Kwa vile nilikuwa na ahadi na mtu, usingizi uliniruka. Nilikwenda kukaa sebuleni hadi saa tano na nusu nikiangalia televisheni. Baada ya hapo nilizima televisheni, nikaenda kupenua pazia la dirisha na kuchungulia nje.
Nilikuwa nimezima taa, hivyo mtu wa nje asingeniona, isipokuwa mimi ndiye ningeweza kumuona.
Nilisimama hapo dirishani kwa dakika nyingi nikiangalia nje. Nilikuwa ninataka nimuone Shefa atakapowasili. Si kwamba nilikuwa namsubiri kwa hamu, bali ulikuwa ni wasiwasi wangu tu.
Ilipofika saa sita kasoro dakika kumi nikaona gari likisimama nyumba ya tatu kutoka ile nyumba yetu, lakini ilisimama kwenye nyumba iliyokuwa upande wa pili wa barabara, sio ule uliokuwa na nyumba yetu.
Baadaye alishuka mtu, nikamuona akimfuata mlinzi wa nyumba aliyokuwa ameegesha gari na kuzungumza naye, kisha akatembea kuelekea upande uliokuwa na nyumba yetu. Mpaka alipofika karibu kabisa ndipo nilipotambua kuwa ni Shefa. Alikuwa amefika na gari lake.
Kwa vile hakutaka atambulike, aliamua kuliegesha mbali na nyumba yetu ili hata kama mtu ataliona na kulitambua, hataweza kujua kama Shefa alikuja nyumbani kwangu.
Ilikuwa ni akili nzuri ya kuwazuga wambea wa mambo ya watu.
Kwa vile sikutaka Shefa abishe mlango kama mgeni, mlango huo niliuegesha tangu mapema ili akiusukuma aingie ndani kama mwenyeji. Nikaondoka pale kwenye dirisha na kwenda kukaa.
Mara nikaona mlango unasukumwa, nikasema:
“Karibu.”
Shefa akaingia ndani haraka haraka na kisha akaufunga mlango. Lilikuwa jambo la hatari lakini lilikuwa katika mazingira yaliyo salama.
“Karibu ukae,” nikamwambia Shefa huku nikimuona aibu vile alivyokuwa shemeji yangu.
“Asante.”
Shefa akaja kukaa karibu yangu. Mara moja nikagundua kuwa alikuwa amelewa. Hakuwa sawa. Nilijua alilewa kusudi kuondoa aibu. Nilikuwa shemeji yake, kwa vyovyote vile angeniona aibu.
Mimi nisiye na aibu ndiyo nilikuwa macho makavu!
“Vipi?” ndiyo neno lililomtoka mdomoni.
“Poa tu,” nikamjibu, kisha nikamuuliza:
“Unatoka baa?”
“Nilikwenda kusubiri muda uliuoniambia.”
“Kwani utalala hapa, si utaondoka baadaye?”
“Nitaondoka kwenye alfajiri.”
“Utarudi kwako alfajiri?”
“Haina shida.”
“Mkeo utamwambia nini?”
“Si unajua sisi watu wa magari hatuna muda maalumu wa kurudi nyumbani. Anajua niko kwenye kazi.”
“Karibu chumbani,” nikamwambia.
Tukainuka na kuingia chumbani. Nilitangulia mimi kisha akaingia Shefa. Unaona kosa langu la kumuingiza mwanamume chumbani mwa mume wangu. Je, kama angetokea usiku ule ingekuwaje? Lakini yote hayo sikuyawaza. Ibilisi alikuwa ameshanisimamia.
“Karibu ukae kitandani,” nikamwambia Shefa, ambaye alikuja kitandani na kukaa pamoja nami.
Hapo hapo simu yangu ikaita. Nilipoishika na kuitazama niliona namba ya Sufiani. Moyo wangu ukashituka kidogo. Kuna nini? Kwanini amenipigia usiku ule? Nikajiuliza.
Sufiani hakuwa na tabia ya kupiga simu usiku mwingi. Nilitaka nisipokee ile simu ili Shefa asisikie mazungumzo yetu, lakini wasiwasi ulishanipata. Sufiani alikuwa na habari gani ya kunieleza? Nikamtazama Shefa.
“Naongea na mume wangu,” nikamwambia, kisha nikapokea ile simu.
“Hello…!”
“Ulikuwa umelala?” Sufiani akaniuliza kwenye simu.
“Umeniamsha,” nikajidai kumwambia, kisha nikamuuliza:
“Mbona umenipigia usiku?”
“Nilikuwa nataka kukufahamisha kuwa nimepata safari ya Zambia. Naondoka alfajiri hii.”
“Kurudi?”
“Kama sitakuta foleni ndefu mpakani, nitawahi kurudi.”
“Sawa. Safari njema.”
Mume wangu akakata simu.
“Anasemaje?” Shefa akaniuliza.
“Anakwenda Zambia asubuhi.”
“Atarudi lini?”
“Hakuniambia siku ya kurudi.”
Nawakatishia hapa. Sitaki niwaeleze kilichotokea baada ya hapo. Nataka mjue tu kuwa siku ile niliivunja amri ya sita. Nikalala na Shefa hadi saa kumi nilipomuamsha aende zake.
Shefa akatoka kwenda msalani. Nyumba tuliyokuwa tukiishi licha ya kuwa ni ya ghorofa, ilikuwa ni mijengo ya kizamani. Unapotaka kwenda msalani inabidi utoke ukumbini ambako ndiko kulikokuwa na vyoo na ndiko kulikokuwa na mlango wa kuingilia.
Shefa alipotoka kwenda msalani nilibaki kitandani kumsubiri arudi ili tuagane aende zake. Alichokuwa anakitaka alikuwa ameshakipata. Nilitaka kujua baada ya tendo hilo angenipa nini.
Nikamsubiri mpaka nikapitiwa na usingizi. Baadaye nikazinduka lakini Shefa hakuwepo. Nikadhani labda alikuwa hajarudi kutoka msalani, lakini nilipotazama saa iliyokuwa kwenye simu yangu niliona ilikuwa imepita zaidi ya nusu saa tangu alipokwenda msalani. Isingewezekana akae msalani kwa muda wote huo!
Nikajiambia labda alirudi akanikuta nimelala, akaamua kuondoka. Nilipowaza hivyo nilishuka kitandani, nikaenda kwenye dirisha na kuichungulia gari yake. Gari ilikuwepo. Nikajua Shefa alikuwa hajaondoka.
Sasa yuko wapi muda wote huu?
Nikatoka ukumbini kumuangalia. Nilikwenda upande uliokuwa na vyoo. Mahali hapo palikuwa na kiza. Kama kungekuwa na mtu, taa ingekuwa inawaka. Nikapata wasiwasi.
Niliwasha taa, kisha nikainua hatua ili nifungue mlango wa msalani.
Mama yangu! Kama ningeuteremsha mguu bila kuangalia chini ningekanyaga mwili wa mtu aliyekuwa amelala chini kando ya mlango wa kuingilia msalani.
Alikuwa amelala kifudifudi. Damu iliyokuwa imemtoka mdomoni na puani ilienea katika eneo alilolala.
Nikashituka. Ni nani?
Macho yangu yakanithibitishia alikuwa Shefa. Huku moyo ukinienda mbio, nilimuita:
“Shefa! Shefa!”
Shefa alikuwa kimya kama aliyekuwa amelala usingizi mzito. Nikainama na kumshika. Japokuwa sikuwa na uzoefu wa kugundua watu waliokufa, lakini Shefa alikuwa ameshakufa! Mwili wake ulikwisha kuwa baridi.
Mbali ya mwili wa Shefa kuwa baridi, macho yake yalikuwa wazi lakini yalionesha hayakuwa yakiona chochote.
Karibu yake palikuwa na rungu mfano wa yale marungu wanayobeba askari wa makampuni ya ulinzi.
Lilikuwa limeganda nywele pamoja na damu. Nikajua kuwa Shefa alikuwa ameshambuliwa, na alishambuliwa kwa rungu nililoliona hapo. Aliyemshambulia aliamua kuliacha rungu lake hapo hapo.
Miguu yangu ilitetemeka mpaka nilikaribia kuanguka kwa uoga ulionipata. Nilitaka kupiga kelele lakini nilishindwa. Ningepiga kelele, maana yake ningeita watu. Hivyo nilikuwa ninaita watu waje wanifumanie na mume wa watu, wakati mwenyewe pia nilikuwa mke wa mtu.
Sikupiga tena kelele, lakini nilijishika kichwa huku moyo wangu ukipiga kwa vishindo kama vile ulitaka kutoka kifuani mwangu.
“Mama yangu wee! Nini kimetokea jamani?” nilijisemea peke yangu kwa sauti ya kusikika, tena sauti ya mtu anayetaka kulia kwa hofu.
Nikahisi kwamba kulikuwa na mtu aliyeingia humo ndani na kumshambulia Shefa. Kama ilikuwa ni hivyo, nilijiuliza, huyo mtu aliingia kwa wapi wakati mlango wa mbele tuliufunga kwa ndani?
Nikaondoka hapo na kwenda kando ya mlango huo. Niliona mlango ulikuwa bado umefungwa kwa ndani, hali iliyoonesha kuwa hakukuwa na mtu yeyote aliyeingia.
Lakini nilipotazama katika dirisha lililokuwa pembeni mwa mlango, nikaliona liko wazi. Dirisha lenyewe lilikuwa la shata za vioo. Halikuwa na nondo. Linapokuwa wazi linakuwa na nafasi ya kupenyeza mtu.
Nilikumbuka kwamba dirisha hilo nililifunga. Kwa hiyo kulikuwa na mtu aliyelifungua. Nikagundua kuwa aliyemshambulia Shefa alijipenyeza hapo.
Lakini nikajiuliza aliwezaje kukifungua kipete kinachofungia dirisha hilo ambacho kipo kwa ndani? Baada ya kufikiri sana nikahisi huenda nilisahau kukifunga kipete hicho. Kwa hiyo mtu aliyeingia alilisukuma dirisha likafunguka na hivyo akajipenyeza ndani.
Ilikuwa wazi, baada ya kujipenyeza na kumshambulia Shefa kwa rungu, alitokea na hapo hapo. Nikathubutu kuchungulia nje kupitia dirisha hilo.
Nje kulikuwa kimya na sikuweza kuona mtu yeyote. Nikalifunga lile dirisha na kurudi ulipokuwa umelala mwili wa Shefa.
Maswali yalikuwa yakiendelea kupita ndani ya akili yangu. Nilijiuliza: ni nani ambaye alifanya ushenzi ule? Wa kwanza kumshuku ni mtu aliyeingia kwa nia ya kuiba. Alipomuona Shefa akitokea msalani, akamshambulia kwa rungu.
Wazo hilo lilinifanya nirudi chumbani na kuchunguza kama kuna wizi uliotokea. Baada ya kukagua chumba, niliona kila kitu kilikuwepo na hakukuwa na dalili yoyote iliyoonesha kulikuwa na mtu aliyeingia humo chumbani.
Sasa kama kulikuja mwizi, aliishia ukumbini, hakuingia humu chumbani? Nikajiuliza. Hapo nikaona aliyemshambulia Shefa hakuwa mwizi.
Mtu wa pili kumshuku alikuwa mume wangu. Labda alirudi na kumkuta Shefa, likawa ni fumanizi, na ndipo alipompiga rungu.
Lakini kama ni mume wangu, asingepita kwa dirishani. Angeingia kwa mlangoni na ugomvi wao ningeusikia.
Pia kama ni mume wangu, angelipata wapi lile rungu wakati hatukuwa na rungu kama lile pale nyumbani?