CRDB yakamilisha uboreshaji wa mfumo, Dubai ukikaribia

Dar es Salaam. Benki ya CRDB Plc imekamilisha mchakato wa kuhamia katika mfumo mpya wa kibenki, hatua inayofungua njia ya kupanu huduma zake kikanda, ikiwamo kufungua tawi Dubai mwishoni mwa mwaka huu.

Benki hiyo ya Kitanzania, ambayo pia ina matawi tanzu nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imehama kutoka Mfumo wa Fusion Banking Essencewald (FBE) kwenda Temenos T24 kupitia kazi iliyochukua saa 72 mwishoni mwa wiki.

Mkurugenzi Mtendaji, Abdulmajid Nsekela akizungumza na Mwananchi  leo, Septemba 8, 2025 amesema mchakato huo ulikuwa muhimu kwa kuimarisha uwepo wa CRDB katika ukanda na kutoa huduma zinazofanana katika masoko yote.

“CRDB ni taasisi ya kimataifa, ikihudumia Burundi na DRC, huku tukikamilisha maandalizi ya kuingia Dubai. Huwezi kuhudumia wateja katika nchi hizi bila mfumo imara unaolinda taarifa za wateja na kurahisisha miamala. Hii ndiyo sababu kuu ya kuboresha mfumo wetu mkuu,” amesema.

Nsekela ameeleza kuwa, uhamisho huo ulihusisha kuhamisha taarifa za wateja wote waliopo pamoja na kuwezesha usajili wa wateja wapya ndani na nje ya Tanzania.

Amesema mfumo mpya utaondoa ulazima wa kwenda matawini, kwa kuwa huduma nyingi zitapatikana kwa njia za simu na kidijitali.

“Wateja wanapaswa kutarajia maboresho zaidi kadri tunavyoendelea, teknolojia hii inaturuhusu kuzindua huduma mpya kwa ufanisi zaidi,” amesema.

Mfumo wa Temenos T24, unaotumika kwa kiwango kikubwa na taasisi za kifedha duniani, unajumuisha shughuli kuu za kibenki, usimamizi wa uhusiano na wateja, na huduma za kidijitali katika jukwaa moja.

Nsekela pia amesema uboreshaji huo ulikuwa muhimu kwa kuwa, CRDB inahudumia wateja katika nchi zenye lugha, sarafu na mifumo ya sheria tofauti.

“Tanzania ina Kiswahili na Kiingereza kama lugha rasmi, Burundi hutumia Kifaransa na Kirundi, DRC ina Kifaransa na lugha nyingine za asili, Dubai inatumia Kiarabu na lugha za kimataifa. Popote pale, wateja watapata huduma kwa lugha wanayoichagua na kufanya miamala kwa sarafu wanayoipendelea,” amesema.

Aidha, Nsekela amewashukuru wateja kwa uvumilivu wa siku tatu za mchakato, ambazo baadhi ya huduma zilisitishwa kwa muda.

“Nawashukuru sana wateja wetu kwa ushirikiano wao katika kipindi hiki, naomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza kutokana na kusitishwa kwa muda kwa baadhi ya huduma,” amesema.

Akijibu maswali ya wateja waliobaini mabadiliko ya mizania ya akaunti na changamoto nyingine, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa CRDB, Bruce Mwile amesema tofauti hizo zilihusiana na uhamisho wa taarifa kati ya mfumo wa zamani na mpya.

“Wale waliobaini tofauti wafahamu kuwa, hili lilitokana na mchakato wa kuhamia kutoka mfumo wa zamani. Wateja wanapaswa kuelewa kuwa hatukuwa tunaboresha tu mfumo, bali tulihamia kwenye mfumo mpya kabisa unaotuwezesha kufikia viwango vya kimataifa na kushirikiana na taasisi za kifedha duniani,” amesema.

Nsekela pia, ameeleza kutambua mchango wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wadau wengine katika kufanikisha mchakato huo.

 Amesema uboreshaji huo ni sehemu ya mageuzi mapana ya CRDB wakati benki hiyo ikitimiza miaka 30 mwaka huu, ikidhihirisha mchango wake katika kipato cha wananchi na uchumi wa Taifa.

CRDB ndiyo benki kubwa zaidi nchini Tanzania, ikiwa na mali zenye thamani ya Sh19.7 trilioni hadi  kufikia  mwisho wa Juni 2025.

Hadi kipindi hicho, mkopo wa jumla ulikuwa umefikia Sh12.2 trilioni, ukiendeshwa zaidi na mikopo ya kampuni na ile ya wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs). Amana za wateja zilifikia karibu Sh14 trilioni.

Benki imeendelea kudumisha ubora wa mali zake, kwa kuwa na uwiano wa mikopo chechefu wa asilimia 3.05, kiwango kilicho ndani ya viwango vya kisheria.

Uwiano wa gharama kwa mapato ulipungua hadi asilimia 42.6 kutoka asilimia 45.4, hatua inayoonesha ongezeko la ufanisi.