia mbinu zipi za ubunifu kama carbon credits au blended finance kufadhili miradi yenu?
Tunutu: Tunatumia mbinu kadhaa za ubunifu. Ufadhili wa kichocheo unawawezesha wajasiriamali kuibua na kuuza bunifu mpya, modeli za biashara na teknolojia zinazopanua upatikanaji wa nishati na kupunguza umasikini.
Baadhi ya kampuni pia zinatumia Results-Based Financing (RBF), ambapo malipo hufanywa baada ya kufikiwa kwa viashiria vya utendaji, kuhakikisha uwajibikaji na athari halisi kabla ya malipo.
Swali: Mnahakikisha vipi au kusaidia utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kutumia nishati safi ya kupikia?
Tunutu: Elimu na uhamasishaji ni sehemu ya mpango. Tunahitaji kampuni zinazopewa msaada kuingiza elimu ya jamii katika mipango yao. Zaidi ya hayo, tunatumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kusambaza ujumbe kuhusu faida za kiafya, kiuchumi na kimazingira.
Pia, tunashiriki katika majukwaa na meza za mazungumzo ili kutoa maarifa na kuhamasisha mabadiliko ya tabia kwa wananchi.
Swali: Mnashirikishaje wanawake na vijana katika miradi ya nishati safi?
Tunutu: Wanawake na vijana wapo katikati ya mpango wetu. Tunapendelea kampuni zinazoongozwa au kumilikiwa na wanawake na tunahimiza uongozi wa vijana ndani ya wajasiriamali. Makundi haya yana nafasi kubwa zaidi kwenye kupata ufadhili.
Angalau asilimia 50 ya ajira zinazoundwa lazima zichukuliwe na wanawake na vijana, kuhakikisha wanakuwa siyo tu wanufaika bali pia wakiwezesha kuendesha sekta.
Swali: Mnashirikiana vipi na Serikali au taasisi kama Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) katika kuendeleza nishati safi ya kupikia?
Tunutu: AECF inashirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania na mashirika kama Wakala wa Nishati Vijijini.
Shirika hili ni miongoni mwa walioshiriki katika uundaji wa Mpango wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia, linaendana na programu za Serikali na linashiriki katika majukwaa, meza za mazungumzo na vikundi vya kiufundi kuhakikisha sauti ya sekta binafsi inawakilishwa ipasavyo.
Swali: Ni changamoto gani mnazokabiliana nazo na mnawezaje kuzitatua?
Tunutu: Changamoto ni nyingi. Kampuni nyingi hazina rekodi sahihi za biashara ya nyuma au mifumo imara, jambo linalofanya uchambuzi wa kina kuwa mgumu kabla ya kuwapatia ufadhili. Sekta bado ni ndogo na idadi ya wajasiriamali wanaokidhi vigezo vya uwekezaji ni chache.
Baadhi ya kampuni zinategemea ufadhili kuanza badala ya kujenga mifumo mizuri na endelevu kwa kampuni zao.
Pia, upatikanaji wa matching funds (fedha inayolingana na fedha ya ufadhili) ni changamoto, pamoja na upungufu katika utawala, uwezo wa kiufundi na mifumo ya usambazaji.
Tunatatua hili kwa kutoa msaada wa kiufundi, udhibiti wa fedha na ushauri wa karibu, pamoja na kutetea mazingira bora ya uwekezaji.
Swali: Fursa zipi sekta binafsi zinaweza kutumia kuharakisha upatikanaji wa nishati safi Tanzania?
Tunutu: Sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kuongeza wigo wa suluhisho safi. Kuna fursa kubwa katika vijijini na miji inayokua, mahitaji ni makubwa. Kampuni zinaweza kutumia mitandao ya usambazaji, wakala na majukwaa ya kidigitali.
Sera za Serikali, ikiwamo kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT), ruzuku na vizuizi kwa kampuni hizi pia inaweza kuwa msaada.
Zaidi, miradi ya wafadhili, ikiwa ni pamoja na TCCP, inatoa ufadhili, msaada wa kiufundi na ushirikiano.
Fursa hizi zinaunda msingi imara kwa sekta binafsi kukuza na kuongeza upatikanaji wa suluhisho la nishati safi wa Watanzania.