Mambo mengi yanajenga kumbukumbu kuhusu Mei 18, 1966. Chombo cha anga cha Surveyor 1, kilichobuniwa na kuundwa na Shirika la Sayansi ya Anga la Marekani (Nasa), kilitua kwa mara ya kwanza mwezini kwa majaribio. Kwa Canada, ni kumbukumbu mbaya kwani magaidi walilipua jengo kuu la Bunge la nchi hiyo kwa mabomu yaliyotegwa.
Kinyota, Mei 18 kwa nchi za Magharibi, waliozaliwa tarehe hiyo huitwa Taurus (nyota ya Ng’ombe). Wenye kufuata mpangilio wa nyota za China, waliozaliwa Mei 18 ni Horse (nyota ya Farasi). Mei 18, 1966 ilikuwa Jumatano, na siku hiyo, eneo la Makadara, Zanzibar, alizaliwa mtoto ambaye kwa miongo mitatu amekuwa sehemu ya siasa za mageuzi Tanzania.
Ni mtoto kutoka ukoo wa Ambar, ambao ni mashuhuri wa kibiashara Pemba na Zanzibar yote. Jina la mtoto tajwa kutoka ukoo huo wa Ambar ni Ambar Khamis Haji, ambaye ndiye Mwenyekiti wa chama cha National Convention for Construction and Reforms – Mageuzi (NCCR-Mageuzi).
Pamoja na kuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Ambar ndiye aliyeteuliwa na chama chake kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kumpitisha na kumteua rasmi.
Ambar ni mwanachama wa NCCR-Mageuzi tangu mwaka 1994. Aligombea ubunge Jimbo la Mkoani, Pemba, mwaka 1995 lakini kura hazikutosha.
Tangu hapo, amekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR-Mageuzi mpaka leo. Kati ya mwaka 1999 na 2012, Ambar alikuwa mjumbe wa Baraza la Wadhamini la NCCR-Mageuzi.
Amewahi kuwa Kaimu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa mwaka 2000 hadi 2001. Ni kipindi ambacho Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, alikwenda kugombea ubunge Jimbo la Vunjo, na baada ya uchaguzi kukawa na kesi ya kupinga matokeo ambayo mlalamikaji alikuwa Mbatia. Kwa muda huo ambao Mbatia alikuwa akipigania ubunge, ilibidi Ambar akaimu uenyekiti.
Mbatia ni mmoja wa vijana wasomi waliofukuzwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya 1990 kwa sababu ya kujihusisha na vuguvugu la mageuzi ya kisiasa. Alifukuzwa akiwa mwaka wa mwisho alipokuwa akisoma shahada ya kwanza ya uhandisi.
Mwaka 2006 hadi 2008 mwishoni, Mbatia alikwenda Uholanzi, alikosoma shahada ya kwanza ya Elimu ya Majanga. Kipindi hicho, Mbatia alipokuwa Uholanzi, Ambar alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Septemba 24, 2022, Mkutano Mkuu wa Taifa wa NCCR-Mageuzi ulimchagua Ambar kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
Ambar ni baharia. Mwaka 1991 aliondoka nchini, akapitia Syria na Lebanon wakati akiitafuta Ugiriki ili kutafuta fursa za kimaisha kupitia ubaharia.
Alipofika Ugiriki, alifanya kazi kwenye meli kama baharia kipindi meli zikiwa zimepaki. Nchini Ugiriki, Ambar alifanya kazi za ubaharia kwa mwaka mmoja, yaani kuanzia 1991 hadi 1992.
Baada ya kurejea Tanzania, Ambar alijikita kwenye biashara na kwa kuwa alikuwa na shauku na siasa, alianza kuingia taratibu, na chama kilichomvutia kilikuwa NCCR-Mageuzi, ambacho alichukua rasmi kadi ya uanachama mwaka 1994, kisha akagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu 1995, ambao ulikuwa wa kwanza kushirikisha vyama vingi vya siasa tangu nchi ilipopata uhuru.
Kabla ya kugombea ubunge au hata hajafikia kiwango cha kuwa mfanyabiashara wa kati, Ambar anasema alianzia chini kabisa. Alianza kwa kuuza ndizi za kutengenezea urojo, akakusanya mtaji hadi akafungua duka la nguo eneo la Darajani, Zanzibar, ambalo lilikuwa linaitwa Seti Enterprise. Sifa kubwa ya duka hilo ni kwamba alikuwa akiuza vitambaa kutoka Dubai.
Ambar anakiri kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni mgombea wa kiti hicho kupitia CCM, amefanya mambo mengi makubwa katika kuwahudumia Watanzania.
Pamoja na kukiri huko, anakosoa viongozi walio chini ya Rais Samia kuwa hawafanyi kazi ipasavyo na hawana ushirikiano kama timu. Anaona hiyo ni sababu ya yeye kumpokea kijiti ili akatende mageuzi ya kiuongozi.
Anasema, Rais Samia alitanguliwa na hayati, Dk John Magufuli, aliyetembea na kaulimbiu yake ya “Hapa Kazi Tu, kisha Samia aliposhika madaraka, alitamka “Kazi Iendelee.”
Ambar anaongeza kuwa kwa vipimo vyote, Rais Samia ameendeleza kazi vema, lakini anakwamishwa na wasaidizi wake ambao hawafanyi kazi kwa ushirikiano.
“Sasa hivi Serikali imekuwa sawa na kambare. Mwanamke, mwanaume na mtoto wote wana ndevu. Mkuu wa mkoa anafanya kazi ya mkurugenzi, mkuu wa wilaya anaingilia majukumu ya mkurugenzi.
“Maofisa tawala wa mikoa na wilaya nao wanaingiliana kikazi. Matokeo yake, migongano ni mingi na ufanisi unakosekana. Nataka niwe Rais wa Tanzania ili nishughulikie hayo,” anasema Ambar.
Kingine ambacho Ambar anasema anataka kukishughulikia ni mihimili kuwa huru na ifanye kazi kwa mujibu wa Katiba inavyotaka. Anafafanua kuwa sasa hivi wabunge hawajui nafasi zao, wanaunga mkono kila kitu cha Serikali. Ambar anatoa ahadi kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atahakikisha Bunge linasimama ipasavyo kuisimamia Serikali bila woga.
Chini ya urais wake, Ambar anasema mgawanyo wa nguvu za mihimili ya dola utatekelezwa ipasavyo. Mahakama itakuwa huru bila kuingiliwa na mhimili wowote, hivyo kuifanya nchi isonge mbele ili iwe mfano wa utawala bora na mgawanyo wa madaraka ya kidola.
“Nasisitiza, Rais Samia amefanya kazi nzuri na ana nia njema sana kwa ajili ya nchi yetu. Hata hivyo, kwa hapa alipofikia inatosha, natakiwa niingie mimi.
“Amefanya kazi kubwa, sisi wote ni mashahidi, lakini nataka Watanzania wanielewe na waniunge mkono. Yeye Rais Samia ameweza, hata mimi nishindwe nina nini?” amehoji Ambar.
Kati ya mwaka 1989 na 1991, Ambar alijikita kwenye biashara za kusafiri kati ya Zanzibar na Mombasa. Alikuwa akichukua dawa za meno, siagi, sabuni na bidhaa nyingine Mombasa na kwenda kuuza Zanzibar, wakati huohuo akawa akisafirisha nguo, pafyumu na marashi asilia ya Kizanzibari na kuyauza Mombasa. Biashara hiyo aliiacha mwaka 1991, aliposafiri kwenda Ugiriki katika safari ya kutimiza ndoto yake ya ubaharia.
Maisha ya kibiashara kwa Ambar ni kama upepo na bahari. Baada ya kurejea kutoka Ugiriki, alifanya biashara mbalimbali, lakini kubwa ni mwaka 2007 mpaka 2014, alijikita katika uuzaji wa magari kutoka Uingereza na Dubai. Magari hayo alikuwa akiyauza Dar es Salaam, kituo chake kikiwa Magomeni.
Anasema, mbali na kukaa Ugiriki, lakini kati ya mwaka 2003 na 2004 aliishi Uingereza na kujifunza mengi. Ambar alifunga ndoa tangu mwaka 1992. Ana mke mmoja anayeitwa Saida Ashuru Abeid na watoto wanne, wawili wa kiume na wawili wa kike. Majina yao ni Ismail, Zulfa, Barke na Jamil.
Ambar anasisitiza kuwa anataka urais ili aongoze nchi, na amekuwa na shauku ya muda mrefu ya kuiongoza Tanzania ili awapatie wananchi maendeleo zaidi ya yaliyopo.
Anasema kuwa uzoefu wake wa kisiasa, kozi nyingi za kisiasa na uongozi alizosoma ndani na nje ya nchi, vilevile uzoefu wa kuishi Zanzibar, Tanzania Bara na nje ya nchi, ni mkusanyiko wa mambo yenye kumpa jeuri Ambar kuona anaweza kuipa Tanzania maendeleo makubwa.
Ambar alizaliwa Mei 18, 1966, Mtaa wa Makadara, Wilaya ya Mkoani, Pemba. Kiasili, Ambar ni Mshirazi. Elimu ya msingi alisoma Shule ya Msingi Uweleni, Wilaya ya Mkoani, Pemba.
Kwa taarifa, Uweleni ndiyo shule aliyosoma Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi za Kiafrika (OAU). Ambar anasema kuwa wakati anasoma Uweleni, alipeleleza sehemu aliyokuwa akiishi Dk Salim. Alipoijua, akawa anakaa hapo ili angalau apate hisia za ‘usalim.’
Maisha ya Uweleni kwa Ambar yalikuwa ya miaka saba kamili, kuanzia mwaka 1977 mpaka mwaka 1984. Baada ya hapo hakusoma sekondari, badala yake alijiunga na Chuo cha Ufundi cha Mikunguni kilichopo Amani, Unguja ambako alifundishwa ufundi seremala.
Maisha ya Mikunguni yalidumu miaka mitano, kuanzia mwaka 1984 mpaka 1989. Walimu waliomfundisha walikuwa Wazungu kutoka Denmark. Alifuzu vizuri, lakini hakuwahi kufanyia kazi utaalamu alioupata chuoni.