Dar es Salaam. Ule usemi wa siku za mwizi ni 40 umetimia kwa Masero Ryoba Muhabe (44), anayedaiwa kuwa kinara wa biashara ya bangi mkoani Mara baada ya kukamatwa akiwa na tani 6.5 za bangi.
Mfanyabiashara huyo anadaiwa kutumika kama daraja kati ya wafanyabiashara kutoka nchi jirani wanaofadhili kilimo cha bangi na wakulima wanaolima zao hilo.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), Muhabe amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, hatimaye alikamatwa akiwa na mzigo huo wa bangi alioufangasha tayari kwa kuusafirisha.
Kamishna Jenerali wa DCEA amesema, mbali na kujihusisha na kilimo na usafirishaji wa zao hilo haramu, mtuhumiwa huyu amekuwa akiwahamasisha wakulima wengine wajikite kwenye kilimo cha bangi.
“Yani huyu amekuwa akitumika kupokea fedha kutoka kwa wafanyabiashara wanaofadhili kilimo cha bangi, na kutumia fedha hizo kuhamasisha wakulima wengine wajikite kwenye kulima bangi,” amesema na kuongeza:
“Tunapofanya operesheni za kuteketeza mashamba ya bangi, yeye alikuwa akipita kuwasisitiza wasiache kulima zao hilo. Alijitapa kwamba hawezi kukamatwa na hakuna anayeweza kuwazuia.”
Mbali na kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, operesheni iliyofanyika katika kipindi cha miezi miwili kuanzia Julai hadi Septemba, imekamatwa watu wengine 939 wakihusishwa na dawa za kulevya kilogramu 33,077, ekari 64 za bangi na kilogramu 4,553 za mbegu za bangi.
Kati ya hao, wapo wahandisi wawili waliokamatwa mkoani Mbeya wakijihusisha na biashara ya biskuti za bangi walizokuwa wakiziuza kwa wahandisi wenzao, wanafunzi na vijana wa mtaani.
Watuhumiwa hao, Henry Shao (36) na Veronika Samumba (31), walikamatwa wakiwa na biskuti 241 zilizotengenezwa kwa bangi, na walipohojiwa kisha kupekuliwa walibainika kuwa na vifaa vya kutengeneza biskuti hizo.
“Hebu fikiria hawa wawili ni wahandisi ujenzi, wanafanya kazi zao lakini wanaharibu vijana wengine. Tulipowahoji walisema wateja wao wakubwa ni wanafunzi wa vyuo, wahandisi wenzao na vijana wa mtaani. Tuwe makini na watu wa aina hii wanaharibu watoto wenzao, nina uhakika hawawezi kuwapa hizo biskuti watoto wao,” amesema.
Katika hatua nyingine, DCEA imezionya kampuni zinazomiliki magari yenye uwezo wa kusafirisha mizigo kuhakikisha wanawakabidhi magari hayo madereva waaminifu.
Angalizo hilo limekuja kufuatia kukamatwa kwa gari aina ya Scania lenye nembo za kampuni ya vinywaji baridi, likikamatwa likiwa na kilo 452 za bangi.
Operesheni hizo zilizofanyika kwenye bar eneo la Mtoni kwa Azizi Ally na Masaki zimewezesha kukamatwa sigara za kielektroniki (e-sigaret) 50 zilizotengenezwa kwa bangi zenye ujazo wa mililita 10 kila moja.
Sigara hizo za kielektroniki zilizotengenezwa kwa kutumia kemikali pamoja na skanka, ziliingizwa nchini kutoka Uingereza.
Njia ya haja kubwa yatumika kusafirisha cocaine
Katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam, mtaa wa Tupendane-Manzese, wilayani Ubungo, wamekamatwa watu watatu, akiwemo raia wa Lebanon, wakiwa na kilo 2.443 za dawa za kulevya aina ya cocaine zinazodaiwa kutoka nchini Brazil.
“Ukitaka kujua hawa watu walivyowasafirisha hizi dawa hatari, walitumia njia ya haja kubwa. Hawakujali ukubwa wa hizo pipi waliziingiza kwenye njia ya haja kubwa bila kujali athari za kiafya.
“Baada ya kuwahoji, wameeleza kuwa kuziweka dawa hizo kwenye njia ya haja kubwa kunarahisisha kuzitoa haraka kuliko njia ya kuzimeza tumboni,” amesema.