Mvumi. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja, ameahidi kupunguza mzigo wa michango ya shule kwa wazazi na walezi endapo chama hicho kitapata ridhaa ya kuunda Serikali.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 8, 2025 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Mpwayungu, Jimbo la Mvumi, Minja amesema michango inayotozwa shuleni imekuwa kero kwa wazazi, jambo linalopingana na kauli ya elimu bure.
“Tutatokomeza michango shuleni kama kweli elimu ni bure, michango ya maji, ulinzi au walimu yote haya hayana maana kama tunasema elimu bure. Tunataka watoto wasome kwa kuwa jukumu la Serikali,” amesema Minja.

Minja pia ameahidi Chaumma ikiingia madarakani akisema Serikali yake itajenga barabara za lami, akieleza kuwa miundombinu ya barabara ya sasa ni duni na kikwazo cha maendeleo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mkazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Devotha, akisema kukosekana kwa barabara za lami kumechelewesha maendeleo ya wananchi.
Aidha, Minja amesema Chaumma imejipanga kuboresha huduma za afya, ajira, makazi ya kudumu pamoja na upatikanaji wa maji ya uhakika.

Amesema chama hicho kitaiboresha sekta ya maji kwa ubinafsishaji ili visima vichimbwe maeneo yote na wananchi wapate huduma hiyo bila usumbufu.
Katika Kijiji cha Ndebwe, msafara wa Minja ulisimamishwa na wananchi, jambo lililomfanya asimame na kuwasalimia huku akisisitiza kuwa huu ni mwaka wa kufanya mabadiliko ya kweli.
Akizungumza katika Kata ya Kaelezi, Minja ameahidi Chaumma itaondoa kodi kwenye mbolea na mbegu, pamoja na kuboresha miundombinu ya maji kwa lengo la kuwawezesha wananchi kulima zabibu kama zao la kibiashara.
“Tutawekeza nguvu kwenye kilimo cha zabibu ili kuondoa umaskini. Dawa na mbolea tutaziondoa kodi, kila mtu aweze kulima zabibu,” amesema.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Mvumi kupitia Chaumma, Mwanga Chibango amesema kipaumbele chake kitakuwa ni ujenzi wa miundombinu, hasa shule na huduma za maji, akidai jimbo hilo limekosa mtetezi wa kweli kwa muda mrefu.
“Tuna shida ya maji. Kata ya Kaelezi ina shule moja pekee ya sekondari, jambo linalonyanyasa wananchi. Hali hii haiwezi kuendelea, tunahitaji kubadili historia ya Jimbo la Mvumi,” amesema Chibango.