Mbeya. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimeonya wagombea wake kuacha kutumia lugha za kejeli na dharau kwenye mikutano ya kampeni, kikisisitiza umuhimu wa kufanya siasa za kistaarabu ili kutekeleza dhana ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Onyo hilo limetolewa leo Jumatatu Septemba 8, 2025 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia mkoa huo, Ndele Mwaselela, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM jijini Mbeya.
“Chama tumejipanga kufanya kampeni bila matusi au kubeza utu wa mtu. Wagombea wanapaswa kueleza mambo mazuri ya Serikali ya awamu ya sita na kuhamasisha wananchi kuwapa kura za ndiyo au hapana kwa heshima,” amesema Mwaselela.
Aidha, amesema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mgumu zaidi kuliko chaguzi zilizopita, hivyo wagombea na mameneja kampeni majimboni wanapaswa kusimamia kwa makini mikutano na kuhakikisha wanashawishi makundi yote kuanzia nyumba kwa nyumba, daladala, bodaboda hadi vijiwe vya kahawa.
“Huu si mwaka wa kulala, upinzani ni mkali zaidi ya chaguzi zilizopita. Hivyo kila mmoja lazima afanye kazi ya kusaka kura bila kuchoka,” amesema.
Tathmini ya kampeni za urais
Mwaselela amesema mwitikio wa wananchi kwenye mikutano ya mgombea urais wa CCM, Rais Samia, umekuwa mkubwa, na ameonekana kuvunja rekodi ya frekwensi ya watu kujitokeza kwenye mikutano ya kampeni.
“Kila alikopita kumekuwa na uwingi wa watu kiasi cha kuhitaji ukaguzi wa kiusalama, jambo linaloonyesha ni kiongozi anayependwa na wananchi,” amesema.
Amebainisha pia kuwa Rais Samia ametoa ahadi zenye kugusa maisha ya wananchi, ikiwamo agizo kwa hospitali kutozuia miili ya marehemu kwa sababu ya madeni, jambo alilosema atalifanyia kazi ndani ya siku 100 za awali endapo atapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi Digital wamesema wanamuona Rais Samia kama kiongozi pekee mwenye kurejesha matumaini kwa Watanzania.
“Samia amegusa maisha ya wanyonge na amefanikisha miradi ya maendeleo mijini na vijijini. Oktoba 29 tutamzawadia kura zetu,” amesema Grace Mapunda, mkazi wa Mbeya.
Kwa upande wake, Mgombea ubunge wa jimbo jipya la Uyole, Dk Tulia Ackson, amesema ni wajibu wa wagombea kufanya kampeni za kistaarabu.
“Watanzania wameona kazi kubwa iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita. Sasa jukumu letu ni kushiriki kampeni na kusubiri Oktoba 29 tupige kura kwa heshima na amani,” amesema Tulia, akitangaza kuzindua kampeni zake rasmi Septemba 13, 2025 katika viwanja vya Hasanga, Uyole.